Na George Mganga
Aliyewahi kuwa mchezaji na Kocha katika klabu ya Simba,
Jamhuri Kihwelo 'Julio', amesema kiwango alichonacho kipa Juma Kaseja hivi
sasa, Aishi Manula wa Simba hana nafasi ya kucheza Taifa Stars.
Julio amesema kwa kiwango alichokionesha Kaseja tangu
aitwe Stars na Kaimu Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije, ni bora na inaonesha
namna gani alivyo na uzoefu kumzidi Manula.
Julio
amefunguka akimwelezea Kaseja kuwa alisaadia Stars kuiondoa Kenya katika mechi
ya mwisho kufuzu fainali za CHAN 2020 baada ya kuibuka shujaa ikiwemo kudaka
penati moja huku Stars ikiibuka na ushindi wa mabao 4-1 kwa njia ya matuta.
Kocha huyo ambaye aliwahi kuinoa Simba, amefunguka kuwa
Manula amekuwa na uzembe ambao unamfanya afungwe mabao ambayo hauwezi tarajia,
kitu ambacho kwa Kaseja hauwezi ukakiona.
"Kwangu mimi Kaseja ni kipa bora kuliko Manula
sababu ya utofauti wa viwango baina yao wawili, Manula amekuwa akiruhusu mabao
ya kizembe kitu ambacho kimekuwa kikimharibia.
"Ndani ya kikosi cha Stars chaguo langu la kwanza
litabakia kwa Kaseja sababu namjua vema namna anavyocheza na anavyopambana, ana
uzoefu na yupo makini akiwa langoni.
"Kila mtu amemuona katika mechi alizochezwa tangu
arejeshwe Stars, sidhani kama unaweza ukampa nafasi Manula kwa namna
alivyowaonesha watanzania kuwa bado yumo," alisema.
Kwa upande mwingine, Julio amesema Manula si kipa mbaya
bali anajitahidi na anahitaji kujifunza zaidi ili kuboresha kiwango chake
tofauti na namna ambavyo amekuwa akionesha madhaifu langoni.
Ameongeza akisema, hata kikosi cha Simba bado Kaseja
anastahili kuwa namba moja tofauti na Manula sababu ya uwezo wake, japo
akieleza siasa za timu hiyo hazitaweza kumpa tena nafasi, akiamini kuna baadhi
ya viongozi hawamtaki.
"Kaseja hata sasa ningekuwa mimi ndiye Kocha
angesalia kuwa chaguo la kwanza na Manula angekuwa namba mbili, nasema haya
sababu anachokifanya kinajulikana, shida siasa za pale Simba zimesababisha hadi
leo asiwepo, najua kabisa kuna baadhi ya viongozi walisababisha aondoke."








0 COMMENTS:
Post a Comment