BANDA AFUNGUKA NAMNA USALAMA WAKE ULIVYO HUKO SAUZ
Na George Mganga
BEKI Mtanzania anayekipiga katika Klabu ya Highlands Park ya Afrika Kusini, Abdi Banda, amesema hali iliyopo nchini humo imechakufwa na matukio mengi lakini kwa upande wake kama mchezaji haijamuathiri.
Afrika Kusini imekumbwa na matukio mengi ya watu ambao si wazawa 'Xenophobia' kufanyiwa vurugu ikiwemo kupigwa na makazi yao kuchomwa moto sambamba kuuawa.
Kutokana na uwepo wa hali hiyo, Banda ameeleza yeye kama mchezaji na wenzake ambao si wazawa wa nchi hiyo, hawajapatwa na tatizo lolote sababu mazingira wanayokaa yapo salama.
"Ni kweli Afrika Kusini hivi sasa hali si shwari, ila kwa upande wetu kama wachezaji hakuna matukio kama hayo na usalama upo kwa asilimia kubwa.
"Hakuna kitu ambacho kinanifanya mimi nikose amani ya kuwa huku, tunaendelea na majukumu yetu ya kila siku bila wasiwasi wowote.
"Kingine nawashukuru Watanzania kwamba wanajali kwa kuulizia hali zetu maana nimesikia hata Serikali yetu huko Tanzania wanalizungumzia hilo mara nyingi, wawe na amani," alisema Banda.
Mbali na kueleza hayo, Banda ambaye awali alikuwa Baroka FC na baadaye kuachana nayo kisha kujiunga na Highlands Park, amewaasa Watanzania waliopo Sauz kuwa makini na namna hali ilivyo nchini humo kwa kuweka tahadhari mbele.
0 COMMENTS:
Post a Comment