Na Saleh Ally
WATANZANIA tumeingia kwenye gumzo la moja ya nchi ambazo zimefanya vizuri katika msimu wa 2018/19 wa Ligi ya Mabingwa Afrika hadi sasa.
Tanzania ni kati ya nchi zenye timu, kati ya zile nane bora za Afrika kwa kuwa Simba imefanikiwa kuingia katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa bara hili upande wa klabu.
Kwa historia au rekodi, hii si mara ya kwanza kwa timu ya Tanzania kufikia katika hatua hiyo lakini kwa hesabu za ubora kwa kuwa kipindi hiki soka la Afrika lina mabadiliko makubwa, lazima tukubali haikuwa kazi nyepesi kufikia hapo.
Tanzania ni yetu sisi ndio maana hakuna Mwanasimba anaweza kujisifia kwamba mafanikio hayo ni nguvu ya kundi moja. Wengi wameshiriki kufikia kilichotokea ingawa ukianza na uongozi, wachezaji na makocha wa Simba wanastahili pongezi.
Pongezi hizo, nyingi zaidi pia zitatakiwa kwenda kwa mashabiki ambao walifanya kazi kubwa ya kuipa moyo timu yao kukimbilia kwenye mafanikio ambayo sasa wote wanajivunia.
Wakati Simba wakipambana kuishangilia timu yao, lazima walikuwa na hofu ya kuzodolewa na watani wao Yanga lakini bado walikuwa wanajua wanaipigania Tanzania, ndiyo maana unaona mafanikio ya sasa ya Simba hayajawa ya Simba pekee, badala yake ni taifa zima.
Huu ni wakati mwingine sasa, tukianza na mashabiki wa Simba, Yanga, Azam FC na timu nyingine kuungana kwa kipindi hiki cha wiki moja kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha timu yetu ya taifa inakuwa na nguvu za kutosha kuwaangusha jirani zetu Waganda.
Taifa Stars inatakiwa kuifunga Uganda kwa aina yoyote ilimradi ibebe pointi tatu muhimu zitakazoiwezesha kusonga mbele na kuingia kwenye kioo kipya cha mpira wa Afrika. Kumbuka mechi itachezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, si mbali na muda umeisha.
Tunaamini Cape Verde itaidondosha Lesotho ambayo itakuwa ugenini, hivyo Stars ikishinda maana yake itakuwa imesonga mbele na kuingia kucheza Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), hii itakuwa ni safari ya pili.
Mara ya mwisho, Stars ilicheza michuano hiyo mwaka 1980 ikifanyika nchini Nigeria. Angalia kizazi cha mpira cha sasa na mwaka huo, utagundua waliopo si zaidi ya asilimia 20 ambao waliishangilia Stars ikiwa nchini Nigeria.
Kizazi cha sasa kimekuwa kikisikia mambo kwa hadithi tu, yote ni yale ya kusimuliwa na itakuwa jambo la faraja na kujivunia kuiona Taifa Stars ikishiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza wakati wa kizazi chetu.
Hii ni nafasi nyingine muhimu, kama namna ambavyo wikiendi iliyopita Simba walivyokuwa wakipigania nafasi yao na ya Tanzania. Safari hii ni mikono na mwili mzima unapaswa kupambana kupigania jambo hili.
Hili ni jambo muhimu na Tanzania kushinda na ikafanikiwa kufuzu, rekodi mpya itakuwa imeandikwa kwa kizazi chetu. Hivyo kikubwa kabisa ni kufuta Usimba na Uyanga kwa muda, ushabiki wa timu nyingine, tuungane na kuwa timu moja.
Lazima tuungane ili kuishinda historia inayoifanya Tanzania iwe nchi ya simulizi linapofikia suala la kuelezea mafanikio ya soka. Maana inaonekana mafanikio yalikuwepo enzi zile, za watu wale kama akina Leodegar Tenga na wenzao na sasa hakuna lolote.
Huu ndio wakati wetu, tusahau ushabiki wa klabu na kuungana pamoja kama taifa bila ya kujali kuna hadithi gani na kwa pamoja iwe kulipigania taifa letu.
Wachezaji wataingia uwanjani wakijua wanakwenda kupambana kwa ajili ya taifa lao nasi tuwe tunafanya hivyo kuwapa nguvu na kuwanyong’onyeza Waganda ambao ni majirani zetu, hivyo thamani yao haiwezi kufanana nasi.
Tunajua Waganda wameshafuzu na huenda wangependa kutufunga kwa ajili ya heshima tu. Sisi tunahitaji heshima zaidi ya kusonga mbele na kuingia kwenye Afcon, jambo ambalo tunaliweza.
Tuonyeshe sisi ni wazalendo, tunalipenda taifa letu kwa kupenda maendeleo yake. Kama kulikuwa na tofauti ziwekwe nyuma, zitarudishwa baadaye kupambana kuzimaliza au vinginevyo, sasa kazi iwe ni Taifa Stars kuzufu kwenda kucheza Afcon, michuano itakayofanyika nchini Misri.
Hakika tunaotaka Afcon, tukifuzu itakuwa sehemu nyingine ya afya ya soka ya nchi yetu kwa kuwa tutaheshimika na kufuatiliwa na mabadiliko ya ubora yataanzia hapo kwa kuwa hata sisi tutakuwa tumetengeneza nguvu ya kujiamini kwa mara nyingine.
Weka pozi ushabiki wa klabu zetu iwe Yanga, Simba, Azam, Pamba na kadhalika halafu twendeni Taifa pamoja kwa ajili ya kulitetea taifa letu ambalo linaundwa na sisi wenyewe.
0 COMMENTS:
Post a Comment