April 2, 2019


MATAJIRI wa Jiji la Lubumbashi, TP Mazembe Aprili 6, wanakuja machinjioni katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Vigogo hao wa soka la Afrika wanakuja maalum kwa ajili ya kuvaana na Simba katika mechi ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mchezo huu ni muhimu kwa kila timu kutokana na mshindi kwenda nusu fainali. Timu hizi zimefika hapa baada ya kupenya katika hatua ya makundi. Vita ya timu hizi mbili inapaliliwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji wa vikosi vyote viwili. Cheki jinsi itakavyokuwa wachezaji watakavyokutana baina ya timu hizi mbili.

UNKORO VS AISHI MANULA

Huku Manula kule Muonkoro. Kazi wanayo. Mounkoro raia wa Mali ndiye kipa namba moja wa Mazembe wakati Manula yeye ndiye kila kitu katika lango la Simba. Makipa hawa watakuwa na vita ya kila mmoja kutotaka lango lake lifungwe, watakuwa bize kuokoa michomo itakayoelekezwa kwake na mwisho watataka kutoka wakiwa na ‘clean sheet’.

ARSENE ZOLA VS EMMANUEL OKWI

Okwi ni mbaya akitokea wingi ya kulia au kushoto kutokana na vile atakavyopangwa. Okwi atakuwa na vita kali wakati akikabiliana na beki wa kushoto wa Mazembe, Zola. Wakati Okwi akiwa na sifa hizo anakutana na Zola ambaye ni hatari katika kukaba pia kupandisha mashambulizi ndiyo maana anakuwa chaguo la kwanza mbele ya Mganda Joseph Ochaya. Katika nafasi yao kutawaka moto.



KABASO CHONGO VS CLAYTOUS CHAMA

Chama mara mbili aliibeba Simba mgongoni mwake katika michuano hii mikubwa. Alifunga bao lililowapeleka makundi kisha akapiga msumari wa mwisho uliowafikisha robo fainali, kiufupi Mzambia huyu ni mashine hatari kwa Simba.

Katika mechi hii Chama ambaye kwenye mfumo wa 4-3-3 hutumika kama mshambuliaji msaidizi atapambana na Chongo ambaye ni kitasa hasa kwenye ukuta wa Mazembe. Hawa jamaa bhana kila mtu anamjua mwenzake kwa sababu wote ni Wazambia.

KELVIN MONDEKO ZATU VS JOHN BOCCO

Beki Kevin Zatu ana mabao mawili katika michuano hii aliyoyafunga katika ushindi wa kishindo wa 8-0 dhidi ya Club African. Zatu mwenye miaka 23 katika dakika zote 90 za mechi hii atakuwa na shughuli ngumu ya kupambana na Bocco, ambaye huwa siyo rahisi kukubali kushindwa na beki.

ISSAMA MPEKO VS MEDDIE KAGERE

Kagere anasifika kwa uwezo wa juu wa kufunga mabao, kutoa asisti lakini pia kasi na kupambana mwanzo mwisho. Beki Mpeko ndiye amepewa kazi maalum ya kumzuia Kagere asifanye vurugu katika mechi hii. Je ataweza? Dakika 90 pekee ndizo zitaonyesha nani ameshinda.

MICHE MIKA VS JAMES KOTEI

Hili eneo ndipo moto utawaka. Miche ndiye kiungo matata zaidi nchini DR Congo ambaye atapambana na Mghana mgumu James Kotei,katika kugombania madaraka ya kati ya uwanja. Wote hawa ni viungo chuma na kama mmoja akishinda basi timu yake inaweza kushinda.

CHRISTIAN KOFFI VS JONAS MKUDE

Hapa ni vita ya Mtoto wa Morogoro, Mkude na mzaliwa wa Dabou, Ivory Coast. Hawa watachagiza ile vita ya Miche na Kotei eneo la katikati ya uwanja. Mkude kwenye mechi hii anaingia kwa nguvu kubwa kwani mechi ya mwisho dhidi ya AS Vita hakuwepo.

ELIA MESCHAK VS TSHABALALA

Kwa sasa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye anayeaminiwa katika beki ya kushoto ya Simba akimuweka pembeni Asante Kwasi. Tshabalala au Zimbwe yeye kibarua chake kwenye mechi hii ni kupambana na Elia ambaye ni hatari akitokea kulia.

Elia anaunda safu kali ya ushambuliaji ya Mazembe akishirikiana vizuri na wenzake kina Mputu na Kalaba. Katika mechi tano zilizopita za Ligi ya Mabingwa hajacheza moja tu tena hakuwepo kabisa.



JACKSON MULEKA VS PASCAL WAWA

Mzee wa miaka 33, Wawa atakuwa anapambana na katoto chenye miaka 21, Mulekwa. Licha ya kuwa na utofauti wa umri baina yao lakini hii ni vita kali mno ikichagizwa na mafanikio ya kila mmoja. Mulekwa ndiye mfungaji hatari nje ya Mputu ndani ya Mazembe.

Katika michuano hii ana mabao manne. Wawa yeye analingia uzoefu wake wa kucheza mechi za kimataifa, hivyo hatakuwa na wasiwasi sana, mmoja kati ya hawa jamaa wawili lazima mechi ikiisha akameze dawa za kutuliza maumivu kutokana na watakavyopelekana.

TRESOR MPUTU VS ERASTO NYONI

Hawa wote ni mafaza katika klabu zao. Mputu ana heshima ya kutupwa ndani ya Mazembe wakati Nyoni amejijengea jina Tanzania. Vita yao haitakuwa na mambo mengi kutokana na umri wao, kuzidi miaka 30.

Ingawa wanaonekana miaka kwenda lakini ni hatari wanapokuwa uwanjani, Mputu ndiye kinara wa mabao katika Ligi ya Mabingwa kwa upande wa Mazembe akiwa nayo manne wakati Nyoni yeye ni hatari katika kuwazima washambuliaji ambao ni hatari.

RAINFORD KALABA VS ZANA COULIBALY

Kadiri siku zinaenda ndivyo Coulibaly anaonyesha kwamba alistahili kuvaa uzi wa Simba, japo mwanzo alibezwa. Katika mechi hii Mbukinafaso huyo atakuwa na kazi moja tu ya kumzuia winga tereza Kalaba asifanye mambo kwa upande wao.

Mzambia Kalaba ni hatari katika kutengeneza nafasi, ana akili ya mpira na mzuri katika kumtikisa beki yeyote atakayekutana naye. Lakini yote kwa yote Shabaan Dilunga na Erasto Nyoni wamewaambia mashabiki wa Simba kwamba wanajua cha kufanya na hawajawahi kufeli Taifa. Wamewasisitiza kwamba wajae kwa wingi Taifa Jumamosi washuhudie jinsi Manzembe anavyokufa.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic