February 4, 2019








Na Saleh Ally
TUNAKUBALIANA kwa pamoja kabisa kwamba uwezo wa Simba katika kiwango walichofikia bado wanahitaji kufanya makubwa ili kuhakikisha wanafikia sehemu kubwa.


Ndani ya mechi tatu za Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi, Simba wameshinda mechi moja na kushindwa mbili za ugenini.

Ukiangalia mechi waliyoshinda ni ile ya nyumbani ambayo walishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya JS Saoura lakini baada ya hapo wamekwenda kukutana na kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya AS Vita Club kwao DR Congo kabla ya kukutana na kipigo kingine kama hicho dhidi ya Al Ahly, vigogo wa Afrika.


Ndani ya mechi tatu, Simba wamefunga mabao matatu na kufungwa 10. Ndani ya mechi mbili, wamefungwa mabao 10 na hawajafunga hata moja, hapa ndipo sehemu sahihi ya kujipima.

Kujipima namna gani? Upimaji wa hapa zaidi ni ukweli sahihi ambao unatakiwa kwenda katika mioyo ya wahusika wakuu wakubali kwamba uwezo uliopo wa Simba katika kiwango walichofikia lazima unahitajika kuboreshwa.


Tatizo la Simba kupitia takwimu za mechi tatu zinaonyesha timu nzima ina matatizo kuanzia kocha hadi wachezaji wenyewe. Inaonyesha wazi hakuna muunganiko mzuri au sahihi lakini hata mtengeneza mifumo ambaye ni kocha, hana uzoefu na soka la Afrika katika kiwango alichofikia, nitarudi kwake.


Ukiangalia kikosi cha Simba, hakuna ubishi kwa kiwango cha nyumbani Tanzania wana timu nzuri na bora na hata wachezaji wengi walionao ni wale wanaotamba Afrika Mashariki na Kati.

Kwa kiwango cha Afrika na hasa hatua ya makundi ambayo ina "cream" ya Afrika kwa maana ya ubora upande wa klabu, hakuna ubishi kabisa kwamba bado na inatakiwa bao 10 ziwe somo.


Simba inaweza kufanya vema lakini haitafanya hivyo kama haitashinda mechi yake ijayo dhidi ya Al Ahly itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kipigo cha aina yoyote humnyong'onyesha mwanadamu kama ambavyo ushindi unavyoweza kumpa hamasa zaidi na zaidi. Simba wakishindwa mechi ijayo, basi nafasi hakuna.


Hivyo, wanatakiwa kushinda lakini tujiulize wanaweza kushinda kwa timu waliyonayo? Ndiyo wataweza kama watajifunza kupitia 10 za ugenini ndani ya mechi mbili na kama watashindwa kufanya hivyo hata nyumbani wataambulia pointi ziro.

Simba inapita shule, hiki ndiyo kipindi cha mpito kwenda kule ambako wanaamini walikuwa wanapataka. Mwekezaji Mohamed Dewji ‘Mo’ amesema anataka kuiona Simba inachukua ubingwa wa Afrika.




Kuchukua ubingwa Afrika sasa ndiyo imeanza mafunzo, inapita katika njia iliyo sahihi kwenda katika unachokitaka. Kwamba wanaona wanachokihitaji kinakuwaje ili kukipata.


Kuna mapungufu mengi ndani ya kikosi cha Simba, weledi ni wa kiwango cha chini sana na kuna wengi ambao wamelewa sifa na kujiona ni wakubwa.


Wachezaji hawataki kuelezwa, anayesema ukweli anaonekana ni mbaya wa klabu. Lakini ukweli ni kwamba, Simba haijawa na kiwango cha AS Vita au Al Ahly. Hivyo kufanya vema lazima ijue timu hizo katika kiwango hicho zinafanya nini na kipi.


Ukitaka ubingwa wa Afrika hakuna ubishi lazima uwe katika kiwango cha Ahly, TP Mazembe, AS Vita, Esperance na kadhalika. Je, Simba ipo huko, jibu ni hapana. Na kama Dewji hii ni ndoto yake, yuko sahihi kwa kuwa anayataka haya, sasa shule hiyo aanze kupitia mapungufu na kukata majani yaliyokauka.



Ukiwaambia Simba ubingwa wa Afrika Mashariki, wanajua, ubingwa wa Ligi Kuu Bara wanajua njia. Hawajawahi kuwa mabingwa wa Afrika, sasa huko ndivyo kulivyo.


Kulivyo vipi? Kunataka wachezaji makini, walio na nia ya kufanya vizuri na kutaka kufanikiwa. Wachezaji wa Simba wana tatizo hata kama watajisikia vibaya kuelezwa. Kwamba walionekana wameshindwa kufanya vizuri katika michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kutoka kambini na kwenda kwenye starehe siku moja kabla ya mechi.

Wakafungwa mabao 2-1 na Bandari ya Kenya, tena wakiwa wametangulia. Je, unafikiri nini kingefuatia dhidi ya Al Ahly. Simba inahitaji wachezaji wenye mawazo tofauti na hili Simba wanajifunza baada ya kufungwa mabao 10 katika mechi mbili tu.


Achana na wachezaji, kocha wao ni wa aina gani? Mechi mbili bao 10? Anacheza mfumo upi? Maana anawajua wachezaji wake, vipi hakujifunza kutokana na makosa na anakwenda kuruhusu mabao matano ndani ya dakika 45 dhidi ya Mafarao hao?


Patrick Aussems ni kocha mzuri, lakini leo Simba wanaona kwa kiwango kipi. Kwamba ubora wake una eneo fulani na kwa kiwango walichofikia na kama wakati mwingine watafikia, basi Simba wanahitaji kocha zaidi ya Aussems.

Mfano mzuri angalia JS Saoura, wamefungwa na Simba mabao 3-0. Waliporejea kwao wakatoka sare ya 1-1 na Al Ahly, kocha ametimuliwa. 


Hakika kuna mambo mengi sana ya kujifunza kwa kile kinachowatokea Simba na hasa kama utaamua kutuliza akili na kuimba mambo kishabiki.


Mashabiki wana haki hao ambayo ni kelele bila ya vipimo, lakini ukitaka kusikia raha ya mpira, upime kwa maswali na majibu kwa kubungua bongo, utaona ni shule iliyo tamu zaidi ya utamu.




2 COMMENTS:

  1. Mohamed Mo ni raha pekee iliyobaki ndani ya Simba kwa wanachama wake na mashabiki wa simba lakini tayari wameshapoteza matumaini juu ya uwezo hasa wa kocha wao na timu yake. Na kuna hatari kubwa simba kukosa nafasi ya kushiriki mashindano yeyote ya Africa mwakani kwani timu hii ya Simba ya sasa wasitarajie maajabu yeyote ya kutetea ubingwa wake wa ligi kuu bara wacha tusubiri na tuone.

    ReplyDelete
  2. Siku zote tumeimba.. tumepaza sauti wee kuwa #Simba bado haijawa timu bora.. Aina ya wachezaji, morali ya wachezaji, aina ya kocha wao!!
    Na zaidi ya yote aina ya viongozi walio nao...!!
    Ila muhimu kujua ni kuwa #Simba itabadilika na kuwa imara zaidi.. Ni suala la muda lakini timu itazidi kuimarika mara dufu..!!

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic