April 11, 2019











Na Saleh Ally, Liverpool
MJI wa Liverpool ni kati ya miji “mirembo” ya nchini England na aina yake ya ukaaji zaidi ni watu wanaopenda ushirikiano kwa kuwa asilimia kubwa wameunganishwa na mchezo wa soka.



Idadi ya wakazi bila ya wageni ni takribani milioni 2.3 lakini ni mji wenye mchanganyiko wa watu wengi kwa maana ya asili na una mgawanyiko wa maeneo, yakiwemo yale yaliyotulia sana lakini kuna sehemu zilizochangamka kwelikweli.



Niko hapa na usiku wa kuamkia jana, nilishuhudia mechi Liverpool FC wakiivaa FC Porto katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0. Lakini bado kuputia Spoti Xtra tunaweza kujifunza mengi kupitia mji wa Liverpool na soka.



Kuwepo kwa mashabiki wengi wa soka kutoka katika klabu mbili kubwa maarufu zaidi za Liverpool na Everton FC, kunaufanya mji huu kuwa na harufu ya kisoka zaidi.

 

Hii inatokana na kuwa hivi; biashara nyingi zinazoendeshwa katika eneo hili, zinakuwa zinautegemea mchezo huo hasa kwa kuwa kwa msimu mmoja tu kunakuwa na mechi zaidi ya 35 za Ligi Kuu England kwa maana zile za nyumbani za klabu hizo mbili.



Everton wanakuwa na mechi 19 za nyumbani hali kadhalika Liverpool na hivyo kulifanya eneo la Meryseside kuwa busy muda wote kwa kuwa viwanja hivyo haviko mbali kwa utofauti wa eneo kwa kuwa unapokuwa juu ya Uwanja wa Anfield, basi utauona vizuri kabisa Uwanja wa Goodon Park wa Everton.


Hii inaufanya mji huu kuzitengemea sana klabu hizo kama chanzo cha biashara kwa ile ila ya mvuto na uletaji wageni.


Jina Liverool kuchukuliwa na klabu ya Liverpool imekuwa sehemu nyingine ya kuufanya mji huu kuwa maarufu na wenye mvuto zaidi.



Mvuto huo umetambaa duniani kote kwa wale wanaoipenda klabu hiyo, hivyo kufanya kuwe na idadi kubwa ya wageni ambao wangependa kufika kwenye mji huu na kuishuhudia klabu hii.


Wageni wengi wanaofika hapa Liverpool, asilimia hadi 68, huulizia kuhusiana na klabu ya Liverpool na wangependa kununua bidhaa zenye lebo ya klabu hii.



Asilimia 56 hununua vifaa au bidhaa zenye jina la Liverpool hata lingekuwa la mji huu tu kwa kuwa wana mapenzi na klabu ya Liverpool.


Hii ni sehemu ya kuonyesha namna gani Liverpool imesaidia soko la Liverpool kama jiji lakini bado Everton ambayo iko chini kwa msaada huo lakini ni sehemu ya mafanikio hayo kutokana na ile mechi yao kuwa moja ya derby maarufu duniani.


Zinapokutana Everton na Liverpool ni sehemu ya gumzo la mji huu, England, Ulaya na duniani kote kwa wale wapenda mpira kwa kuwa kuna historia ndefu kuhusiana na timu hizi mbili za soka ambazo karibu kila sehemu zinazungumzwa.


Katika hoteli niliyokuwa nimefikia ya Holiday Inn, asilimia 35 ya wageni walikuwa wamefika kwa ajili ya mpira na wanatokea sehemu mbalimbali zikiwemo zile za hapahapa England.


Wako mashabiki wa Liverpool ambao wanaishi nje ya Liverpool na walitaka kuiona ikipambana katika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya FC Porto kwa kuwa waliamini ni timu isiyoaminika, hivyo ni lazima waipe nguvu.




Kawaida, wakazi wengi wa England hushangilia timu za maeneo yao lakini ukubwa wa Liverpool unaifanya kuwa moja ya klabu chache zenye mashabiki wengi hata nje ya mji wa Liverpool.


Hapa unagundua nguvu kubwa ya Liverpool hata ndani ya England, tofauti na klabu nyingi. Angalau Manchester United na Arsenal ni kati ya timu zinazounda idadi kubwa ya watu wanaoweza kuziunga mkono hata wanaopokuwa nje ya mikoa husika.


Mashabiki wa Liverpol, wengi wameiambia Spoti Xtra kwamba ni klabu wanaoyoiheshimu kama klabu lakini pia kutokana na heshima ya kuwaendeshea maisha kwa kuwa ni klabu inayogawana nao.

Wanaamini Liverpool FC inagawana nao maisha kwa maana ya upendo. Wanaona ni klabu ambayo mashabiki wanafanya biashara na kuendesha maisha yao kupitia klabu hiyo inapokuwa na mechi au wakati wote wakiuza vifaa vya klabu hiyo.



Liverpool imeajiri zaidi ya vijana 500, hawa unajumuisha wenye ajira ya moja kwa moja na wale hulipwa kwa ajira maalum kunapokuwa na mechi au hafla maalumu.


Liverpool ni tegemeo la uchumi la mji wa England na sehemu ya maisha ya watu wa mji huu. Hauwezi kuishi hapa bila ya kuitaja Liverpool au kuhusiana nayo hata kwa kuisikia kwa wingi kuhusiana na habari zake.

Nyumbani Tanzania mambo bado yako tofauti kidogo, huenda klabu zinachukuliwa kama sehemu ya maisha ya soka na hayawahusu wengine ambao hawapendi au kufuatilia soka.


Hii inatokana na ubunifu mdogo wa wahusika walio ndani ya klabu husika. Kama wangekuwa wabunifu zaidi, ushabiki, upendi wa dhati na maisha kujumuika kwa watu na klabu zetu kubwa zenye watu hasa Yanga na Simba ungekuwa mkubwa sana na faida kubwa kwa klabu na watu wenyewe.

 

Kila mmoja angeishi akipata chake kutokana na kutegemeana na kingekuwa cha haki na mafanikio. Hii maana yake, kila upande ungeyaka kuutunza mwingine na kufanya maisha yaendelee kwa upendo wa juu kabisa kutoka kila upande.



Bado hatujachelewa, muda unaturuhusu. Lakini tunaakiwa kukubali kujifunza kama ambavyomimi nimefika hapa kama mwakilishi wa Spoti Xtra lakini nimeona ninachojifunza, nigawane na wasomaji wetu ambao wengi wao ni wapenda mpira, viongozi wa klabu hizi wakiwemo lakini ninaamini wako wanaopenda kujifunza na wanaweza kubadilika kupitia hili na kubadilisha mambo hapo baadaye.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic