Katibu Mkuu wa zamani wa Simba, Kassim Dewji leo amefika katika Mahakama ya Haimu Mkazi wa Kisutu na kutoa ushahidi.
Dewji ambaye alianza kuwa katibu mwenezi wa Simba mwanzoni mwa miaka ya 2000, alitoa ushahidi katika keshi inayowahusu viongozi wa zamani wa klabu ya Simba.
Kiongozi huyo ambaye sasa ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba na shahidi namba nane katika kesi inayowakabili Evans Aveva aliyewahi kuwa mwenyekiti na Geofrey Nyange ambaye alikuwa makamu wake mwenyekiti pamoja Zacharia Hans Pope kuhusiana na mauzo ya mchezaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi.
Dewji ameieleza mahakama jinsi walivyopanga matumizi ya fedha za mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi ambaye alikuwa ameuzwa katika klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia.
Kassim ambaye ni mfanyabiashara wa vifaa vya michezo vya Kampuni ya Romario Sports 2010 Limited aliiambia mahakama akiwa kama mjumbe wa kamati ya utendaji chini ya uongozi wa Aveva waliitwa kamati ya utendaji na kuelezewa kuwa fedha ambazo aliuzwa mchezaji Okwi kwenye klabu ya Etoile du Sahel dola 300,000 zimefika.
Shahidi huyo aliielezea mahakama kuwa kama kamati ya utendaji walijadiliana matumizi ya zile fedha. Alianza kufafanua Dewji mahajamani hapo.
“Kipindi tunajadiliana kuhusu zile fedha dola 300,000 Simba ilikuwa na madeni kipindi hicho na madeni mengine ya nyuma ya uongozi uliopita.
“Tukaona zile fedha zinaweza kuisha kuna mwenzetu mmoja tulikuwa tumekopa ambaye ni Hans Pope tuliamua kumlipa fedha yake ambayo ilikuwa ni dola 17,000," alifafanua Dewji na kuendelea.
“Baada ya hapo fedha ambayo ilibakia kama kamati tulikubaliana kuwa ifunguliwe akaunti ambayo zile fedha zitaweka na ni kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Bunju ambapo hapo kulitakiwa manunuzi ya nyasi bandia kumlipa mkandarasi na mambo mengine."
Kuhusiana na suala la akaunti ambayo ilikuwa kando na ile ya klabu ya Simba, Dewji alifafanua.
“Na hiyo akaunti aliyetakiwa kuifungua ni rais (Aveva) pamoja na mhasibu/katibu (Amos) ndiyo walikuwa na jukumu hilo kwa kuwa ndiyo watendaji wa juu.
"Aidha, iliundwa kamati ya kusimamia uwanja huo iliitwa Bunju Project, lakini baada ya hapo sikujua kama akunti ilifunguliwa au la kwa sababu sikuhudhuria tena kwenye kikao cha kamati ya utendaji kwa kuwa nilisafiri.”
Baada ya ushahidi huo, kesi hiyo ambayo ipo chini ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba alihairisha kesi hiyo mpaka Septemba, 4 mwaka huu huku Aveva na Kaburu wakirudishwa tena mahabusu.
0 COMMENTS:
Post a Comment