April 19, 2019





WIKIENDI iliyopita tulishuhudia Simba ikiondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kufungwa mabao 4-1 na TP Mazembe.

Katika mchezo huo wa marudiano wa hatua ya robo fainali, Simba ilikuwa inahitaji sare ya mabao au ushindi ili isonge nusu fainali kutokana na mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar kumalizika kwa suluhu.

Simba ilianza vizuri kwa kupata bao la mapema dakika ya pili tu ya mchezo kupitia kwa Emmanuel Okwi, baada ya hapo wengi tuliamini kwa Simba kufuzu nusu fainali kunawezekana.

Kwa namna ambavyo niliushuhudia ule mchezo, niliona Simba wakianza kulinda lango lao mapema tu baada ya kupatikana kwa bao hilo kitu ambacho kiliwaponza.

Siku zote nimekuwa nikisema kwamba njia rahisi na nyepesi ya kujilinda ni kushambulia, lakini Simba walikuwa wakijilinda kwa kukaribisha mashambulizi langoni mwao kutokana na kutoshambulia.

TP Mazembe walianza kulishambulia kwa kasi lango la Simba na hatimaye mashambulizi yao ya mara kwa mara yakawafanya kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao 2-1.

Kipindi cha pili TP Mazembe wakamaliza kazi kwa kufunga mabao mengine mawili na kuifanya kuondoka na ushindi wa mabao 4-1 uliowapeleka nusu fainali.

Licha ya kwamba Simba imeondolewa robo fainali, lakini tunatakiwa kuwapongeza kutokana na kufika hatua hiyo ambayo ni kubwa na imevuka malengo yao ya msimu huu.

Kama unakumbuka, Simba iliweka malengo ya kufika hatua ya makundi msimu huu, lakini imevuka na kuishia robo fainali.

Kilichobaki kwa msimu ujao ni kuona mwakilishi wetu, wawe Simba, Yanga, Azam au timu yoyote ile iweze kufika mbali zaidi ya hapo kutokana na kwamba Simba imefungua njia na kuonyesha kwamba katika soka lolote linawezekana.

Baada ya Simba kuondolewa kwenye michuano hiyo, sasa Serengeti Boys ndiyo wamebeba jukumu la kuwapa furaha Watanzania ikiwa inashiriki michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (Afcon U17) inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Kuanza kupigwa mchezo wa kwanza si mwanzo mzuri, hivyo kazi kubwa ni kupambana kwa mechi Iliyobaki kupata matokeo chanya ili kufikia malengo ya kufika mbali.

Ikumbukwe kwamba, mechi ambayo imebaki mkononi ni moja dhidi ya Angola baada ya kupoteza mchezo wa pili mbele ya Uganda kwa kufungwa mabao 3-0 na mnatakiwa kushinda ili kusonga mbele.

Kwenye mpira hakuna kinachoshindikana endapo mtapambana kutafuta matokeo chanya ndani ya uwanja na kubadili mbinu baada ya ile ya kwanza kushindwa kuleta ushindi.

Tumeona namna ilivyokuwa mchezo wa kwanza na wa pili, vijana walijitahidi kupambana ila mwisho wa siku walizidiwa mbinu na kupoteza.

Nikukumbushe tu kuwa, Serengeti Boys iliyopo Kundi A kwenye michuano hiyo, Jumapili iliyopita ilifungwa mabao 5-4 na Nigeria katika mchezo wa ufunguzi uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, pia wakafungwa mabao 3-0 na Uganda mchezo wa pili.

Hakuna haja ya kukata tamaa hasa kwenye michuano hii, nafasi tunayo na kazi kubwa ni kwa wachezaji wenyewe kuamua kupambana.

Benchi la ufundi lifanyie kazi makosa waliyoyaona na kuwapa moyo vijana kupambana kwa ajili ya taifa hali itakayosaidia kufanya vizuri.

Naona wengi wameanza kujadili mambo yao na kukosoa kikosi, muda bado unaruhusu, kikubwa sapoti iwe kubwa mwanzo mwisho.

Mashabiki ni muda wenu sasa kuongeza ile hamasa na kujituma kuishangilia timu yetu ya taifa kwani kufanya hivyo kutaleta hamasa kwa wachezaji kuongeza nguvu ya kupambana uwanjani.

Wachezaji msiwaangushe mashabiki, fanyeni kila linalowezekana katika kutafuta matokeo chanya, hakuna kazi nyingine mnayotakiwa kufanya mkiwa uwanjani.

Mnatakiwa kucheza kwa umoja na siyo kutegeana, siku zote umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

Kama safu ya ushambuliaji inafanya kazi kwa kutegeana, hii haileti picha ya timu kamili, bali ubinafsi, hali hiyo inapaswa iachwe mara moja kama ipo kikosini.

Upande wa safu ya ulinzi, nimeona kama vile haina ushirikiano mzuri katika kufanya maamuzi, wahusika ambao ni benchi la ufundi nadhani hili mmeliona, lifanyieni kazi mapema kabla ya mchezo ujao wa hatua ya makundi.

Mafanikio yamebebwa kwenye miguu ya wachezaji, hivyo pambaneni kurejesha furaha kwa mashabiki na taifa kwa jumla.

Namna mtakavyosonga kwa sasa ni kwa mtindo wa hesabu kali na dua, kwa kuwa kundi A lipo wazi ukianza kuangalia kwa nafasi ambayo ipo.

Nigeria mwenye pointi sita tayari ameshafuzu, huyu hayupo kwenye mahesabu, sasa kazi ipo kwa Angola na Uganda ambao wote wana pointi tatu.

Endapo Serengeti Boys itafanikiwa kuifunga Angola kwa mabao yaziyozida matano, kisha matokeo ya mchezo wa Nigeria ikamshindilia mabao manne Uganda matumaini yatafufuka na kupata nafasi ya kusonga mbele.

 Ubaya wa mpira hata kama nafasi ya kupata matokeo ni ndogo huwa tunapaswa kuwa na imani kubwa ambayo ndiyo nguzo ya mafanikio. 

Kila la kheri, Serengeti Boys, pambaneni Taifa linawategemea.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic