Moja ya
sakata kubwa lililotanda hivi sasa kwenye soka ni suala la ubaguzi kwa wachezaji
kwenye mitandao ya kijamii.
Hasa
wachezaji weusi ndio walioandamwa mno kwenye soka la England ambayo ni ligi
pendwa duniani kote.
Sio suala
dogo, limekuwa kubwa kupita kiasi hadi
baadhi ya makampuni ya mitandao ya kijamii imeingilia kati ili kuweza kunusuru
biashara yao.
Yote hayo yanafanywa
na mashabiki ambao wanaonyesha kuwa hawana simile hata kidogo, wao wanataka
kufurahi tu basi.
Sasa tuje
hapa kwetu Bongo, wachezaji na viongozi wa mpira wetu wanateseka kweli kwenye
hiyo mitandao ya kijamii ila bahati mbaya hakuna wa kuwasaidia kupaza sauti.
Moja ya
mashabiki ambao hawana nidhamu kabisa ni mashabiki wa soka la Bongo, yaani wao
kukurushia matusi kwenye mitandao hawaoni shida.
Tena
hawatoishia kukutukana wewe tu, bali watafika hadi kwa familia yako na hata
wazazi wako nao wanamwagiwa matusi ambayo hayana msingi wowote.
Yaani ukiwa
mchezaji au kiongozi kwenye soka la Bongo ujue umeyaita matusi kwako maana
mashabiki wa soka wa nchi hii akili zao wanazijua wenyewe.
Lazima
tuseme ukweli mashabiki wengi wa soka kwenye nchi hii hawana nidhamu hata
kidogo na ndio maana wao hawaoni shida kumwaga matusi hadharani bila wasiwasi
wowote.
Wenzetu
mbele hasa hasa kwenye ligi za Ulaya ni rahisi kuwadhibiti mashabiki wahuni
kutokana na ukubwa wa teknolojia yao, ila kwa hapa Bongo ni shida, yaani shabiki
atakutukana lakini hakuna hatua yeyote itakayochukuliwa dhidi yake.
Mfano hivi
sasa wanasakwa mashabiki waliotoa maneno ya kibaguzi kwa Paul Pogba wa
Manchester United na nina hakika watakamatwa na sheria itafanyakazi yake lakini
Bongo ndio ingekuwa ishapita hiyo.
Siku hizi ukipita
kwenye mitandao ya kijamiii utaona kinachoendelea huko kejeli tu zinatawala kwa
wachezaji na viongozi hasa pale timu inapofanya vibaya, lakini hawapati msaada
wowote wa kisheria.
Tunajua
kwetu ni ngumu sheria kufanyakazi yake kwenye hilo, lakini mashabiki basi wawe
wastaarabu maana huyo mchezaji au kiongozi ni binadamu kama wewe, naye anaumia.
Ifike wakati
uhuni usipewe nafasi kwenye soka letu na ndio maana kuna baadhi ya watu wamesusa
hata kwenye viwanjani na kuwa karibu na mpira kwa sababu hiyohiyo ya tabia ya
uhuni na wakati ndio huu wa kuondoa.
0 COMMENTS:
Post a Comment