KOCHA wa timu ya Lipuli, Seleman Matola amesema amefunga jumla hesabu za ushindi wake mbele ya Mbao,alioupata kwenye Uwanja wa Samora kwa kushinda bao 1-0 sasa kinachomuumiza kichwa ni bao la mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo alilofungwa kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Taifa.
Makambo aliifunga Lipuli dakika ya tisa bao ambalo liliwanyima pointi tatu Lipuli na kuondoka mikono mitupu, sasa Matola ameamua kuanza kuinoa timu yake kuimaliza Yanga.
Matola amesema kuwa hesabu kubwa ni kuona anaimaliza mapema Yanga kwa kuanza kuwapa mbinu wachezaji wake kuelekea mchezo wao wa Yanga.
"Majalada ya ushindi wetu dhidi ya Mbao tumeachana nayo sasa akili zetu ni mchezo wetu dhidi ya Yanga, hakuna atakayetuzuia kwa sasa kupata matokeo kwani nimewasoma vilivyo wapinzani wangu lazima nilipe kisasi.
"Nalikumbuka lile bao la yule mshambuliaji wao Makambo, sasa kila nikifikiria namna tulivyopoteza pointi nakosa usingizi nafikiria tu namna ya kuimaliza, hesabu zangu ni kuona nabaki na pointi tatu," amesema Matola.
Yanga itaifuata Lipuli mwezi Machi 16 mchezo utakaopigwa Uwanja wa Samora.
0 COMMENTS:
Post a Comment