YANGA NA TFF WAFIKIA HATUA HII JUU YA UCHAGUZI
VIONGOZI wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), juzi Jumatano walikutana na kujadiliana juu ya utata uliojitokeza kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Yanga ambao awali ulisimamishwa.
Uchaguzi huo wa kujaza nafasi zilizo wazi katika klabu hiyo ikiwemo ya mwenyekiti iliyokuwa ikishikiliwa na Yusuf Manji, ulipangwa kufanyika Januari 13, mwaka huu lakini uliahirishwa baada ya baadhi ya wanachama kufungua kesi mahakamani kuupinga.
Baada ya juzi kukutana, imeelezwa kuwa wamekubaliana kuanza upya mchakato huo wa uchaguzi. Chanzo makini kimesema katika kuanza huko upya, wagombea watalazimika kuchukua fomu upya katika zoezi ambalo litaanza mara tu baada ya kutangazwa.
“Kuhusu utata wa wanachama wenye sifa ya kupiga kura, wanachama walioandikishwa katika leja ya klabu wataruhusiwa kupiga kura bila ya kujali kama wana kadi za kitabu au za benki,” kilisema.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa kama mambo yataenda kama ilivyopangwa basi uchaguzi huo unatazamiwa kufanyika Machi 24, mwaka huu. Alipotafutwa Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Siza Lyimo kuzungumzia hilo, alisema: “Baada ya kukutana, kesho (leo) Ijumaa ndiyo itatangazwa mchakato mzima wa uchaguzi huo utakavyokuwa.”
0 COMMENTS:
Post a Comment