MAZEMBE WAONDOKA DAR NA HOFU KUBWA
NAHODHA wa TP Mazembe, Rainford Kalaba, amesema kuwa kitendo chao cha kushindwa kupata bao lolote katika mchezo wa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Simba kimewaweka katika nafasi mbaya ya kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Timu hizo zitarudiana Jumamosi hii mjini Lubumbashi na kama Simba ikipata bao moja ugenini, wenyeji watalazimika kutafuta mabao mawili ili kusonga mbele. Simba ikipata sare yoyote ya mabao itasonga mbele kwa faida ya mabao ya ugenini. Itatupwa nje ikiwa itafungwa tu.
Kalaba alisema kuwa matokeo ambayo waliyapata katika mechi hiyo, siyo mazuri kwao kwani yamewaweka katika mazingira magumu katika mchezo wa marudiano.
“Tungetoka sare ya bao 1-1 tungekuwa na faida ya bao la ugenini, lakini matokeo haya ya bila kufungana siyo mazuri kwetu. Simba wanaweza kuja kwetu na wakapata sare jambo ambalo linaweza kutuondoa mashindanoni, kwa hiyo inatubidi kwenda kujipanga vilivyo kuhakikisha tunapata ushindi katika mchezo huo.
“Simba ya sasa ni nzuri sana na ina uwezo mkubwa wa kupata ushindi sehemu yoyote ile ukilinganisha na ile ya mwaka 2011 ambayo ilikuwa na Mbwana Samatta ambayo hapa tuliifunga 3-2 na kwetu tukaifunga 3-1,” alisema Kalaba.
0 COMMENTS:
Post a Comment