October 25, 2019


 OCTOBA 27, Taifa kwa muda litasimama kutazama namna wawakilishi wetu  wa kimataifa watakavyopambana kwa ajili ya kupeperusha bendera ya Taifa.

Utakuwa ni mchezo ambao utashika hisia za wadau wengi wa soka kutokana na umuhimu wake na ushindani ulivyo jambo ambalo tayari limeanza kuonekana kabla ya pambano.

Rekodi zinaonesha kuwa msimu huu Yanga haijafanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa katika mechi zake zote ilizoanzia nyumbani kwa kuwa hakuna ushindi zaidi ya kuambulia sare.

Yanga ambayo ilianzia safari yake kwenye Ligi ya Mabingwa ilipigwa chini na Zesco kwa jumla ya mabao 3-2 jambo lililoidondosha jumla kwenye Kombe la Shirikisho.

Mchezo wao wa kwanza hatua ya awali dhidi ya Township Rollers uwanja wa Taifa ilikubali sare ya bao 1-1 ikajiongezea mzigo ugenini ikashinda bao  1-0 lililoipeleka mbele.

Mambo yakazidi kuwa magumu tena kwani mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani uwanja wa Taifa walikubali kulazimisha sare ya bao 1-1 na Zesco na kwenye mchezo wa marudio kichapo cha mabao 2-1 kiliwahusu na safari yao ikaishia hapo.

Kwa sasa wapo kwenye kombe la Shirikisho na wana michezo miwili mkononi ambayo itaamua nani asonge mbele hivyo kazi kwa benchi la ufundi ni kufanyia makosa kazi waliyoyafanya kwenye hatua ya Ligi ya Mabingwa.

Licha ya kuwa na nafasi ya kutinga hatua ya makundi Yanga ilikwama kutokana na kushindwa kutumia nafasi walizokuwa wakizipata pamoja na mbinu ngumu ambazo walikuwa wakizitumia.

Ukubwa wa kazi upo uwanjani na sio kwenye maneno hapo kila mmoja ni mshindi, Yanga inapaswa itulie na ifanye kweli kiufundi na kupata ushindi.

Nimeona kwamba wameamua kuhama uwanja wa Taifa na kukimbilia Mwanza hakuna haja ya kujipa ushindi jumla kisa uwanja umebadilika.

Kama uwanja umebadilika basi na mbinu inabidi zibadilike kuanzia kwa wachezaji na benchi la ufundi katika kusaka ushindi kwenye mechi ya kwanza itakayopigwa Oktoba 27 uwanja wa CCM Kirumba.

Wapinzani wa Yanga ambao ni Pyramids ukiwatazama unaweza kudhani ni wa kawaida ila rekodi zao zinawabeba ukali wao hauchagui uwanja iwe nyumbani ama ugenini wao wanashinda tu.

Katika michezo yao waliyocheza wamekuwa na ushindani mkubwa na jambo ambalo linatakiwa kutazamwa kwa haraka ni kasi yao wawapo uwanjani na wanasifa ya kutafuta matokeo mapema kisha wanamaliza kwa kupaki basi.

Hapo ndipo benchi la ufundi linapaswa litazaame mbinu za mpinzani na kisha kujipanga kupambana kufa na kupona kupata ushindi ndani ya dakika tisini.

Ikumbukwe kuwa rekodi za Yanga msimu huu uwanja wa Taifa zimewahukumu na wameamua kusepa Mwanza ambako nako pia rekodi zinaonyesha kwamba ni sawa na uwanja wa Taifa kwani kwenye michezo mitatu ambayo walicheza hapo hakuna hata mmoja ambao walishinda kimataifa.

Ni wazi kwamba Yanga wana kazi kubwa na ngumu ya kufanya kupeperusha bendera ya kimataifa na hilo ndio ambalo mashabiki na Taifa kiujumla linahitaji kuona.

Mashabiki wa Mwanza ni wakati sahihi wa kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu yao ambayo kwa muda mrefu haijatumia uwanja wa Mwanza kucheza michezo ya kimataifa.

Kujitokeza kwa wingi kutawapa nguvu wachezaji kutafuta matokeo chanya kwenye mchezo wao ambao ni mgumu na wa ushindani mkubwa.

Kila mchezaji anapaswa atambue kwamba watanzania wanawaamini na wanawategema jambo ambalo linapaswa liwape hasira katika kutafuta matokeo ndani ya uwanja.

Kujituma kwenu kutawapa raha mashabiki na kufuta yale maumivu ambayo walikuwa nayo awali hasa ukizingatia kwamba hakuna ushindi ambao umepatikana kwenye mechi za kimataifa zilizochezwa nyumbani.

Mbinu ya kujilinda nyumbani itakuwa ngumu kwa Yanga kushinda kwani kujilinda kunatoa ruhusa ya kushambuliwa na presha ikiwa kubwa ni rahisi kupoteza.

Kila la kheri wachezaji na mashabiki pia mjitokeze kwa wingi kuipa sapoti timu kila kitu kinawezekana na wakati wa ushindi ni sasa hakuna wakati mwingine.



1 COMMENTS:

  1. Nenda kamusaidie kocha kwani kila baada ya dakika mbili unaanza kulaumu. Kazi yako siyo kulaumu sisi wapenzi wa Yanga hatuko upande wako. Haya ni mawazo yako iache timu yetu icheze huru Jumapili.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic