UCHAGUZI WA YANGA GIZA NENE, SIMBA KAZI IPO
Unaweza kusema kwa sasa kuna wingu zito kuhusiana na hatma ya uchaguzi wa Klabu ya Yanga kutokana na kwamba haijfahamika ni lini utafanyika. Uchaguzi huo ni kwa ajili ya kujaza nafasi ya mwenyekiti ambaye awali alikuwa Yusuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe watatu ambao wote walijiuzulu.
Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Januari 13, mwaka huu, lakini ukasogezwa mbele kutokana na baadhi ya wanachama wa Yanga kufungua kesi mahakamani kupinga kufanyika kwake.
Kitendo cha wanachama hao kufungua kesi katika mikoa zaidi ya mitano kilisababisha Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuahirisha tarehe ya awali ya kufanyika kwa uchaguzi huo mpaka itakapotangazwa tena.
Kamati hiyo iliyopo chini ya mwenyekiti wake, Malangwe Mchungahela, walitangaza kuwa baada ya siku saba kuanzia Januari 14, wangeweka hadharani hatma ya uchaguzi lakini mambo yamekuwa tofauti na kamati imekuwa kimya. Siku zinazidi kusonga, bado Yanga haijafahamu uchaguzi wake na kujua hatma yake, klabu imekosa viongozi wake muhimu wanaohitajika kuikomboa klabu hiyo.
Umekuwa ni mtihani na kwa sasa Yanga ina hali mbaya na inahitaji msaada kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa hasa masuala ya fedha za mshahara na kipindi hiki cha ungwe ya pili ya Ligi Kuu Bara, lazima timu ipambane kweli kuhakikisha inatwaa ubingwa.
Kwa upande mwingine, nguvu kama hiyo inapungua kutokana na hali halisi ilivyo, hakuna viongozi wakuu zaidi ya wanaokaimu nafasi. Nikiwa kama mdau wa michezo, ningependa kuikumbusha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kulikumbuka suala hili na kuitangaza haraka tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo ili mbivu na mbichi zifahamike.
Nikienda upande wa pili, Jumamosi ya wiki hii Simba inatarajiwa kuvaana na Al Ahly ya Misri ukiwa ni mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Simba itakuwa na kibarua mbele ya Waarabu hao kutokana na kiwango chao kuonekana kuyumba katika michezo yake mitatu ambayo imecheza hivi karibuni. Utakuwa siyo mchezo rahisi kwao na ingawa Simba itataka kulipa kisasi kwa Waarabu baada ya mara ya mwisho kuoga mvua ya mabao kutoka kwa AS Vita Club ya DR Congo.
Timu hiyo inatakiwa kwenda kupambana kwa nguvu zao zote ili kupata pointi tatu muhimu na kuweza kurudisha imani kwa mashabiki wao ambao wamepoteza matumaini kwa sasa. Mashabiki ni moja kati ya watu ambao msimu huu wamekuwa bega kwa bega na timu yao hiyo, lakini ghafla wamekuja kukatishwa tamaa na tabia chafu za wachezaji wao ambazo mwisho wa siku zinaigharimu timu kwa kushindwa kupata matokeo chanya.
Mambo yaliyotea hivi karibuni kuhusiana na wachezaji wa Simba kudaiwa kutoroka kambini, kwa kiasi kikubwa mashabiki wameikatia tamaa timu hiyo kuweza kufanya vizuri dhidi ya Al Ahly. Kutokana na hali hiyo, ni vyema wachezaji Simba mkapambane kwa nguvu zote na kwa kupata ushindi wa nguvu mbele ya Waarabu ili kurudisha imani kwa mashabiki wenu ambao wamekata tamaa.
Ninaamini maandalizi ambayo amefanya Kocha Patrick Aussems, ni makubwa ambayo yataweza kuibeba timu hiyo. Kila kheri Simba, nendeni mkapambe na kuipeperusha vema bendera yetu ya Tanzania, najua siku zote hakuna kinachoshindikana endapo tu mkiweka bidii.
0 COMMENTS:
Post a Comment