KISA WARABU MABOSI YANGA WAIHAMISHA TIMU
Yanga ni kama imeshtukia jambo hivi, kwani baada ya kusikia kwamba wapinzani wao katika mchezo wa Kombe la Shirikisho, Pyramids kwamba watafikia katika hoteli ya kifahari ya Malaika iliyoko wilayani Ilemela nje kidogo ya Jiji la Mwanza, nao wakafanya maamuzi.
Kutokana na taarifa hizo, Yanga ikaamua kuhamia katika Hoteli ya Victoria Palace ikitokea MY Hotel walikofikia awali tangu walipowasili jijini hapa Oktoba 19, mwaka huu kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wake na Pyramids kutoka nchini Misri utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema sababu kuu ya wao kuhama hoteli waliyofikia tangu mwanzo ni kuwa, tangu walipowasili jijini hapa hoteli walizopanga kufikia zilikuwa zimejaa.
“Tangu tulipowasili Mwanza hoteli zote tulizopanga kufikia zilikuwa zimejaa wageni, hivyo ikatulazimu kukaa katika Hoteli ya MY tukisubiri wageni wapungue ndiyo maana tumeamua kuhamia Victoria Palace ili wachezaji wetu wakae eneo lenye utulivu kama tulivyokuwa tumepanga,” alisema.
Bumbuli amewaomba mashabiki wao wajitokeze kwa wingi katika mchezo huo ili kuisapoti timu yao na kuipa nguvu kwa kuwa wanaamini shabiki ni mchezaji wa 12 uwanjani.
0 COMMENTS:
Post a Comment