UONGOZI wa timu ya Lipuli umesema kuwa malengo makubwa kwa sasa ni kuona wanabeba kombe la Shirikisho ambalo wanashiriki kwa sasa hivyo hawana cha kupoteza mbele ya Singida United kwa mchezo wa leo utakaochezwa Uwanja wa Samora.
Singida United ni miongoni mwa timu ambayo ilitinga hatua ya fainali ya kombe la Shirikisho enzi za Hans Pluijm itakaribishwa na Lipuli ikiwa chini ya kocha Fred Minziro baada ya kocha mkuu Dragan Popadic kufungishiwa virago.
Kocha wa Lipuli, Seleman Matola amesema kuwa wachezaji wake wapo tayari kiushindani na wana morali kubwa ya kupata matokeo mbele ya wapinzani wao Singida United.
"Mchezo utakuwa mgumu hasa ukizingatia ni hatua ya mtoano, na kwa namna ilivyo kwa sasa kila timu hesabu zake ni kubeba ubingwa ukizingatia kwa sasa hakuna bingwa mtetezi kama ilivyokuwa kwa Mtibwa Sugar ambao wametolewa nasi tutafanya hivyo.
"Kila kitu kinawezekana na kwenye mpira chochote kinaweza kutokea, tutakuwa nyumbani tukicheza na wapinzani wetu tunawatambua vema wapinzani wetu hivyo tutapambana kupata matokeo chanya ili kusonga mbele, tunaamini tutapata matokeo chanya ambayo yatatufanya tusonge hatua ya nusu fainali na mwisho kubeba kombe kabisa," amesema Matola.








0 COMMENTS:
Post a Comment