MSIMU wa Ligi
Kuu Bara 2019/20, umeanza Jumamosi ambapo mechi tano zimechezwa
kwenye viwanja vilivyopo kwenye mikoa mbalimbali.
Mechi za Jumamosi Mbao ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Alliance, Mbeya City ililazimisha sare ya bila kufungana na Prisons, Namungo ilishinda kwa mabao 2-1 mbele ya Ndanda,
Polisi Tanzania ikaichapa bao 1-0 Coastal Union na Biashara United ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar.
Jambo zuri
ni kwamba, kabla ya ligi haijaanza kuchezwa, tayari Bodi ya Ligi Kuu
Tanzania (TPLB) imefanya maboresho ya kanuni zake na kuziweka hadharani.
Sasa
kila timu shiriki na wadau mbalimbali wakiwemo mashabiki wa timu hizo
wanazitambua sheria hizo.
Ikitokea
siku timu, mchezaji au kiongozi yeyote wa timu amepewa adhabu kulingana na kosa
alilolifanya kwenda kinyume na kanuni zinavyotaka, hakutakuwa na malalamiko kwa
sababu vitu vipo wazi.
Kitu kikubwa
pia ambacho binafsi nimeona kizuri katika hili ni namna ya kuweka wazi timu
ambazo zitashuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara baada ya kumalizika msimu huu,
lakini pia njia za kuzipata timu ambazo zitapanda kutoka
Ligi Daraja la Kwanza
kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2020/21.
Msimu
unapoanza, kila timu itakuwa inafahamu inatakiwa kufanya nini ili kuepuka janga
la kushuka daraja.
Tuliona
msimu uliopita ambao timu mbili za Ligi Kuu Bara zilishuka daraja moja kwa
moja, huku mbili zikiponea tundu hilo baada ya kushinda mechi zake za play off.
Lakini pia
ukiwa katika nafasi ya 15 na 16, utakuwa kwenye hatari ya kushuka pia kwa
sababu utalazimika kucheza mechi za play off. Kushinda kwako ndiyo kutakuokoa,
la sivyo unakwenda na maji.
Ni wakati
sasa wa timu kuzichanga vema karata zao ili kutoa ushindani wa kweli msimu huu
tofauti na ilivyokuwa msimu uliopita ambapo kuna baadhi ya mechi kabla
hazijachezwa, unaweza kutabiri kwa uhakika nani atakuwa mshindi.
Tunahitaji
ligi yenye ushindani mkubwa, kwa staili hii ushindani utakuwepo, lakini pia
uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupunguza idadi ya timu kutoka 20
hadi 18 kwa msimu ujao, kisha timu 16 msimu ule unaofuata wa 2021/22, ni uamuzi
mzuri kwani hapo itaondoa ile hali ya kushindwa kuimudu ligi yenyewe
inayozalisha viporo visivyo na ulazima.
Nikiachana
na Ligi Kuu Bara, nije katika hili suala la wawakilishi wetu kwenye michuano ya
Shirikisho la Soka Afrika (Caf). KMC walicheza na AS Kigali baada ya
mchezo wa kwanza kule Kigali nchini Rwanda kumalizika kwa matokeo ya 0-0 ukiwa
ni wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Na wametolewa kwa kufungwa mabao 2-1 uwanja wa Taifa kbala ya jana Simba nao kufungashiwa virago kwa faida ya bao la ugenini walilolipata UD do Songo baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Yanga huko Botswana ilifanya kweli mbele ya Township Rollers baada ya mchezo wa kwanza hapa nyumbani
wa Ligi ya Mabingwa Afrika kumalizika kwa sare ya 1-1, wakwafungashia virago wenyeji wao kwa kuwafunga bao 1-0 ugenini.
Watanzania tukubali kwamba mpira ni dakika tisini na kuweka maneno mengi mdomoni bila vitendo hayatusaidii bali yanatupoteza.
Kupoteza kwa timu zetu nyumbani inauma lakini hakuna namna zaidi ya kujifunza kufanya vema kwa ajili ya wakati mwingine kitaifa na kimataifa.
Hivyo iwe darasa kwa wawakilishi wetu waliobaki kimataifa ambao ni Yanga kwa upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC kwa upande wa Kombe la Shirikisho.
0 COMMENTS:
Post a Comment