KMC WAIWAHI MAPEMA TP MAZEMBE
KIKOSI cha timu ya KMC Alhamisi hii kinatarajia kukwea pipa kuelekea nchini Rwanda kwa ajili ya kuwawahi wapinzani wao TP Mazembe katika michuano ya Kombe la Kagame.
KMC ambao wanafundishwa na kocha Jackson Mayanja raia wa Uganda, ni miongoni mwa timu shiriki za kombe hilo la Kagame ambapo walipata nafasi hiyo baada ya Yanga na Simba kujitoa.
KMC wamepangwa Kundi B wakiwa na TP Mazembe ya DR Congo, Rayon Sports ya Rwanda na Atlabara ya Sudan Kusini.
Ofisa Habari wa KMC, Anwari Binde ameliambia Championi Jumatatu, kuwa wanawahi kwenda Rwanda kwa ajili ya kujipa muda wa kuzoea mazingira kabla ya kuanza kwa kombe hilo Julai 7, mwaka huu.
“Sisi safari yetu kwenda Rwanda kwenye Kagame tutaondoka Julai 4, tukiwa na kikosi kizima sambamba na kocha Mayanja.
“Tunawahi kwenda huko tukazoee mazingira pamoja na kujiweka sawa kabla ya kuanza kupambana na wapinzani wetu kwani kama unavyojua, hii ndiyo mara ya kwanza kushiriki lakini tunataka kufanya vizuri na kuweka rekodi,” alisema Binde.
0 COMMENTS:
Post a Comment