"SIAMINI kama timu niliyoifunga mabao 5-0 nyumbani leo inatinga hatua ya robo fainali, haya ni maajabu ya mpira sikutarajia jambo kama hili ila mpira una matokeo ya ajabu sana," alisema kocha wa AS Vita Florent Ibenge baada ya kupoteza mchezo wa mwisho mbele ya Simba uliochezwa Uwanja wa Taifa.
Safari ya Simba, haikikuwa nyepesi kama ambavyo wengi walifikiria mwanzo ulikuwa mzuri ila kati uchungu ulizidi kiasi ambacho wengi walianza kuikatia tamaa, ila mwisho wa siku wametinga hatua ya robo fainali.
Rekodi zao namna zilivyo chungu na tamu kimataifa zipo hivi:-
Imepigwa nje ndani
Hatua ya awali Simba walianza kwa mbwebwe baada ya kuwatungua Mbabane Swallow kutoka Eswatin nje ndani, walianza Uwanja wa Taifa kwa kuwafunga mabao 4-1 kabla ya kumaliza kazi ugenini kwa kuwafunga mabao 4-0 na kufanya wakusanye jumla ya mabao 8-1.
Wafungaji kwenye michezo hiyo miwili walikuwa ni John Bocco dk ya 7, na dk ya 32, Meddie Kagere dk ya 83 na Clatous Chama dk ya 90.
Mkali wa pasi za mabao
Chama ndiye kinara wa pasi za mabao kwa Simba ambapo mpaka sasa ametoa pasi tatu za mabao akifuatiwa na Emanuel Okwi mwenye pasi mbili za mabao kimataifa.
Chama ametoa pasi za mabao kwa Kagere, Okwi na Mkude huku Okwi akitoa pasi zote kwa Kagere.
Fundi wa kutupia
Kinara wa kutupia ndani ya Simba ni Kagere ambaye ametupia mabao sita mpaka sasa, ambapo mabao 5 amefunga kwa kutumia mguu wa kulia na bao moja amefunga kwa kichwa.
Anayemfuatia ni Chama mwenye mabao 5 ambayo manne amefunga kwa mguu wa kulia na bao moja kwa mguu wa kushoto.
Wamepindua meza kibabe
Michezo mitatu Simba wamepindua meza kibabe baada ya kufungwa ugenini, walianza kupoteza mchezo mbele ya AS Vita kisha wakapokea kichapo mbele ya Al Ahly kwa jumla ya mabao 10 ambapo kila mchezo walifungwa mabao 5-0.
Mchezo wa marudio Uwanja wa Taifa hakuna aliyeambulia pointi Simba walipindua matokeo kwa kuanza kuwamega Al Ahly bao 1-0 kabla ya kukata tiketi kwa AS Vita baada ya ushindi wa mabao 2-1.
Wamepinduliwa meza kigaidi
JS Saoura waliposhuka bongo, Simba haikuwaacha salama iliwatungua mabao 3-0, ngoma ilikaza hasa baada ya wao kuwafuata Algeria walipinduliwa matokeo na kushangaa namna mpira ulivyo wa ajabu kwa kukubali kipigo cha mabao 2-0.
Vipigo vya kutisha
Mechi mbili mfululizo Simba walikuwa wanahaha kutafuta pa kutokea kwani walipokea vichapo vyenye ujazo, wakiwa na maumivu ya kuchapwa mabao 5-0 dhidi ya AS Vita, Al Ahly nao waliwaongezea furushi la mabao 5-0. Simba inakuwa ni timu iliyofungwa mabao mengi kwenye kundi D.
Mabao ya usiku
Chama ameweka rekodi yake baada ya kutupia mabao matatu ya usiku ambapo alianza kufanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Mbabane dk ya 90, kwenye mchezo dhidi ya Nkana alifunga bao dk ya 88 na kwenye mchezo dhidi ya AS Vita alifunga dk ya 90.
Mabao 2 ya usiku yaliivusha Simba hatua moja kwenda nyingine, alilofunga dhidi ya Nkana liliivusha Simba hatua ya makundi na lile dhidi ya AS Vita limeipeleka Simba hatua ya robo fainali.
Fundi wa penalti
Bocco ambaye ni nahodha alipewa jukumu la kupiga penalti ambazo wamezipata ambapo mpaka wanatinga hatua ya robo fainali wamepata mabao 2 kwa njia ya penalti.
Penalti ya kwanza ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Mbabane baada ya Okwi kuchezewa rafu Bocco alizamisha nyavuni dk ya 32 na penalti ya pili ni dhidi ya Nkana FC baada ya Kagere kuchezwa rafu, Bocco alifunga dk ya 73.
Kituo kinachofuata
Baada ya kutinga hatua ya robo fainali kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya AS Vita kituo kinachofuata ni hatua ya robo fainali ambapo hesabu za kocha mkuu Patrick Aussems ni kuona kikosi kinapata matokeo chanya kwenye hatua hiyo.
"Mpira una maajabu yake, wapinzani wetu walitufunga mabao 5-0 kwao nasi tuewafunga mabao 2-1 tumesonga mbele, kama ambavyo awali nilisema kundi lipo wazi hesabu zetu ni kuona tunasonga mbele zaidi mpaka kufika fainali," alisema Aussems.
Walipo kwa Sasa
Simba tayari wameshaanza safari kukamilisha dakika 180 za hatua ya robo fainali ambapo tayari dakika 90 za mwanzo wamekwama kuibuka na ushindi nyumbani, huku fundi wa Penalti, Bocco akikosa kuzamisha wavuni penalti kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya TP Mazembe.
Cha kufanya nini
Wachezaji na benchi la ufundi kwa sasa wanatakiwa wajue ushindani ni mkubwa na mchezo wao unaofuatwa ni mgumu la wasiwe na papara watulie wacheze kwa kujiamini na kwa nidhamu, kwenye ulimwengu wa soka kila kitu kinawezekana.
SI YUPO MTAALAMU MMOJA WA KUOTA ALIANZA KWA KUSEMA SIMBA NI UNDERDOG. WALIPOMKOSOA BADO KASHIKILIA SIMBA HAMNA KITU NI UNDERDOG. SASA HUWA NAJIULIZA HUYU JAMAA ANAJIHISI ANAUJUA SANA MPIRA KULIKO AKINA KIBADENI NA KITWANA MANARA? MBONA SIJAKUTANA NA JINA LAKE HATA KWENYE WAANDISHI WA MICHEZO WALIOBOBEA AKINA TOMMY SITHOLE, WILLIE CHIWANGO (MAREHEMU) NA MUHIDIN MICHUZI ? HUYU KATOKEA WAPI?
ReplyDeleteuyo katokea kwenye ukoo wa njaa anaangaika tu mpumbavu mmoja
Delete