April 19, 2019



MAFANIKIO katika soka ni hatua ambayo inahitaji muda mrefu kupitia kuanzia kwenye mchakato ambao upo na kama ukifuatwa kwa umakini katika kila njia ni rahisi kupata kile ambacho unakihitaji, vinginevyo hakuna njia mbadala.

Tumeona namna wawakilishi wetu kwenye michuano ya kimataifa, Simba wakiondolewa katika hatua ya robo fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na TP Mazembe, wikiendi iliyopita.

Mpaka Simba inaondoshwa, ilipitia mabonde na milima, mwisho wa siku ikavuka vikwazo vyote vilivyokuwa mbele yao na ikavuka malengo.

Kwa hatua ya Simba kutinga robo fainali wanahitaji pongezi kubwa na kupewa heshima yao kwa namna walivyopambana kuipeperusha Bendera ya Tanzania kwenye michuano ya kimataifa.

Simba wajanja na wana akili ya kutumia fursa kwani wameua ndege wawili kwa jiwe moja na matokeo yake wamepiga hatua kubwa kwenye soka na kuipeperusha kwa ufasaha bendera yetu ya taifa.

Nasema ndege wawili kwa jiwe moja ni mpango ambao wamekutana nao kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf), baada ya kufanyika maboresho kwenye michuano hii mikubwa Afrika, dodo likawadondokea na hawakufanya ajizi, wakapambana hadi wamefikia robo fainali.

Zamani ilikuwa mpaka kufika hatua ya makundi unatakiwa kupitia hatua zisizopungua tatu, lakini safari hii ukianza hatua ya awali, kisha hatua ya kwanza, unatinga makundi.

Jambo lingine ni mfumo wa uendeshaji wa Klabu ya Simba ambao umefanyiwa maboresho na msimu wa kwanza tu umeleta matokeo chanya kwa timu kufika mbali. Kwa hapo nawapa pongezi zangu binafsi Simba.

Pia kutolewa robo fainali na timu kubwa ya TP Mazembe mnapaswa mjue kwamba mmeanza kupiga hatua kama ilivyo kwa mtoto anaanza kutambaa kisha ndiyo kutembea.

Benchi la ufundi linapaswa pongezi licha ya makosa ya kiufundi yaliyowaponza pale DR Congo ikasababisha mkatwisha mzigo wa mabao 4-1 licha ya kupambana, lakini bahati haikuwa kwenu.

Tatizo kubwa lililowasumbua Simba ni kushindwa kukaba kwa umakini wa hali ya juu. Baada ya bao la mapema walilopata waliona kama kazi wamemaliza kitu ambacho kikawa hatari kwao.

Hapa sio kosa la beki tu ama kiungo, ni timu nzima imekuwa chini, inatakiwa ifanyiwe kazi, wachezaji wanaufuata mpira ila wanashindwa kuumiliki kwa wakati.

Hili linatakiwa lifanyiwe kazi na benchi la ufundi ili kama Simba itapata fursa ya kuiwakilisha nchi msimu ujao ilete ushindani wa kweli na wenye tija zaidi kwa kuwa uzoefu wameshaupata.

Hatua ngumu na kubwa zinabebwa na kujiamini pamoja na mipango ambayo itapangwa hatua ijayo kila kitu kitakuwa sawa.

Muda wa kujipanga ni sasa na inawezekana kujipanga na kwa sasa iwe ni kwa ajili ya msimu ujao.

Timu nyingine ni muda wa kujifunza na kupambana usiku na mchana kutafuta mafanikio kwa ajili ya soka letu, ni wakati wetu kuwa wa kimataifa.

Mwisho kabisa nigeukie kwenye michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) chini ya miaka 17 ambayo inaendelea jijini Dar es Salaam huku wawakilishi wetu wakiwa Serengeti Boys.

Serengeti Boys imeanza michuano hiyo kwa kufungwa mabao 5-4 na Nigeria katika mchezo ambao ulikuwa wa ufunguzi uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Kipigo hicho kisiwavunje moyo, licha ya kupoteza tena mbele ya Uganda kwa kufungwa mabao 3-0, mechi ya mwisho dhidi ya Angola ndiyo imebeba mafanikio yenu ili muweze kufikia malengo ya kutinga Kombe la Dunia.

Timu nne zitakazotinga nusu fainali kwenye michuano hii moja kwa moja zinajikatia tiketi ya kucheza Kombe la Dunia kwa vijana wa umri huo itakayofanyika Brazil Septemba, mwaka huu.

Kikubwa ni benchi la ufundi kukaa na wachezaji na kuzungumza nao kwa kina kuwaelekeza wapi walikosea na wanatakiwa kufanya nini ili wasirudie yale makosa ambayo yanaonekana ni ya mara kwa mara.

Imani yangu ni kwamba, Serengeti Boys inaweza kufika mbali kwenye michuano hii na kututoa kimasomaso kwani nimewaona vijana wetu wapo vizuri sana, hivyo hesabu zenu iwek kupata mabao mengi kesho mkiomba Nigeria nao washinde kwa mabao mengi.

Niwatakie kila la heri katika maandalizi yenu, pia niwaombe Watanzania tujitokeze kwa wingi uwanjani kuwasapoti, kwa sasa hatuna kisingizio tena kwa sababu serikali yetu pendwa imeondoa viingilio, hivyo tunaingia uwanjani bure.


1 COMMENTS:

  1. Tatizo la Simba inahitaji wachezaji wazawa wenye kujitambua pia.kwani Simba ni fursa na wanapaswa kuifukuzia na kuitumia ipasavyo naona bado wamelala. Wakati Simba ikielekea kukiimarisha kikosi chake kwa msimu ujao hasa kwa malengo ya kuja kuleta ushindani zaidi kimataifa ningewaomba wachezaji wazawa kutoka kila kona ya Tanzania wenye malengo ya dhati ya maisha kupitia mpira na wenye moyo wa kupambana kuichangamkia fursa ya Simba kwani mnahitajika.kama kweli kauli ya haji Manara yakwamba kuna maombi zaidi ya 100 ya wachezaji wanaotaka kujiunga na Simba basi mimi naona maombi hayo ni kidogo kwani hayo ni maombi ya wachezaji wa Daresaalam tu. Zanzibar kuna vijana wenye uwezo mzuri wa mpira ila ni waoga wa kubadilisha mazingira.Tunataka vijana wa kazi kutoka mwanza,Wa Arusha,wa Kigoma,wa Kagera,wa Mara nakadhalika nakadhalika wenye kujitambua kama wachezaji na kufukuzia fursa na kama Manara angesema angalau kuna maombi 1000,elfu moja ya wachezaji wanaotaka kujiunga na Simba basi kidogo ingependeza.Ni shida kwa wachezaji wetu kukosa mawakala wa uhakika wa ndani wenye kuzingatia maslahi zaidi ya baadae ya mchezaji na badala yake huwa wanaeka tamaa mbele kitu ambacho kimewafanya vijana wengi kushindwa kwenda kwenye klabu ambazo zingewatangaza zaidi au kuwaongezea uwezo wao wa kazi.Ukimuangalia kagere sio kwamba ana maajabu yaliyojificha. Kilicho wazi juu ya uwezo wa kagere ni kujituma kwa nguvu zake zote kwa muda wote akiwa uwanjani. Ninachowaomba viongozi wa Simba ni kutokuwa na muhali wa kuachana na mchezaji ambae haoneshi dalili ya kubadilika. Suala la kuoneana muhali na mtu kwa kuhofia lawama ndicho kitu kinachotufelisha watanzania. Waswahili husema ukupigao ndio ukufunzao na vipigo walivyovipata Simba ugenini mara hii klabu bingwa Africa nadhani ni fundisho tosha ya nini cha kufanya mwakani ili kuwa na ushiriki wa mafanikio zaidi ya msimu huu kama watapata fursa ya kuiwakilisha nchi kimataifa.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic