June 10, 2019









NA SALEH ALLY
MJADALA umekuwa mkubwa sana kuhusiana na viungo wawili, mmoja ni Ibrahim Ajibu ambaye ameichezea Yanga msimu uliopita na Jonas Mkude wa Simba.


Hawa wote ni vijana wa Kitanzania ambao tayari wamejitengenezea ajira kupitia mchezo wa mpira wa miguu.


Ni jambo guri sana kumuunga mkono mwenzako unapoona amefanikiwa katika jambo fulani. Sisi sote ni Watanzania, lazima tuungane mkono kwa maana ya kila mmoja anapaswa kuishi kwa furaha.

Pamoja na kuungana mkono, kunapofikia wakati kuna ukweli unapaswa kuwa wazi, unapaswa kuwa na njia iliyonyooka kwa ajili ya kulisaidia taifa letu basi ni vizuri kuwa hivyo.


Kwa sasa tuna msala wa Ajibu na Mkude kwa sababu ya mapenzi ya klabu kubwa mbili za Yanga na Simba. Bahati mbaya nimeona baadhi ya mashabiki wanajaribu kuuhamisha mjadala hadi kwenda kwa Shomari Kapombe kwa kisingizio kuwa Kocha Emmanuel Amunike hawapendi wachezaji wa Simba.


Wakati mwingine inakuwa vizuri kutafakari mambo kabla ya kuanza kuyatoa. Kapombe sote tunajua ni majeruhi, Amunike alimuita huenda aliamini angeweza kupona. Anayesema kuwa Kapombe anaonewa, atuthibitishie kwamba yuko fiti ila kaachwa tu. Vizuri tuzungumze mambo ya msingi na hasa katika hili la taifa letu.

Kapombe si beki pekee, timu ya taifa haichagui watu sababu ya ushabiki wa klabu au kulazimisha. Wakati mwingine lazima tujiondoe katika ushabiki hasa kama kuna uhalisia linapofikia suala la timu ya taifa.


Acha nirejee katika suala la Ajibu na Mkude, ambao kuachwa kwao na Amunike linaendelea kufanya tusahau mjadala wa timu yetu ya taifa inafanyaje na badala yake ishu ni Ajibu na Mkude.

Tumepata taarifa ya Mkude kuchelewa kufika kambini, mmekuwa mkisikia namna Simba wakilalamika kuhusiana na utovu wa nidhamu. Ingawa wamekuwa wakifanya makosa ya kulalama chinichini.


Chinichini ya Simba, inafanya watu wengi wasijue matatizo ya Mkude na hili linasababisha hata inapotokea akatendewa haki, wengi wanaamini ameonewa. Simba wamekuwa wakificha maradhi lakini unaona “kifo” kinamuumbua.


Huyu ni kijana Mtanzania, tumtengeneze kwa kumueleza ukweli badala ya kupaka mafuta kwa mgongo wa chupa.


Kuna mtu alihoji kuhusiana na Ajibu, akisema kama Ajibu tatizo ni kukaba, Messi Mbona hakabi Barcelona, au Chama mbona hakabi Simba? Ana haki ya kuhoji. Lakini timu moja haiwezi kuwa na kina Messi wawili.


Taifa Stars uwe na Samatta asikabe, uwe na Ajibu asikabe, itakuwa timu ya namna gani. Mwalimu anamuachia Samatta muda wa kupanga mashambulizi na kuhifadhi nguvu. Halafu na Ajibu naye iwe hivyo!


Ndio maana anaweza kuona bora kuwa na mchezaji asiye na kipaji sana lakini akaisaidia timu inapokuwa inashambuliwa. Badala ya kuwa na timu mkianza kushambuliwa mnabaki pungufu ya wachezaji wawili, haiwezekani na hasa ukizingatia tunakwenda kama timu isiyopewa nafasi.


Binafsi mimi si mtu ninayemkubali sana Amunike kutokana na uchezaji wa timu ulivyo. Lakini bado naweza kuheshimu matakwa yake halafu tutaona kitakatochokea Misri ingawa kama Mtanzania ninaomba yawe matokeo bora kwa kuwa Amunike ni Mnigeria na sisi tumemuajiri tu.


Lazima tukubali kuwaambia ukweli vijana wetu. Lazima tupime na kuangalia, hivi kama kweli kabisa Amunike angekuwa anajua atasaidiwa na Ajibu na Mkude atawaacha vipi wakati na yeye angependa kuweka rekodi.


Mfano, mtu kaitwa na hata kabla ya kujiunga tayari kaonyesha utovu wa nidhamu.


Tukubali wakati mwingine kuwaeleza watu wetu maneno magumu ambayo yatawabadilisha badala ya kuendelea kuwa mashabiki wao wakati tunaona wanatumbukia shimoni.



Wakati huu ni mzuri kufanya mjadala kwa wale walio na kikosi cha Afcon nchini Misri na watafanya nini na Ajibu na Mkude, tuwaache na mapumziko yao.

2 COMMENTS:

  1. Salehe tunaheshimu maoni yako kama mtanzania na kama Mdau wa soka na habari ambae ukisema neno basi watu wanaweza kuacha shughuli zao na kuanza kusikiliza unasemaje. Lakini nashangazwa na unavyojaribu kumumunya maneno juu ya uwezo wa Amunike ila la kujiuliza kwani Amunike tangu awe kocha wa stars alishawahi kuwa na muda wa kutosha kufanya nao kazi Ajibu na Mkude? Sidhani hata kama walibahatika kucheza angalau mechi moja ya kufuzu chini ya Amunike. Sasa wakati gani Amunike amewaona hawa vijana hawana nidhamu? Wasi wasi wangu Amunike anakaririwa taarifa za wachezaji wake na labda kwa maelezo yako salehe jembe ungefurahi kuona Simba wanamfukuza mkude kwa hayo madai ya utomvu wake wa nidhamu badala ya jitihada za makusudi za Simba za kuhakikisha kuwa mkude anakuwa bora zaidi licha ya mapungufu yake. Pengine kama si Simba watu walishamsahau mkude. Sio kila kinataka nguvu ili kiwe bora. Kama kocha ana amini mchezaji wake anauwezo bali ana matatizo ya nidhamu alafu anaamua kumuacha tu apotelee mbali aende akajifunze adabu mwenyewe basi mara hii tumepata kocha wa kuwaendeleza vijana wetu? Kwa uwezo wa Simba kama wanataka kuachana na Mkude ni kitu kidogo ila naona Simba wana busara zaidi na amini dawa ya ushindani wa namba ndani ya Simba hasa kwa msimu wa ligi uanaokuja utamuongezea mkude na wachezaji wengine wazawa uwezo wa kujitambua zaidi badala ya kukatishwa tamaa. Amunike kusema kuwa ana bifu na wachezaji wa Simba? Inawezekana akawa hana bifu ila anaelewa kuwa Simba wapo vizuri zaidi kuliko timu yake ya Taifa stars hilo halina ubishi sasa anachofanya Amunike ni kujiekea kinga ya kuwa yeye yupo juu zaidi ya Simba na ni kweli ila anatakiwa kutambua kuwa timu bora katika nchi yeyote ile ambayo haina hazina kubwa ya wachezaji wanaocheza nje ya nchi basi timu hiyo ndio inayochangia wachezaji wengi zaidi kwa timu ya Taifa na lengo ni moja tu. Mara nyingi timu za taifa huwa hazina muda wa kutosha wa kuwaunganisha wachezaji tofauti kuwa kitu kimoja kabla ya mashindano. Sasa kuwa na wachezaji wengi waliocheza pamoja kwa muda mrefu kutoka timu moja unarahisisha uwiyano wa timu kwa muda mfupi.

    ReplyDelete
  2. Unaposema kapombe sio beki pekee wakati timu ilipoenda cape Verde Na Lesotho ulikuwa uchochoro Na kufungwa magoli ya ajabu,labda kuachwa kwake kuwa hajaimarika kutokana Na kuwa majeruhi WA muda mrefu lakini kapombe Ni issue achana Na Ajibu au Mkude maana tunaweza kuwa Na wabadala lakini sio kapombe hapo umechemka.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic