"UONGOZI si lelemama na haupaswi kukimbiliwa, kwa yule ambaye atakuwa anaukimbilia kuna haja ya kuchunguza na kujua uhitaji wake umejificha wapi." Hii ni nukuu ya Rais wa kwanza wa Tanzania, hayati Julius Kambarage Nyerere.
Nimeamua kuanza namna hii, tofauti kidogo kutokana na mchakato ambao unaendelea kwa sasa ndani ya klabu ya Yanga, inayotarajiwa kufanya uchaguzi wake kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi ili kusonga mbele.
Kwa muda mrefu Yanga imekuwa ikijiendesha bila kuwa na viongozi rasmi zaidi ya kuwa chini ya makaimu ambao nao wamekuwa wakisimamia mipango kwa kiwango kidogo si kama ambavyo angekuwepo kiongozi aliyechaguliwa angefanya hivyo.
Sasa ni fursa nyingine kwa wanachama na mashabiki wa Yanga kutimiza jukumu lao la kuchagua kiongozi ambaye wanamuhitaji kwa dhati atakayeweza kuleta mabadiliko ya kweli na sio porojo haitasiaidia.
Mei 5 si mbali ni siku moja tu ambayo italeta maamuzi yenu na nguvu yenu hasa kwa kupiga kura kwa kuchagua kiongozi ambaye ataleta mabadiliko na kuwaletea maendeleo ambayo mnayahitaji, mkikwama katika hilo basi maumivu yatakuwa juu yenu kwa kuwa mtakuwa mmekosea kufanya maamuzi.
Kikubwa ambacho mashabiki wa Yanga ambao ni wanachama wasikubali kuangalia sura ili wachague viongozi bali wanatakiwa wasikilize sera na kuelewa kile ambacho kinaelezwa hapo watapata kile wanachohitaji.
Endapo kila mmoja atachagua kiongozi kwa sura ama kuleta undugu naye na urafiki, atavuna kile ambacho amekipanda kwani kama kiongozi hana sera nzuri matokeo yake hayataonekana kuwa bora hapo baadaye.
Natambua mchakato mkubwa ambao umefanyika kwa kila mmoja kuona namna ambavyo ana shauku ya kupata viongozi wapya ili kuendeleleza ile safari ya kufuata mafanikio ya soka ambalo kwa sasa linazidi kukata mbunga kuelekea kwenye hali ya kimataifa.
Umakini kwa wanachama hasa wakati wa kusikiliza sera unahitajika ili kupata kile kilicho bora kutokana na ukubwa wa timu ya Yanga pamoja na ukubwa wa majukumu ambayo wataanza nayo kuyatimiza.
Rai yangu kwa wagombea pia kuwa watulivu na waachane na tabia ya kutoa rushwa ili wachaguliwe kwani vitendo hivyo si vya kisoka na havina nafasi kwa maendeleo.
Kwa mgombea ambaye atategemea kutoa rushwa ili apewe nafasi inabidi ajitathimi kwamba ni kwa namna gani ataweza kuisaidia timu endapo atapata nafasi ilihali mazingira aliyofika hapo si sawa.
Kwa wanachama ambao watagundua kwamba wanarubuniwa kwa vitu vidogo ni budi kwao kuwakwepa watu wa namna hii na kuwapa adhabu ya kutowapa nafasi kwani watawapoteza.
Tukiachana na mchakato wa uchaguzi hebu tuzungumzie pia na Ligi Daraja la Kwanza ambayo kwa sasa ipo kwenye mechi za lala salama na kila timu kupania kupanda daraja.
Tayari tumeona Namungo FC kutoka kundi A wamepenya mpaka Ligi Kuu wanapaswa pongezi kwa kupambana sasa kazi inabaki kwenye kundi B ambalo lina patashika nyingi mechi mojamoja kwa kila timu ndiyo imebaki.
Jicho la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa litazame vema hali halisi ya soka letu hasa kwenye hizi ligi za chini na sio kuwekeza macho kwenye ligi kuu pekee.
0 COMMENTS:
Post a Comment