KISA KITI, MISRI WATIA AIBU ZONE V UGANDA
WAKATI mchezo wa mpira wa kikapu kati ya Tanzania dhidi ya Kenya upande wa wanaume ukichezwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Lugogo, Kampala nchini Uganda, wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Misri walitia aibu na kuzua vurugu kubwa.
Vurugu hizo zilizosababisha mchezo huo wa mashindano ya Kanda ya Tano (Zone V) kusimama ndani ya robo ya tatu, zilitokana na baadhi ya wachezaji hao wa Misri kutaka kuchukua viti ambavyo vilikuwa kwenye benchi la timu ya Taifa ya Tanzania.
Tukio hilo lililoshuhudiwa na Championi, lilijiri wakati ambapo mmoja wa wachezaji hao kuchukua kiti, kisha Kamishna wa Mashindano kutoka Shirikisho la Mpira wa Kikapu Afrika (Fiba), Zulfikar Kareem, kuwakataza kukiondoa, ndipo mvutano na vurugu zilipoibuka.
Mvutano huo uliodumu kwa zaidi ya dakika tatu, ulikusanya umati wa mashabiki waliokuwa wakifuatilia mchezo kujikuta wakishangaa kwa tukio walilofanya lililosababisha askari kuitwa uwanjani tayari kwa kutuliza hali ya hewa.
Baada ya dakika chache kupita, vurugu zilisimama na kila mmoja kurudi nafasi yake, kisha wachezaji wa Misri wakatengewa viti vyao na kuendelea kuwafuatilia Watanzania waliokuwa wakicheza ambapo hadi mchezo unamalizika Tanzania ilipoteza kwa pointi 112-74 dhidi ya Kenya.
0 COMMENTS:
Post a Comment