AZAM WAITISHA SIMBA, MIKAKATI YA KUIMALIZA KESHO YAANIKWA
Na George Mganga
Uongozi wa klabu ya Azam FC umeitangazia vita Simba kuelekea mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kesho Jumatano.
Ofisa Habari wa Azam, Jaffary Idd Maganga, amesema wataingia kukipiga na Simba wakiwa na faida ya kutokuwa na majeruhi mpaka sasa huku akieleza mchezo wa soka ni dakika 90.
Maganga amefunguka kwa kusema anajua kila timu inahitaji alama tatu akiahidi watapambana kwa namna wawezavyo ili kupata ushindi siku hiyo.
"Mpaka sasa hatuna mchezaji ambaye ni majeruhi hata mmoja.
"Tutaingia uwanjani kupambana tukiwa na malengo ya kusaka alama tatu, hivyo jukumu litabaki kwa Mwalimu na wachezaji.
"Kuhusu rekodi za nyuma hilo hatuwezi kulitazama sana, badala yake tunaangalia kinachofuata."
Simba ambayo itakuwa mwenyeji wa mchezo huo, itaikaribisha Azam ikiwa na kumbukumbu za ushindi wa mabao 4-2 katika mchezo wa Ngao ya Jamii iliyopigwa Agosti 17 mwaka huu.
Katika mechi hiyo, Azam itacheza mechi hiyo ikiwa na Kocha wake Mkuu mpya, Mromania Aristica Cioaba ambaye aliwahi kuitumikia timu hiyo miaka kadhaa nyuma.
Mromania huyo amekuchukua nafasi ya Mrundi Etienne Ndayiragije aliyepewa majukumu ya kuinoa Taifa Stars.








0 COMMENTS:
Post a Comment