February 22, 2019


MCHAKATO wa Klabu ya Simba kuelekea kwenye mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo unaelekea kuzuri na taarifa ni kuwa ule uwekezaji wa Mohamed Dewji ‘Mo’ sasa nao upo katika hatua nzuri.

Mo alikubali kuwa mwekezaji kuelekea katika mabadiliko hayo ambapo ilielezwa kuwa yuko tayari kuwekeza Sh bilioni 20 kwa kununua hisa na kuwa sehemu ya wamiliki wa klabu hiyo kwa asilimia 49 huku asilimia 51 ikimilikiwa na wanachama.

Habari za uhakika kutoka klabuni hapo ni kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi huu kuna uwezekano wa kiasi cha fedha kuwa kimetolewa kutoka katika bilioni 20 ambazo aliahidi kuwekeza ikiwa ni mwendelezo wa kuiwezesha klabu kuingia katika mabadiliko hayo.

Mara baada ya uchaguzi mkuu wa klabu uliofanyika Novemba, mwaka jana, viongozi sita waliteuliwa kutoka upande wa wanachama wakaungana na wawakilishi wa Mo ambaye ni mwekezaji na kuunda bodi ya wakurugenzi ambayo ndiyo inayosimamia masuala yote ya Kampuni ya Simba.

Kiongozi mmoja wa juu ndani ya Simba, hivi karibuni alinukuliwa akisema mchakato huo wa mabadiliko upo katika hatua za mwisho kwa kuwa kuna mambo ya kiofisi hayajakamilika.

“Kuna taratibu ambazo zilikuwa hazijakamilika lakini kwa sasa mambo yanaonekana kwenda sawa na mwishoni mwa mwezi huu, Mo anaweza kutoa sehemu ya fedha kutoka katika zile bilioni 20 za uwekezaji wake klabuni kwa ajili ya kuunda kampuni na maendeleo ya klabu.

“Vikao mbalimbali vya bodi vimekuwa vikiitishwa kwa ajili ya kukamilisha mchakato huo na mambo yanaonekana kwenda vizuri,” alisema mtoa taarifa huyo kutoka klabuni hapo. Aidha, Championi Ijumaa lilimtafuta Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Simba, Crecentius Magori kuzungumzia suala hilo lakini hakupokea simu na alipotumiwa ujumbe mfupi pia hakujibu.

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic