March 7, 2019





Na Saleh Ally, Antalya
MICHUANO ya Kombe la Mataifa Afrika maarufu kama Afcon kwa upande wa vijana chini ya miaka 17 inafanyika nchini kwetu Tanzania, mwezi ujao.

Kwa taarifa yako, tokea taifa letu lipate uhuru, hii ndio michuano mikubwa zaidi kufanyika nchini kwetu. Ni Kombe la Mataifa Afrika na hapo, tutakuwa na nafasi nyingine kama kuomba michuano mikubwa zaidi na hasa kama tutaandaa vizuri.

Michuano hii inakuja kwetu kama sehemu kubwa ya kujifunza lakini kuanzisha kwa usahihi kutaka kuhakikisha tunaingia katika soka la ushindani na kuondokana na maisha ya kichwa cha mwendawazimu.

Wakati tunaingia kwenye kujifunza, lazima tutataka kufanya vizuri kwa maana ya kuhakikisha timu yetu ya vijana, kikosi cha Serengeti Boys kinafanya vizuri licha ya kwamba kinakutana na vigogo.

Timu za Afrika Kaskazini na Magharibi ndio vigogo wa michuano hiyo kwa kuwa wameanza zamani kuamka na kujua umuhimu wa soka la vijana, tunajua leo linawafaidisha.

Vizuri tuanze kuelezana mapema kwamba, haitakuwa rahisi hata kidogo na lazima tuendelee kuwaamini tunakwenda kushindana na haitakuwa lelemama.

Uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutafuta nafasi ya Serengeti Boys kushiriki michuano ya Uefa Assist inayoendelea hapa jijini Antalya ni la msingi na msaada mkubwa sana.

Serengeti Boys ipo hapa katika michuano hiyo tena tayari imeanza michuano hiyo juzi kwa kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Guinea.

Baada ya mechi hiyo, niliona mijadala kadha wa kadha ikiwemo ile ya kutia moyo lakini ile inayokatisha tamaa kama ilivyo ada yetu kwamba timu yetu ni dhaifu sana!

Hii ilinishangaza kidogo ingawa nimekuwa mzoefu na mwendo wetu wa Kitanzania. Kila mmoja ana elimu ya juu katika kulaumu hata katika kile kinachopaswa kutoa maneno ya kutia moyo.

Katika mechi hiyo, Serengeti Boys walianza vibaya sana katika uchezaji hasa kipindi cha kwanza. Wakaweza kuweka nidhamu ya ukabaji ambayo hakika iliwasaidia sana kumaliza wakiwa nyuma kwa bao 1-0 tu.

Kipindi cha pili, timu hiyo ilifunguka na kuwapa wakati mgumu Guinea ambao kimaumbo na ikiwezekana kiumri ni wakubwa. Mwisho mechi hiyo ikaisha kwa Guinea kushinda kwa bao 1-0.

Mechi iliyofuata jana wameibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Australia na hakuna anayesema kitu kwa maana ya kuonyesha wameshinda. Kitu cha kulaumu tunakifanya kinakuwa kikubwa kupita kiasi.

Kutaka Serengeti Boys ishinde ni uzalendo lakini mimi ningependa kuona kama inafungwa, basi ifungwe tu na hasa kama itakuwa imefanya makosa ili makosa wapate nafasi ya kuyaona na kuyafanyia kazi.

Kama itakuwa na uwezo wa kushinda, basi ishinde lakini kwa makocha bado kutatakiwa kuwa na jicho la pili kulingana na hali yenyewe.

Kufungwa na Guinea kutakuwa na faida kubwa kwa vijana hao kuliko ushindi. Kuna makosa ambayo watayaona na kadhalika, mfano suala la nguvu licha ya kwamba wenzao wana maumbo makubwa lakini lilionekana kuwasumbua vijana wetu.

Katika soka kuna namna ya kucheza na kila aina ya mtu, mfano mwenye nguvu na kasi na mpira wa kuachia badala ya kusubiri mgusane. Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo atakuwa kaona kitu na anajua jambo la kufanya ni lipi.

Hatupaswi kulumbana na kuonyesha lawama na maneno ya kishabiki, badala yake tuchangie kwa lengo la kusaidia kwa maana kama utakuwa umeona kosa, basi zungumza katika njia ambayo unaona kutakuwa na msaada.

Timu inayofungwa bao 1-0 nayo inapaswa kulaumiwa kwa maneno rundo ya kukatisha tamaa? Tena ni vijana ambao wameishi maisha tofauti kwa maana ya akademi bora ukilinganisha na wale wa Afrika Magharibi au Afrika Kaskazini?

Tanzania sasa imewaona Uganda, Angola na Nigeria wanavyocheza. Hawa itakutana nao katika Kundi A la Afcon na kutakuwa na nafasi ya kujua nini cha kufanya.

Jana kikosi kizima cha Serengeti Boys kilikuwa uwanjani kuwashuhudia Nigeria, pia Waganda wakicheza mechi zao. Maana yake kutakuwa na jambo ambalo wamejifunza na hakuna ubishi kwamba watakuwa wamefaidika.

Waunge mkono vijana wetu, kosoa kwa nia ya kujenga na wape moyo wakati huu wakijaribu kutafuta ubora.

Kumbuka, hawa bado ni watoto na unapozungumza maneno usifikiri ni sawa na unapowakosoa Taifa Stars au kama ni klabu basi Simba, Yanga au timu nyinginezo. Yapo ya kuzungumza vizuri ili waelewe na kuendelea kupambana na tuwaunge mkono.










0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic