KAKOLANYA KUMPA CHANGAMOTO MANULA SIMBA, KAZI IPO
ALIYEKUWA kipa wa Yanga, Beno Kakolanya amefunguka kwamba anatua Simba kwa msimu ujao huku akichimba biti kwa kipa mwenzake, Aishi Manula kuwa ajipange kisawasawa kwa ajili ya kugombania nafasi ya kuanza.
Kakolanya kwa sasa ni mchezaji huru baada ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kuuvunja mkataba wake na Klabu ya Yanga.
Kwa maana hiyo sasa Kakolanya aliyetua Yanga msimu wa 2016/17 akitokea Tanzania Prisons ya Mbeya, yuko huru kusajiliwa na klabu yoyote ambayo itamhitaji.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Kakolanya amefunguka kwamba anaweza kutua Simba endapo mabosi wa timu hiyo chini ya mwekezaji wake, Mohammed Dewji wakimtengea dau la maana.
Hata hivyo, amegoma kutaja hilo dau la maana analotaka ni kiasi gani.
“Ndiyo nimesikia juu ya hilo suala la mimi kuwa huru baada ya kuvunjwa kwa mkataba wangu na Yanga.
“Ninachokiangalia kwa sasa ni timu mbalimbali zije ili nisaini kwao. Inawezekana mimi kutua Simba au Azam, cha kwanza ninachokitazama ni juu ya maslahi yangu binafsi.
“Ikitokea timu inanipa kiasi ninachokihitaji basi ninajiunga nao. Kuhusiana na eti nitakutana na kina Manula (Aishi) na Dida (Deogratius Munishi) Simba wala siogopi, nitapambana nao katika kupata namba na jambo kubwa ninaamini juu ya uwezo wangu,” alisema Kakolanya.
Simba kwa muda mrefu ilitajwa kuwa inamtaka kipa huyo ambaye aliwabania pointi tatu muhimu kwa kuokoa michomo mingi katika mchezo dhidi ya Yanga kwenye mzunguko wa kwanza msimu huu uliomalizika kwa suluhu.
Hata hivyo, viongozi wa Simba walipotafutwa jana mchana, simu zao hazikuwa zikipokelewa.
AJE SIMBA JAMANI VIONGOZI SIMBA KAMILISHENI MIPANGO MWAKANI TUNA MECHI ZA KIMATAIFA LAZIMA KUWA NA TIMU ILIYOSUKWA KWELIKWELI TUNAHITAJI MAGOLIKIPA 3 BORA SANA.
ReplyDelete