September 8, 2019



MOTO wa Ligi Kuu Taznania Bara (TPL) umerejea ambapo kazi imeanza kwa timu zote 38 kucheza mchezo mmojammoja ndani ya TPL.

Namungo FC ni miongoni mwa timu ambazo zinashiriki ligi msimu huu wa 2019/20 imepanda Daraja na mchezo wa kwanza ilishinda kwa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC.

Hitimana Thiery aliweza kuipambania timu kutoka chini mpaka sasa hajapigwa chini bado anakomaa ndani ya Namungo huku mipango ikiwa kabambe kwa mafanikio zaidi.

 Mwenyekiti wa Namungo FC, Hassan Zidadu amefunguka mengi kuhusu mipango ya kikosi hicho huyu hapa:-

“Kitu cha kwanza ambacho tulipanga awali kabla ya kuanza kwa Ligi Daraja la kwanza ilikuwa ni kushiriki Ligi Kuu na jambo hilo limetimia kuna umakini mkubwa na mbinu nyingi ambazo zimefanywa kufikia hapa.

“Benchi la ufundi wao wamefanya yanayowahusu, viongozi pia usiwasahau mashabiki ambao wamekuwa bega kwa bega na timu ni kitu kizuri.

Malengo makubwa kwa sasa ni yapi?

“Tumeanza kuangalia namna ushindani ulivyo hasa kwa kusuka kikosi bora ambacho kitaleta ushindani ndani ya ligi. Mahitaji ya Ligi Daraja la Kwanza na huku ndani ya ligi Kuu ni tofauti kabisa.

“Kwanza kikosi kikiwa bora cha ushindani hapo tutaweza kushindana na timu zote ile kubaki ndani ya ligi kwa misimu mingi zaidi na sio kuja kutalii na kurejea tulikotoka.

Kikosi kwa sasa kipoje?

“Sio mbaya ni kikosi imara ukizingatia wachezaji ambao tumewasajili ni bora na wana uwezo mkubwa ndani na nje ya uwanja, hakuna kinachotupa wasiwasi kwenye ligi kuu ukizungumzia wachezaji.

Nani amewasajili wachezaji ?

“Uongozi umewasajili wachezaji na kwa mapendekezo ya Kocha Mkuu, Hitimana Thiery ambaye yeye pamoja na benchi lake la ufundi ndio wanajua ni aina gani ya mchezaji walikuwa wanamhitaji viongozi tunakamilisha hesabu kwa kumleta mchezaji.

Kwa nini mmechukua wachezaji kutoka timu kubwa ambao hawakuwa wakipewa nafasi?

“Hakuna mchezaji ambaye hakuwa akipewa nafasi nasi tukamchukua, wote walikuwa wakionyesha uwezo kwenye kikosi ndio maana mwalimu akakubali uwezo wa hao wachezaji.

“Imani yetu ni kwamba kwa kushirikiana na wachezaji wengine ndani ya kikosi wataleta ushindani na kufanya timu ipete katika michezo yote takayocheza.

“Paul Bukaba na Mohamed Ibrahim ni wachezaji makini ambao tumewachukua kwa mkopo kutoka Simba uzoefu wao utaleta muunganiko mzuri.

Mnahitaji kubeba Kombe la Ligi?

“Utakuwa ni uongo kama tukisema ndio, kwanza namna ambavyo kwa sasa tunaanza mipango yetu ni kuona timu inabaki kwenye ligi na tusiwe kwenye nafasi zile za mwisho hapana.

“Nafasi ya mwisho kabisa tunataka iwe ya 10 tena kwa taabu sana maana tuna amini wachezaji watapambana kupata matokeo.

Uwanja wenu una uwezo wa kubeba watu wangapi?

“Uwanja wetu kwa sasa bado unaendelea kufanyiwa maboresho ili uwe bora zaidi, ukikamilika utakuwa unabeba zaidi ya watu 3000 na ni uwanja bora tunajivunia.

“Unaitwa Uwanja wa Majaliwa.

Mbali na wachezaji hawa wa ndani je mna wachezaji wa kigeni?

“Tuna wachezaji saba wa kigeni mbao ni pamoja na Abarola, Leopold Toure, Stephen Duah, Abdul Waheed, Jerome Sina, Styve Nzigamasabo na Bigirimana Blaise.

Vyanzo vya mapato vinatoka wapi?

“Jina la Namungo ni eneo la mlima ambao upo Lindi huu ni maalumu kwa ajili ya machimbo ya madini, kuna dhahabu pamoja na aina nyingine hapo ndipo sehemu yetu ya kwanza ya mapato, mbali na hiyo wadau wapo pamoja na timu mashabiki nao.

“Kwa sasa tunafanya mazungumzo na baadhi ya wadhamini ili watupe sapoti kwani tunahitaji kumudu gharama kwa uhakika mambo yakikamilika kila kitu kitakuwa wazi hakuna cha kuficha kwetu,” anamalizia Zidadu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic