KIKOSI cha Yanga leo kimeendelea kujikita kileleni baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Kagera Sugar mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Katika mchezo wa leo, Kagera Sugar walianza kuandika bao la kwanza dakika ya 31 kupitia kwa nahodha wao Paul Ngalyoma akimalizia mpira wa kona kwa kichwa, dakika ya 35 Yanga walipata bao la kusawazisha baada ya mchezaji wa Kagera Sugar Kassim Khamis kujifunga wakati akiokoa mpira uliopigwa na Papy Tshishimbi baada ya Yanga kupata kona fupi iliyopigwa na Thaban Kamusoko.
Kipindi cha pili Yanga walianza kwa kasi na dakika ya 48 Herritier Makambo alifunga bao la pili kwa Yanga akimalizia pasi ya Kelvin Yondani, iliwachukua Kagera Sugar dakika tisa kusawazisha bao kupitia kwa Kassim Khamis dakika ya 58 ambaye ndiye pia aliisawazishia timu ya Yanga.
Bao la ushindi wa leo lilipatikana dakika ya 72 kupitia kwa Thaban Kamusuko baada ya kuchezewa rafu na mlinda mlango wa Kagera Sugar na kufunga bao kwa 'freekick' ambalo lilidumu mpaka mwamuzi alipomaliza mpira.
Yanga ilimaliza mchezo wa leo ikiwa pungufu baada ya mkongwe, Kelvin Yondan kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 82 baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Kagera Sugar, Kassim Khamis.
Matokeo haya yanaifanya Yanga kucheza jumla ya michezo 31 ikiwa imejikusanyia pointi 74 huku Kagera ikiwa imecheza michezo 32 na ina pointi 36 ikiwa nafasi ya 17 kwenye msimamo.
0 COMMENTS:
Post a Comment