TAMBWE AWAPA UJANJA SIMBA JUU YA TP MAZEMBE
Baada ya juzi Jumamosi, Simba kushindwa kuutumia vema uwanja wake wa nyumbani dhidi ya TP Mazembe, mshambuliaji wa Yanga, Mrundi, Amissi Tambwe amewapa mchongo wachezaji wa timu hiyo wa kuwamaliza wapinzani wao hao nyumbani kwao.
Simba itarudiana na TP Mazembe, Jumamosi ijayo huko Lubumbashi nchini DR Congo katika mchezo wa pili wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya juzi Jumamosi kutoka suluhu jijini Dar.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Tambwe alisema kuwa Simba wanatakiwa kujipanga vilivyo kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zote ambazo watakumbana nazo katika mchezo huo wa marudiano.
Alisema, TP Mazembe wanapokuwa katika uwanja wao wa nyumbani huwa si timu ya mchezo na ambayo huwa na hila nyingi kuanzia nje mpaka ndani ya mchezo, kwa hiyo wanapaswa kujipanga juu ya hilo.
“Waanze mara moja maandalizi yao kwa ajili ya mchezo wa marudiano, kwani TP Mazembe wakiwa kwao hawafai hata kidogo, wana figisufigisu nyingi, kwa hiyo ni vizuri wakajipanga kukabiliana nazo ili waweze kufanya vizuri,” alisema Tambwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment