April 11, 2019



Na Saleh Ally
TUWAACHE wale wanaoendelea kujadili penalti iliyopigwa na nahodha wa Simba, John Raphael Bocco na kuinyima Simba ushindi wakati ikiivaa TP Mazembe katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Hatua ya Robo Fainali.

Halafu tuijadili kitaalamu mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya bila mabao, kwa kuwa kulikuwa na uwezekano wa Simba kuibuka na ushindi na kuendeleza rekodi yake ya kuwa hatari na kiwembe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Sare hiyo imetengeneza ugumu katika kikosi cha Simba lakini hakuna uhakika kama Simba imetolewa. Badala yake, maandalizi yao kwenda katika mechi hiyo ya jijini Lubumbashi ndiyo yatakayoamua nini kitafuatia, kusonga mbele au kutolewa.

Simba wana kila sababu ya kusonga mbele kwa kuwa TP Mazembe ni wakubwa lakini Simba ni wazuri na wana uwezo na imejionyesha katika mechi yao hiyo ambayo wengi walitarajia isingewezekana hata hiyo sare.

TP Mazembe haijawahi kupoteza Tanzania lakini haikuwahi kutoka sare pia. Ushindi finyu iliifunga Yanga bao 1-0 lakini tayari ilishaichakaza Simba na wazi inapokutana na timu za Tanzania, ushindi ni uhakika “ndani nje”.

Safari hii mambo yalikuwa tofauti na tunapaswa kujifunza jambo, Simba wanapaswa kupongezwa kwa kubadili mambo kutokana na namna walivyopiga hatua, leo timu kama Mazembe inalazimika kupoteza muda ili kujiokoa na kipigo.

Hili pekee ni jambo la kujifunza na kulifanyia kazi. Kwamba leo TP Mazembe imefika Tanzania na imeingia hofu, halafu wakati wa mchezo inaonekana kweli ilistahili kuwa na hofu kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na Simba.

Kocha Mkuu wa Mazembe, Mihayo Kazembe ambaye alikuwepo katika mechi ya Mazembe ikiziadhibu Simba amekiri kwamba Simba imeonyesha kiwango cha juu sana na walijipanga kwa kuwa walitarajia hilo kutokea.

Wanaamini pia mechi yao dhidi ya Simba jijini Lubumbashi haitakuwa rahisi, hivyo watajipanga sawasawa ili kupata ushindi. Maana yake, ubora wa Simba sasa ni gumzo barani Afrika.

Angalia takwimu zilizotolewa na wataalamu wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kuhusiana na mchezo huo wa juzi, Simba wanaonekana walikuwa bora zaidi ya TP Mazembe. Kwani kwa umiliki, Simba ilikuwa na 56% na Mazembe ambao ni wakubwa wakabaki na 44%.

Kawaida, Mazembe licha ya kucheza ugenini walikuwa na kiwango cha juu cha umiliki karibu kwa mechi zote dhidi ya Yanga na Simba na hofu ilikuwa kwa wenyeji hata kuliko wageni, jambo ambalo linaonyesha Simba wameibadilisha Tanzania kutoka nchi ya soka la watu wenye hofu, hadi wanaojiamini kwa yeyote kuchapwa anapotua Dar es Salaam.

Simba ilipiga mashuti 12 langoni, mawili yakalenga lango na Mazembe wakapiga kumi matatu yakilenga. Hapo utaona kujiamini kwa Simba kulikuwa juu zaidi, ingawa kuna la kujifunza kwamba suala la kulenga ni muhimu zaidi kwa kuwa Mazembe wamelenga mara moja zaidi yao.

Simba walipata kona nne dhidi ya moja, na kwenye faulo Simba wakazidi, maana walikuwa na 23 dhidi ya zile 22 za Mazembe na unaona hakuna tofauti kubwa lakini kufikisha 22 maana yake Mazembe walikuwa na hofu.

Kwa mujibu wa takwimu za Caf, timu tano bora katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018/19 ni Al Ahly ya Misri, Esperance ya Tunisia, TP Mazembe ya DR Congo, Al Merreikh ya Sudan na AS Vita ya DR Congo pia.

Hesabu yako pigia hapo, katika timu hizo tano bora zaidi barani Afrika. Msimu huu tatu zimecheza kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Simba ya Tanzania ambayo imetoa vipigo kwa mbili na sare kwa moja.

Simba ilipoteza kwa Vita na Ahly, kila moja ikikubali kipigo cha mabao 5-0, lakini Dar es Salaam ni habari nyingine na tayari Simba imetengeneza hali ya kujiamini Dar es Salaam na sasa inapaswa kujifunza namna ya kuwa bora ugenini ili kutengeneza ubora pacha utakaoifanya kuwa bora zaidi.

Timu tatu za Tano Bora Afrika, zimeshindwa kutamba Dar es Salaam, tumewaona AS Vita na Mazembe wakipoteza muda. Lakini Ahly wakipokea kipigo na kuchezewa soka, hili si jambo la kulichukulia kama bahati nasibu au yale maneno ya kishabiki kwamba waliwekewa dawa vyumbani.

AS Vita hawakuingia vyumbani na wakafungwa, Mazembe hawakuingia vyumbani wakabahatika na sare na sote tumeona. Kipi kingine kitokee ili tuamini mpira wa Tanzania unabadilika tena na Simba wanahusika.

Simba wanapaswa kuigwa ili kuyafanya mabadiliko haya kuwa ya Tanzania yote na si Msimbazi. Kama nilivyosema awali, viongozi wa Yanga, Azam FC na klabu nyingine mliangalia hili la Simba kama chachu badala ya zile hadithi za mitaani ambazo hazina mashiko.

Simba kama itabadilika yenyewe, hautakuwa msaada wa kutosha kwa soka hapa nchini. Badala yake tunapaswa kuwa na timu imara Ligi ya Mabingwa na imara Kombe la Shirikisho Afrika na zote ziwe kiboko ya wageni na matata zinapokuwa ugenini.

Jipangeni, umizweni kwa lengo nanyi la kutaka kubadilika na kutaka kujenga kitu imara kama walivyo Simba leo, kesho muweze kuwa imara na msaada wa mabadiliko ya mpira wa Tanzania.

4 COMMENTS:

  1. Umenena brother very well spoken.

    ReplyDelete
  2. hii ndio ilipaswa kuwa motto kwa wachambuzi wetu sio tunaishia maneno yaliopitwa na wakati. CAF wanaiita timu kama Simba ni outsider, yaani asiyewahi kuchukua kombe wachambuzi wetu wanaita under dog.Huwezi fika mbali na mtazamo finyu kama huo big up sana Saleh.

    ReplyDelete
  3. mwandishi na mchambuzi leo umeona mbali sana

    ReplyDelete
  4. Kwa mara ya kwanza umekubali ukweli usemwe. Hongera mwandishi

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic