July 4, 2019


MICHUANO ya Afcon kwetu sisi ilikuwa ni changamoto mpya kwani tumeona namna gani timu yetu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ikihaha kupata matokeo chanya kutokana na kutokuwa na uzoefu mkubwa.

Kwetu sisi kwa hatua ambayo tumefikia si mbaya ila kuna mengi ya kujifunza ambayo ni lazima tuyafanyie kazi kwa ajili ya maboresho wakati mwingine tukipata nafasi ya kushiriki michuano hii mikubwa.

Tumeshuhudia kwa macho yetu mchezo wa  kwanza dhidi ya Senegal ambao  tulipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 namna ambavyo mashabki waliumia na kulalalamika kutokana na mfumo wa mwalimu.

Mchezo wa pili tuliona kulikuwa na mabadiliko makubwa hasa kwa timu kucheza na kupata matokeo jambo ambalo kwa kiasi fulani lilileta matumaini kwa timu yetu kuonyesha uwezo wake

Licha ya kupoteza mchezo wetu mbele ya Kenya bado kulikuwa na kitu ambacho kilifanywa na wachezaji wetu ambao walipambana kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili mbinu ziliwakataa wakazidiwa ujanja na kupoteza kwa kufungwa mabao 3-2.

Mchezo wa mwisho ukawa funga kazi baada ya kupoteza kwa mabao 3-0 mbele ya Algeria hakuna namna nyingine zaidi ya kuvuna kile tulichopanda.

Tuna kitu ambacho tunapaswa tujifunze kwa wenzetu ambao wamefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora kwenye michuano hii ya Afcon ama wale ambao walipata fursa ya kulinda matokeo yao ambayo walikuwa wakiyapata kwenye michuano hii mikubwa Afrika.

Wenzetu asilimia kubwa ukitazama kikosi chao robo tatu ya wanaounda kikosi cha kwanza wanacheza nje ya nchi hali inayowafanya wawe bora kutushinda sisi ambao asilimia kubwa wachezaji wetu wanacheza ligi ya ndani.

Hali hiyo ipo kwetu pia kwani  wale wachezaji ambao wanacheza  ligi ya nje wanafanya vizuri tofauti na wale ambao wanacheza ligi ya ndani hapa kuna kitu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanapaswa wafanye.

Mtazame mchezaji kama Mbwana Samata, Simon Msuva, Farid Mussa,Thomas Ulimwengu namna wanavyoonyesha kandanda ambalo si la kawaida hasa kwa kucheza kwa ufanisi mkubwa uwanjani.

TFF wanapaswa waangalie namna ya kukuza ligi yetu iwe bora kuliko vile ambavyo ipo sasa ili kutoa fursa ya kutengeneza wachezaji bora na imara ambao itakuwa rahisi kwao kujiuza nje ya nchi.

Kwa wale wa Tanzania ambao wanacheza ligi ya ndani  wapo baadhi ambao nao wamekuwa ni bora na ukiwafuatilia kwa ukaribu utagundua kwamba wamekuwa na misingi mizuri tangu awali.

Kutoka chini wamejengwa vizuri hasa kwa kupitia kwenye vituo vya kuwakuza pamoja na kupata walimu wazuri ambao wanawapa changamoto mpya kila siku jambo ambalo linawafanya nao wawe kwenye chati.

Jambo lingine la ajabu ambalo linapatikana kwenye ligi yetu ni namna wageni ambao wanakuja kucheza ligi yetu wanavyokuwa bora kushinda wazawa hasa kwenye timu za Taifa.

Hapa pia wachezaji wetu wanapaswa kujifunza namna bora ya kulinda viwango vyao pamoja na kujituma bila kujali aina ya timu ambayo wanachezea ili kulinda uwezo.

Kujitambua kwa wale ambao wanacheza ligi zetu kunawapa nafsi ya wao kufanya vizuri hata wanapokuwa nje ya timu zetu za Bongo ambazo zinawapa nafasi ya kucheza.

Cheki Emmanueli Okwi, Juuko Murshid, Thaban Kamusuko, Tafadzwa Kutinyu hawa wanafanya vizuri wakiwa kwenye timu zao za Taifa na wametoka ligi yetu.

TFF iangalie namna ya kubadili watu wa ndani wawe na uimara hata wanapotoka nje  misingi bora ya kusimamia ligi yetu inatosha kuwafanya vijana wetu kuwa imara wakati wote kitaifa na kimataifa.

Ligi iwe bora itasaidia kuwapata wachezaji makini ambao watatupa matokeo chanya kwenye michuano mingine inayofuata na sio kuishia kuwa wasindikizaji.

Tumeona wenzetu wa Cameroon, Uganda wamekuwa wakiwaita wachezaji wakubwa kutoa hamasa, sasa kwetu imekuwa tofauti wamekwenda wanasiasa jambo ambalo linaleta mkanganyiko.

Afcon isituache wapekwe bali itupe somo wakati mwingine tunapaswa nasi tuwape nafasi malegendari wetu ambao wamecheza Afcon, watu kama kina Peter Tino, Edibly Lunyamila, hawa wapewe nafasi ya kuzungumza na wachezaji.

Tusichanganye siasa na mpira ni vitu viwili tofauti itakuwa ngumu kwetu kufikia mafanikio kama tutakubali mpira utawaliwe na siasa.

Wanasiasa wana nafasi zao na sehemu zao za kufanya kazi lakini si kwenye mpira kutoa hamasa ni jambo la kiupekee haina maana kwamba hawapaswi kushangilia timu yao TFF itofautishe haya mambo mawili tofauti kabisa kushangilia na kutoa hamasa.


2 COMMENTS:

  1. Timu ya Taifa inatolewa AFCON....Turudi sasa kwenye "vumbi letu na usajili wa magazeti na mihemko ya ushabiki wa timu za Kariakoo zinazodumaza soka letu"

    ReplyDelete
  2. Saleh Jembe .Atom Haifanyi Kazi Ukibofya Inaleta Habari Za Zamani (50 Day Ago)

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic