September 7, 2019



KAZI imeanza ya kuisaka tiketi kwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kupiga hatua mpaka kwenye Kombe la Dunia linalotarajiwa kufanyika mwaka 2022 nchini Qatar hasa baada ya michezo ya awali kuanza kuchezwa.

Hakika kwa sasa wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ wana kibarua kizito mbele ya Burundi baada ya kulazimisha sare ya kufungana bao 1-1 wakiwa ugenini.

Kwenye mchezo wa kwanza wa kufuzu hatua ya makundi uliochezwa nchini Burundi, Jumatano haikuwa rahisi kwa Stars kupata matokeo hayo kutokana na kushindwa kutumia nafasi za wazi ambazo walizitegeneza.

Pia ikumbukwe Stars ilikuwa ugenini kuna ugonjwa wa hofu ya uwanja ambao ulikuwa unawamaliza hasa dakika za mwanzo kwa kushindwa kuwa makini jambo lililopelekea sare ya kufungana bao 1-1.

Kwa hapo ambapo mabalozi wetu wamefanya wanastahili pongezi kwani wamevuna kile ambacho walikipanda na walistahili kutokana na juhudi ambazo walizionyesha bila kukata tamaa licha ya kuwa nyuma kwa bao moja.

Hapo kuna somo kubwa la kujifunza kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kwamba uwezo wa kuwafunga Burundi tunao nao pia wana uwezo wa kutufunga endapo tutashindwa kuwa makini.

Kikubwa ambacho kwa sasa inabidi kitazamwe kwa umakini na ukaribu ni mchezo wamarudio unaotarajiwa kuchezwa Septemba nane uwanja wa Taifa.

Wachezaji kwa hapo nini tena mnataka kwa sasa zaidi ya kutoa burudani kwa mashabiki? Ukizingatia uwanja ni wa kwenu nanyi mpo kwenye himaya yenu kinachotakiwa ni ushindi wa mapema na kufunga hesabu.

Matokeo ambayo yametokea Burundi piga ua huwezi kuyabadili abadani zaidi ya kubaki stori sasa kinachotakiwa kubadilishwa kwa sasa ni mfumo wa kufikiria kwa wachezaji wetu.

Wachezaji wetu wote wanapaswa wafikirie kwamba wanakutana na mchezo mgumu ambao unahitaji nidhamu ya hali ya juu pamoja na umakini.

Maelekezo ya benchi la ufundi pamoja na wale wachezaji wa zamani ambao wamekuwa wakisafiri na timu yakitendewa kazi kwa ufasaha basi kazi inakuwa imeisha mapema kabisa.

Kitu kikubwa kwa wachezaji kubadili mbinu zao ambazo walizitumia awali kwa kushindwa kuwa na maamuzi ya haraka hasa wanapokuwa karibu na eneo la hatari pamoja na kupoteza mipira kizembe.

Kazi ya kucheza na timu ambayo falsafa zinalingana ni ngumu kwani mbinu zote zinakuwa mikononi mwa wapinzani sasa ili kupenya kundi la namna hiyo akili ya ziada inahitajika bila kusahau juhudi.

Uwepo wa mashabiki ndani ya uwanja wa Taifa iwe ni silaha ya mwisho ya maangamizi kwa wapinzani wetu kwani kama ambavyo wao walikuwa wanajivunia nguvu ya mashabiki kwao basi sisi tuifanye kama silaha ya mwisho ili kuwapoteza jumla.

Mashabiki wote ni wakati wa kuungana kwa ajili ya Taifa Stars ili ipate matokeo chanya yatakayoipa nafasi ya kusonga mbele na kutinga hatua ya makundi kwenye michuano ya Kombe la Dunia.

Sio kazi nyepesi ingawa timu itakuwa nyumbani ni mpaka pale wachezaji wenyewe watakuwa na nia moja na kushirikiana katika kila hatua.

Ule ugumu wa kushindwa kuamua pamoja na uzembe usio na lazima ndani ya uwanja uishie kwenye mazoezi ndani ya uwanja ni kazi juu ya kazi mpaka kupata matokeo.

Kila la kheri Taifa Stars watanzania na wadau wote wanawatazama nyie kuona ni namna gani mtafikia yale malengo ya Taifa na timu kiujumla.

Furaha ya mashabiki imejificha kwenye matokeo na wenye kuamua matokeo ndani ya uwanja ni wachezaji ambao mmepewa dhamana ya kupeperusha bendera ya Taifa kimataifa, msiwaangushe watanzania.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic