Imeelezwa kuwa uongozi wa Azam FC umekamilisha utaratibu wa kuipata saini ya kocha wa KMC, Etiene Ndayiragije na ndani ya masaa 48 huenda akatangazwa ndani ya kikosi hicho cha matajiri wa Dar es Salaam.
Ndayiragije anapewa nafasi kubwa ya kujiunga na kikosi hicho kutokana na kuwa na mwenendo mzuri ndani ya kikosi chake cha KMC ambako amegomea kuongeza mkataba na uongozi ukathibitisha habari hizo jambo ambalo limeongeza uwezekano wa kocha huyo kutua Azam FC.
Kwa sasa Azam FC wanamtafuta mrithi wa mikoba ya aliyekuwa kocha mkuu, Hans Puijm ambaye alifukuzwa kwa kile kilichoelezwa kuboronga ndani ya Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Salehe Jembe, mratibu wa Azam FC, Philip Alando amesema kuwa michakato yote kuhusu kocha inakwenda sawa hivyo kumtangaza ni suala la muda tu.
"Kwa sasa suala la kumtangaza kocha ni suala la muda tu, hivyo mashabiki na wadau wa Azam FC wawe na utulivu kwani mambo mazuri hayataki haraka.
"Mpango uliopo ni ndani ya siku mbili tunaweza kuweka mambo hadharani na kumtangaza kocha wetu atakayeongoza benchi la ufundi," amesema Alando.
0 COMMENTS:
Post a Comment