ASKARI AJIUA KISA MKWEWE
MOROGORO: Inasikitisha! Askari wa Kampuni ya Ulinzi ya Setembo, Rajabu Athumani (60), anadaiwa kujiua kwa kujinyonga, kisa kikidaiwa ni mauaji ya mkwewe, Amani lina habari ya kusikitisha.
Tukio hilo lililoacha simanzi kubwa lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita nyumbani kwa mlinzi huyo Mtaa wa Mafiga A mjini hapa.
Baada ya kutokea kwa tukio hilo baya, baadhi ya wananchi walitoa taarifa kwa mwandishi wetu ambaye alitinga eneo la tukio na kushuhudia umati ukiwa umepigwa na butwaa ukishuhudia mwili wa jamaa huyo ukitolewa na polisi kutoka ndani kwake.
Kwa mujibu wa mashuhuda walioingia hadi ndani ya chumba cha mlinzi huyo, alijinyonga kwa kutumia shuka alilofunga juu kwenye paa la chumba chake. Baada ya kuuchukua mwili huo, polisi waliondoka nao na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ukisubiri uchunguzi na taratibu za mazishi.
Baada ya taratibu hizo za kipolisi kukamilika huku mwandishi wetu akipiga picha hatua kwa hatua, gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na dada wa mlinzi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Amina Athuman, mtoto wa marehemu, Mwajuma Rajab Athuman na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mafiga A, Hassan Magoso ambaye tukio hilo lilijiri kwenye mtaa wake.
KISA MAUAJI YA MKWEWE
Dada huyo wa marehemu, Amina Athuman alisimulia juu ya kifo cha kaka yake; “Chanzo cha kifo cha kaka yangu ni mkewe, Sauda au Mama Hamisi ambaye alizaa naye watoto wawili na kaka yangu. “Mtoto mmoja wa marehemu ni Hamisi anayesoma kidato cha kwanza na mwingine ni Mwajuma anayesoma darasa la sita. “Awali Rajab na wifi yangu walikuwa na mgogoro kwenye ndoa yao.
“Baadaye wifi yangu ambaye ni mke wa Rajab aliamua kutoroka nyumbani takriban miezi miwili iliyopita. “Kaka yangu alimtafuta sana hapa mjini, lakini hakumpata, alipompigia simu haikupatikana, hivyo aliamua kwenda ukweni kwake kule wilayani Kilosa (Morogoro) kwa wazazi wa mkewe.
“Alipofika Kilosa aliambiwa kuwa mkewe hakuwa amefika huko ndipo kaka yangu akaamua kurejea mjini (Morogoro). “Cha ajabu, baada ya siku mbili, watu wasiofahamika walivamia nyumbani kwa wakwe zake kule Kilosa na kumuua mama mkwe wa Rajab na mjukuu wake. “Kufuatia tukio hilo, kaka yangu alikuja kukamatwa akihusishwa na mauaji hayo.
“Hoja ilikuwa ni kwamba, kwa nini mauaji hayo yatokee baada ya yeye kufika Kilosa na kuondoka? “Kufuatia tukio hilo, kaka yangu alikaa sana ndani hadi baadaye alipoachiwa kwa dhamana ambapo kila siku ya kesi alikuwa akienda wilayani Kilosa na kurudi mjini.
“Hivi karibuni kaka yangu alitoka huko kwenye kesi akiwa na msongo wa mawazo ya kesi hiyo na kukimbiwa na mkewe hadi hadi tulipomkuta amejiua kwa kujinyonga. “Kwa hiyo kwa kifupi kaka amejiua kutokana na msongo wa mawazo juu ya kesi ya mauaji ya mkwewe kule Kilosa na mkewe ambaye hajulikani alipo, lakini kubwa kuliko yote ni hiyo kesi ya mauaji ya mama mkwe wake.”
Alipoulizwa kama wifi yake huyo alishiriki mazishi ya mama yake huko Kilosa, Amina alisema; “Hata sisi tulishangaa hakuwepo kwenye mazishi ya mama yake mzazi. Kifupi hatujui alitimkia wapi na kumwacha mwanaye mdogo ambaye kila siku anamuulizia mama yake.”
MTOTO WA MAREHEMU
Naye Mwajuma ambaye ni mtoto wa mwisho wa marehemu Rajabu alipohojiwa na Amani juu ya kifo cha baba yake alikuwa na haya ya kusema;
“Kila siku asubuhi huwa ninamgongea baba anipe pesa ya shule, lakini cha ajabu leo (wiki iliyopita) niligonga sana hakufungua, nikamwambia shangazi ambaye naye aliwaambia majirani, tukaamua kuvunja mlango na kumkuta baba akiwa amejinyonga.” Alipoulizwa kama anajua alipo mama yake, mtoto huyo alijibu;
“Yaani kwa sasa tumebaki yatima mimi na kaka yangu. Tangu mama aondoke huu ni mwezi wa pili hatujui aliko. “Kama alikuwa na ugomvi na baba kwa nini ametutelekeza sisi wanaye tusiohusika na ugomvi wao. “Ona sasa baba amejiua.”
SERIKALI YA MTAA
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mafiga A, Hassan Magoso alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwenye mtaa wake na kwamba jambo hilo lipo chini ya polisi kwa uchunguzi zaidi.
KAMANDA MUTAFUNGWA
Amani lilifika ofisini kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Wilbroad Mutafungwa ili kuthibitisha tukio, lakini alikuwa nje ya ofisi.
0 COMMENTS:
Post a Comment