NA SALEH ALLY
KOMBE la Mapinduzi limeanza kuchanganya huko Zanzibar. Unaona ule ushabiki wa watani Simba na Yanga umepamba moto sasa.
Achana na hivyo, ule upinzani pia wa Yanga, Simba dhidi ya Azam ambayo huwa ikiwapa presha au wakati mgumu wanapokaribia kukutana nao, unaona nao umeamka.
Ushindani wa tatu katika michuano hiyo ni Zanzibar dhidi ya Tanzania Bara. Kila upande unataka kufanya vizuri. Na hii ndio imekuwa raha ya michuano yenyewe.
Binafsi navutiwa nayo lakini naendelea kuwakumbusha waandaaji wawekeze, watafute wadhamini ili kuifanya iwe na mvuto zaidi kwa kuwa na zawadi za juu na hata timu kupata mapokezi, malazi na huduma bora zinapokuwa Zanzibar.
Maana tumeona, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amelalamika sehemu wanayolala.
Acha niingie kwa kile ninachotaka kukigusa. Ni kuhusiana na timu hasa Yanga na Simba ambao waliamua kutumia vikosi B kwa ajili ya michuano ya Mapinduzi.
Niliona Yanga zaidi walijikita katika kikosi B ambacho kilikuwa na mchanganyiko mdogo sana wa wachezaji ambao hucheza katika kikosi kikubwa cha Yanga.
Tena wengi wamekuwa wakipata nafasi mara mojamoja sana katika kikosi kikubwa. Hivyo si vibaya kusema wao walikuwa na kikosi cha pili.
Simba walikuwa na kikosi cha pili katika mechi ya kwanza. Pamoja na ushindi mkubwa, bado kocha Aussems aliamua kutumia kikosi cha kwanza katika mechi dhidi ya KMKM.
Kiufundi, Aussems alikuwa akitengeneza fitnesi katika kikosi chake kabla ya kuivaa JS Saoura ya Algeria katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Baada ya hapo ninaamini atakuwa akitumia kikosi cha pili zaidi kwa kuwa wachezaji hao hawatakuwa na nafasi ya kucheza hadi baada ya mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi.
Jambo hili la kutumia vikosi vya pili linaweza kuonekana kama si sahihi. Lakini kwa makocha wote wamekuwa sahihi kutokana na kukabiliwa na michuano mingi zaidi.
Hivyo wanalazimika kuwapumzisha wachezaji wao tegemeo na kuwapa nafasi wengine. Makocha wanafaidika kwa kuwa wale wanaowapa nafasi, pia wanapata nafasi ya kucheza na makocha nao wanaweza kuona vitu ambavyo huenda wasingepata nafasi ya kuviona kutokana na wachezaji hao kutokuwa na nafasi ya kucheza.
Sasa faida ya kocha inakuwa ni kwamba anagundua wachezaji kadhaa ambao kabla hakuwahi kuona uwezo wao kwa nafasi. Lakini kwa nafasi kama klabu inakuwa imejua mambo mengi yakiwemo thamani ya wachezaji ilionao.
Kwa maana ya kwamba mchezaji fulani anapaswa kuendelezwa, mchezaji fulani anapaswa kuachwa na hata kama itakapofikia suala la kutaka kufanya biashara na kumuuza mchezaji fulani, basi kunakuwa na yule ambaye ataziba pengo lake.
Hapa kitu kikubwa ni muendelezo, kwa kuwa tangu Yanga na Simba watumie vikosi vya pili. Kuna wachezaji ambao wameonekana kwamba wana nafasi ya kuwa msaada katika vikosi vyao.
Wachezaji hao hawakupata nafasi ya kucheza katika mechi za ligi na hata zile za Kombe la Shirikisho. Basi hii ni nafasi nyingine kuanzia kwenye mabenchi ya ufundi, wawaendeleze.
Nasema wawaendeleze kwa kuwa imekuwa ni ada wachezaji wanaofanya vizuri katika Kombe la Mapinduzi, wanaishia hapo na hawapati nafasi tena.
Kama makocha waliamua kujitoa na kuwatumia wachezaji hao, wawape nafasi angalau kidogokidogo katika mechi za ligi.
Yanga imeonyesha ina wachezaji zaidi ya watatu ambao ni chipukizi na wanahitaji kucheza, hali kadhalika kwa Simba ni hivyo. Vema nafasi iendelee kupatikana ili kuwajengea hali ya kujiamini makinda hao.
Kwao makinda, pia wanapaswa kuona wanatakiwa kuendelea na michuano ya Mapinduzi isiwe mwisho wao. Wajitume zaidi na zaidi ili kuwashawishi makocha. Kawaida katika soka, namba ni kunyang’anyana.
0 COMMENTS:
Post a Comment