January 16, 2019





Na Saleh Ally
KUNA mtu hataki uchaguzi ufanyike Yanga? Kama yupo sababu zake za msingi hasa ni zipi, aziweke hadharani!

Wanaotaka uchaguzi usifanyike Yanga, wanafanya hivyo kwa maslahi ya klabu au ni maslahi ya matumbo yao wakilenga zaidi kuendesha maisha yao.

Sote hatuwezi kukataa kwamba kuna kundi kubwa la watu wanaoendesha maisha yao kupitia Klabu ya Yanga. Wamo ndani ya Klabu ya Yanga wakiwa wanatumia sura za utiifu wakati mioyo yao ni ya uchumaji unaolenga kujishibisha binafsi.

Yanga inayoelezwa ni masikini hesabu zinaonyesha kuna upungufu wa mambo mengi ambao unafichwa na mwendo mzuri wa kikosi chake. Wapo wanaojificha kwenye chaka la ushindi wa Yanga.

Ndiyo maana unaona kwa mtu ninayegusa kama hivi suala la maslahi yao siwezi kuwa mtu mwema kwao. Lakini ndio kazi niliyoizoea, kukosoa kwa nia njema.

Kama mtaiacha Yanga iende mwendo huu, kumbukeni kuna baadaye na kesho. Yanga inaendeshwa kwa mwendo wa leoleo. Baada ya hapo, kuna wakati mwendelezo utakuwa mgumu na hapo ndio Yanga itaanza kuporomoka.

Huenda wengi wanaangalia leo, wanaona ni furaha na raha. Wanaona inawezekana na mambo yatakuwa hivi milele. Lakini haiwezi kuwa hivyo muda wote kwa kuwa hakuna mipango imara ya muda mrefu.

Yanga haina mwenyekiti wala makamu wake. Hata katibu mkuu pia ni mtu anayekaimu, nafasi ambayo ni ya ajira. Kwa klabu ambayo haina viongozi wote wa juu, lazima ujue kuna shida.

Suala la uchaguzi wa Yanga, ni muhimu sana. Huenda awali nilikuwa sikufurahishwa na namna TFF walivyolipeleka lakini kisayansi, Yanga lazima iwe na uongozi ili kwenda sahihi.

Kama itaacha watu wafanye wanavyotaka katika kila wanachoona sawa bila ya ushiriki wa viongozi sahihi, ni hatari kwa Yanga. Maana itafikia siku matatizo yanayojificha yameanza kujitokeza, kwa kuwa wanaoongoza si wenye dhamana ya wanachama, yaani hawakuchaguliwa, inakuwa rahisi kuruka.
Yanga ni kubwa, inataka kuwa na watu wanaoiongoza wawe wale waliopewa dhamana. Hii itawafanya wawe na hofu ya kufeli au kuwaangusha wanachama kwa kuwa waliowaomba kura kwa unyenyekevu na kuwaahidi.

Kwa sasa, nani ambaye anajiona anawajibika kwa wanachama? Kama mambo yakiharibika kila mtu atakuwa hajahusika na huenda akajitahidi kukwepa au kukaa kando.

Hivyo, Yanga kupata viongozi ni kufanya uchaguzi. Ndio maana nasisitiza, kwa wale wanaozuia uchaguzi kwa maslahi binafsi, basi waache kwa kuwa hakika wanatengeneza hofu na ugumu wa mambo.

Kama kuna wale wanaofaidika na Yanga kutokuwa na viongozi wa juu, wabadilike. Wajue wanaiangamiza Yanga kwa kuwa inaendeshwa bila ya kuwa na mipango ya muda mrefu.
Wanaotaka uchaguzi Yanga usifanyike, hawajionyeshi badala yake wanawatumia baadhi ya watu. Inawezekana hata wanaotumwa pia wasijue nia thabiti ya waliowatuma.

Kama ni maslahi ya Yanga, basi klabu hiyo iwe na viongozi ambao kwa kuwa baada ya kuingia watakuwepo kwa muda mfupi tu, itakuwa rahisi kuwapima na kuona wanafaa au la. Hivyo achieni uchaguzi ufanyike na Yanga ijiendeshe katika mpangilio utakaoangalia leo na baadaye.

Acheni watu wenye dhamana waingie na kuwa na hofu ya kupoteza au kutotimiza ahadi walizoahidi.

Aidha, hapa kuna funzo pia. Kwamba kumekuwa na watu wengi sana ndani ya klabu hizi kubwa wameweza kuidanganya jamii wakionyesha ni watu wanaosumbuka sana kwa ajili ya klabu. Lakini ndani yake ni hapana kwa kuwa mapenzi yao ni faida ya kile wanachokipata kutokana na wanachopata kwa maslahi yao.

Kila kiongozi atakuambia soka hakuna wanachoingiza. Lakini akifuatiliwa inagundulika ananufaika sana kupitia fedha za klabu.
Kuweni waugwana na onyesheni upendo ambao utafanana mnachokisema na kukitangaza katika jamii na kilicho katika mioyo yenu.

1 COMMENTS:

  1. Nadhani busara ni kuitisha uchukuaji form mpya baada ya hayo maridhiano maana kuna wanachama wengine waliogopa kuchukulia form tff kwa sababu waliona au walihisi ni kuvunja katiba kufanya hivyo. Kila kitu kianze upya ili fursa ziwafikie woye wenye uwezo wa kuongoza yanga

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic