April 7, 2019


MWINYI Zahera ameweka wazi kwamba anahitaji mastaa wapya sita wa maana Yanga msimu ujao.

Lakini habari ya kushtua ni kwamba kama kamati ya kuchangia Yanga chini ya Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu, Antony Mavunde itapata mkwanja wa kutosha mastaa zaidi ya 15 watakwenda na maji mwezi ujao.

Ligi Kuu ya Bara inamalizika mwezi ujao na ndiyo pilika za usajili zinaanza rasmi wakati ambao Zahera atakwenda Ulaya kuiandaa timu yake ya Taifa ya DR Congo kwa ajili ya Afcon.

Habari za ndani ambazo Spoti Xtra imezipata ni kwamba, wachezaji takribani 13 ambao mikataba yao inayoyoma hawataongezwa kama mambo yakiwa mazuri.

Mmoja wa vigogo wa Yanga alidokeza kwamba hawataongezwa kutokana na uwezo wao kuwa wa kawaida lakini klabu iliwavumilia kutokana na ukata na kutokuwa na mbadala.

Wachezaji hao ambao mikataba yao inaelekea ukingoni ni pamoja na Juma Abdul, Mwinyi Haji, Papy Tshishimbi, Thabaan Kamusoko, Deus Kaseke na Emmanuel Martin ambaye yupo kwa mkopo Ruvu Shooting.

Wengine ni Yohana Nkomola ambaye yupo kwa mkopo African Lyon, Juma Mahadhi ambaye pia ni majeruhi wa muda mrefu. Pia wamo Mrisho Ngassa, Amissi Tambwe, Ibrahim Ajibu (anarudi Simba), Yahaya Akilimali na Haruna Moshi Boban. Mbali na hao yupo kipa Beno Kakolanya ambaye tayari ameshajitoa Yanga hivyo nafasi yake ipo wazi.

Chanzo makini kimeongeza kwamba Zahera amewaambia viongozi kwamba wachezaji hao asilimia kubwa hawawezi kuisaidia Yanga msimu ujao kwa kuwa anataka watwae ubingwa.

Habari zinasema kwamba Zahera amepanga kusajili wachezaji wengine wakali kutoka nje ya Tanzania ili kuitengeneza Yanga yenye ushindani na amewaambia viongozi hilo lisipofanyika hataendelea na kazi msimu ujao.

Kocha huyo alikuwa jijini Dodoma wikiendi hii kushirikiana na kamati kuhamasisha kuichangia Yanga kwa njia mbalimbali ambapo lengo ni kupata Sh.Bil 4 na ushee kwa ajili ya kusuka Yanga mpya.

Alipoulizwa na Spoti Xtra baada ya mechi na Ndanda iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, Zahera hakutaka kuweka wazi wachezaji anaowaacha msimu ujao kwa madai kwamba bado hajapata uhakika wa fedha.

“Siwezi kukwambia namwacha nani na nani au wangapi, kwa vile bado sijapata uhakika wa fedha, nikishajua ndio nitapata uhakika,” alisema Zahera.

Lakini akasisitiza kwamba; “Nafikiria kusajili wachezaji wapya sita kwenye nafasi mbalimbali. Nikipata pesa nitasajili mabeki wawili, viungo wawili na mastraika wawili wa maana sana, nataka timu ya ushindani.

“Lakini hayo yote yatategemea na nguvu ya fedha ambayo itatokana na hii michango tunayochangisha,” aliongeza Zahera ambaye timu yake inaongoza msimamo wa ligi ingawa anakabiliwa na ushindani mkubwa wa Simba yenye viporo saba.

3 COMMENTS:

  1. "Si hoja kuzaa, hoja kulea", walisema waliotutangulia

    ReplyDelete
  2. umakini unahitajika pia maana kupanga ni kuchagua, unaweza kusajili wachezaji lakini changamoto ni uendelevu wa hao wachezaji (how to sustain them in terms of salary and upkeeps) Yanga na Simba hazihitaji kuendelea kuwa timu za matukio rather timu za mikakati

    ReplyDelete
  3. All the best, umoja wa wanayanga ndio mafanikio ya malengo hayo, "shine wanajangwani na mashabiki wa mpira, tumuunge mkono Zahera" Timu ni yetu sote wala sio zahera na kamati peke yake tu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic