October 15, 2019



   MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wameanza kazi kwa kasi msimu huu wakiwa na kikosi chenye mabadiliko makubwa kikiwa na kazi kubwa ya kutetea ubingwa wake iliouchukua msimu uliopita.

Simba ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo, msimu wa 2017/18 na 2018/19. Sasa ni msimu wa 2019/20 wameanza kuonyesha maajabu yao mapema.

Baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali na UD do Songo ya Msumbiji, hasira zilihamishiwa ndani ya ligi kuu na mpaka sasa wamefanya haya:-

  Mbinu za Mbelgiji

Patrick Aussems, raia wa Ubelgiji ambaye ni kocha mkuu wa Simba, amekuwa akibadili mbinu kutengeneza kikosi cha ushindi na amekuwa akibadili mbinu katika kila mchezo na kushinda zote.

Alianza na mfumo wa 4-3-3 walipocheza na JKT Tanzania, akashinda 3-1.Mbele ya Mtibwa akatumia mfumo wa 4-4-2 na kushinda 2-1.

Kagera Sugar, akatumia mfumo wa 4-4-2, akashinda 3-0, kisha  4-3-3 dhidi ya Biashara United, akashinda 2-0.

Dakika 360 za ushindi

Simba imecheza dakika 360 sawa na mechi nne, imeshinda zote tofauti na msimu uliopita walishinda  mbili dhidi ya Prisons (1-0) na Mbeya City (2-0) ambazo ni Uwanja wa Taifa, Dar. Ndanda ililazimisha sare ya bila kufungana Uwanja wa Nagwanda Sijaona, Mtwara,  ikafungwa 1-0 na Mbao Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Msimu huu imeshida mechi nne kwa kuifunga JKT Tanzania (3-1), Mtibwa Sugar (2-1). Hizi zilichezwa Uwanja wa Uhuru,  huku ule wa Kaitaba, waliifunga Kagera Sugar 3-0 na kuimaliza Biashara United kule Uwanja wa Karume mkoani Mara kwa mabao 2-0.


3.Rekodi ya ‘super sub’ ndani ya Simba

Miraj Athuman wa Simba ni usajili mpya ambao umekubali kujibu na kuonyesha maajabu ndani ya dakika 87 ambazo amecheza akitokea benchi na kubadili matokeo.

Alianza dhidi ya JKT Tanzania aliingia dakika ya 60 kuchukua nafasi ya Deo Kanda, alifunga bao dakika ya 68 Simba ilishinda mabao 3-1, Mtibwa Sugar, aliingia dakika ya 62 akichukua nafasi ya Hassan Dilunga, alifunga bao dakika ya 62 katika ushindi wa 2-1.

Ilipocheza na Kagera Sugar aliingia dakika ya 61 akichukua nafasi ya Deo Kanda, alisababisha penalti iliyofungwa na Meddie Kagere kwenye ushindi wa mabao 3-0.

Wawa ana balaa

Pascal Wawa ambaye ameongeza mkataba wa mwaka mmoja ameonyesha ubora akiwa beki kisiki kwani kwenye michezo miwili aliyoongoza safu ya ulinzi hakuna hata bao la kuotea lililotikisa nyavu za Aishi Manula.

Mchezo wa kwanza kwa Wawa ilikuwa mbele ya Kagera Sugar, Simba ilishinda mabao 3-0 na mchezo wa pili ilikuwa mbele ya Biashara United Simba ilishinda mabao 2-0.

Kagere yeye na nyavu

Meddie Kagere mpaka sasa amezionea nyavu mara sita ikiwa ni mara mbili ya msimu uliopita baada ya michezo minne alikuwa ametupia jumla ya mabao matatu na safari hii akiwa ameongeza kandarasi mpya amefunga jumla ya mabao sita ndani ya mechi nne.

 Wabrazil wana viwanja vyao

Simba imewasajili wachezaji watatu raia wa Brazil ambao ni Gerson Fraga, Tairone Santos na Wilker da Silva ambao hawa wana viwanja vyao maalumu, ujanja wa Aussems akigundua kwamba uwanja ni mbovu anabadilisha mbinu na kuwaweka benchi kama alivyofanya kwenye mchezo dhidi ya Biashara United.

Umiliki wa mpira

Ilipomenyana na Biashara United, Simba ilimiliki mchezo kwa asilimia 55, wakati wapinzani wakimiliki asilimia 45. Ilipomenyana na Kagera Sugar, iliongoza kwa umiliki wa asilimia 60 kwa 40.

Ilipocheza na JKT Tanzania uwanja wa Uhuru, Simba ilimiliki mpira kwa asilimia 55 kwa 45 na ule dhidi ya Mtibwa Sugar ilimiki kwa asilimia 61 kwa 39 ya wapinzani wake.
 Asisti, mabao ya kumwaga

Msimu wa mwaka 2018/19 kwenye jumla ya michezo minne, Simba ilitengeneza jumla ya asisti tatu pekee na kupata mabao matatu yaliyofungwa na Meddie Kagere, watengeneza asisti walikuwa ni John Bocco kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, Shiza Kichuya na Asante Kwasi kwenye mchezo dhidi ya Mbeya City.

Msimu huu Simba imefunga jumla ya mabao 10 huku watengeneza asisti za kumwaga ni Miraji Athumani ametoa moja sawa na Ibrahimu Ajib huku Sharaf Shiboub, Meddie Kagere na Mzamiru Yassin kila mmoja ametoa asisti mbili huku bao moja likifungwa kwa penalti.

Kinatoka chuma kinaingia chuma

Mpaka sasa Simba ina wachezaji ambao wakiwa benchi Mbelgiji anapasua kichwa amtoe nani ndani amuingize nani , kwa mfano kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania alimtoa Hassan Dilunga akaingia Miraj Athuman, pia alimtoa Clatous Chama akaingia Ibrahim Ajibu.

 Kila kiwanja wanachokanyanga ni mwendo wa mbili

Katika michezo minne waliyocheza, Simba imekuwa ikishinda ushindi wa mabao kuanzia mawili na kila kiwanja msimu huu walichogusa wamecheka na nyavu.

Uwanja wa Kaitaba msimu uliopita waliambulia maumivu kwa kufungwa mabao 2-1 ila msimu huu imeshinda mabao 3-0 huku ule wa Karume imerudia rekodi ya msimu uliopita kwa kufunga mabao 2-0 ikiwa nyumbani haijapoteza mchezo hata mmoja.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic