NA SALEH ALLY
WAKATI nimeanza kuandika habari za michezo katikati ya miaka ya 1990, kila kizuri ambacho ulitaka kukiandika kuhusiana na michezo na hasa soka, kilikuwa migogoro.
Kulikuwa kumejaa migogoro iliyopindukia kuanzia Yanga, Simba hadi Chama cha Soka Tanzania (FAT). Mjanja ni yule aliyekuwa na uwezo mkubwa wa fitna.
Klabu na FAT ilikuwa ni mali ya watu, maana walifanya walivyotaka na hakukuwa na mwenye uwezo wa kuwaangusha, hawakushikika.
Wako walianza kuamini kuwa na nguvu hata kuliko Serikali, wakati huo ndio kulikuwa na makundi ya wanachama yenye nguvu kupita hata baadhi ya viongozi wa klabu zenyewe.
Majina ya Komandoo, yalianzia kipindi hicho. Wakati makomandoo walipigana jeshini, wako watu walijiona wanastahili majina hayo ni kama wanaharakati au wanazipigania klabu zao.
Bahati mbaya hadi FAT nako kulikuwa na makomandoo na wakati fulani “jeshi” la mwenyekiti likapambana ile mbaya na “jeshi” la katibu mkuu.
Upuuzi huu ndio ulichangia kwa kiasi kikubwa hadi baadhi ya matawi ya klabu za Simba na Yanga kujulikana kwa migogoro kutokana na kutumiwa na baadhi ya viongozi katika harakati zao za kuendeleza migogoro ili watawale wanavyotaka si inavyotakiwa.
Kweli kabisa baadhi ya makundi yalikuwa sumu kali katika suala la maendeleo ya klabu hizo kongwe. Matawi hayo yalianzisha na kuongoza migogoro, lengo kufanikisha anachotaka kiongozi fulani na kumuangamiza mwingine bila ya kujali nini kitakosekana au kitakuwa hasara kwa klabu.
Nimepita katika kizazi cha mapambano kubadili hata aina ya kuripoti, kutoka kutegemea taarifa za migogoro na badala yake kuangalia zaidi zile za uwanjani, mapato kiasi gani, nani mdhamini na mechi inachezwa vipi uwanjani, yaani utaalamu.
Hali ilivyo sasa ni tofauti na miaka hiyo tena kwa kiasi kikubwa. Nguvu ilikuwa kubwa na huenda haijawahi kuonekana lakini kupungua kwa fitna kupindukia, kumesaidia mambo mengi kubadilika na hasa angalau watu kuanza kuwaza maendeleo badala ya malumbano tu.
Wakati tumeingia kwenye mabadiliko hayo, ni miaka mingi sasa. Kumi au takribani ya hiyo inafika. Lakini wako ambao bado wana hisia yale ya zamani yapo sana.
Matawi mengi ya klabu za Yanga na Simba kwa sasa yangeweza kuwa na faida kubwa sana na kusaidia mambo mengi ya maendeleo ndani ya klabu hizo, lakini yanaogopwa.
Bila shaka, viongozi wa Yanga kwa asilimia 90 walikuwepo kwenye mpira kama viongozi au wadau katika miaka hiyo. Wanajua kilichokuwa kinatokea, huenda inachangia wao kuyaona matawi ni kama tatizo vile, hakuna anayeyatumia chanya.
Matawi yangeweza kupangiwa utaratibu mzuri kusaidia katika mambo mengi. Uuzaji wa jezi, kuitangaza klabu katika maeneo yao, kuandaa mashindano na kadhalika.
Watu wa matawi wanaweza kuwa mabalozi wazuri wa Yanga na Simba mikoani na sehemu nyingine. Wanaweza kuwa wawakilishi wazuri katika wilaya na vitongoji na wakawa wanaruhusiwa kuwa na mawazo yao huru ikiwa ni sehemu ya kuzisaidia klabu zao na wao wakaingiza chao ambacho kitawasaidia kujiendesha kama matawi.
Yanga na Simba wanapaswa kutanua wigo, kufikiri kwa upana zaidi na matawi ni sehemu nzuri kwao kuwasaidia kujipambanua zaidi na kujitanua kibiashara kwa kuanzia chini.
Hakuna anayebuni jambo kupitia matawi na hisia za kale za kuamini matawi ni hatari, bado zinaonekana kuwa na nguvu sana, jambo ambalo ni hatari sana.
Mara nyingi unachoona kilisaidia kubomoa, maana yake ni hasi. Ukiwa mbunifu unakigeuza na kuwa chanya na kinakusaidia kujenga. Yatumieni vizuri matawi yawasaidie.
0 COMMENTS:
Post a Comment