October 4, 2019


Tungo tata ni moja kati ya njia nzuri ya msanii kufikisha ujumbe wake kwa hadhira. Tungo tata zina utamu wake, zinamfikirisha msikilizaji ili aweze kupima na kuibuka na majibu ambayo yeye anaamini msanii husika atakuwa amekusudia.

Wimbo wa Kijiwe Nongwa ni moja kati ya nyimbo ambazo zimetoka hivi karibuni na kukamata watu kwelikweli, habari ikufikie kwamba mpaka muda ambao naandika makala haya Kijiwe Nongwa umetazamwa na watu wasioupungua Milioni 1.

Wimbo huu wa Roma na Stamina ambao wamemshirikisha Nay wa Mitego ambao kwenye mtandao wa YouTube umepandishwa Septemba 20, mwaka huu, unayo mistari mingi mitamu na ya kusisimua lakini makala haya yanakuchambulia ile mistari ambayo ina nongwa kwelikweli, ujumbe wake unatupa vijembe kwa watu wengine bila kuusahau ule uliotoa majibu kuhusu madai ya muda mrefu kuhusu ndoa zao kuvunjika!

MAREHEMU WALIMSEMA MNYONYAJI…KWANI MUZIKI UNA MAZIWA…

Hapo wakali hao wamewachana wasanii waliokuwa wakilalamika mdau mkubwa wa burudani aliyefariki kwamba alikuwa anawaminya wasanii wasiweze kutoboa, matokeo yake mdau huyo hayupo tena duniani na wale waliokuwa wanalalamika bado hawafanikiwi kimuziki.

BABU WA LOLIONDO YULE MWENYE BLICHI LA KIKONGO… SASA UCHAGUZI UMEKARIBIA AMERUDI CHAMA TAWALA…

Hili ni dongo kwa kiongozi mkubwa wa kisiasa ambaye inaonekana alikuwa upande wa upinzani, akapigania haki lakini baada ya uchaguzi mkuu 2015, amerejea kwenye chama tawala.

ALIKUJA KAMA MASII, TUKAMCHANGIA SADAKA…NA BADO WAKAMLAZA MUUMINI KIFO CHA MENDE.

Hili nalo ni dogo kali kwa kiongozi mmoja wa dini ambaye awali alionekana alikuwa akipata waumini wengi, akiaminika lakini baadaye alipata aibu ya kukutwa na muumini wake faragha.

ALIYEOKOTA ALMASI MCHANGANI ALIKUWA MISS TANZANIA, NA ALIYEKUJA INUNUA DUKANI NI MGANDA ALIYEKUWA NA NIA…

Dongo kwa msanii mkubwa wa Bongo Fleva ambaye anasifika kwa kuwamaliza warembo na mwishoni Roma amemchana kuwa msanii huyo ni mnyanyasaji wa kijinsia.


NIAMBIE MAANA YA TFF…
Hapa wasanii hawa wamejaribu kufikisha ujumbe kwamba shirikisho la soka halikuwa sahihi kumuondoa mmoja wa makocha waliokuwa wakiinoa Timu ya Taifa Stars.



VIPI DADA YETU WA IGUNGA, MH SIMUONI UDANGANI… FUNDI YULE FUNDI GEREJI CHAWA SI KAMTEKA BIBIE NA WAMEFUNGUA MGAHAWA YANI WOTE MAMA N’TILIE.
Hili ni dogo la wazi kwa msanii mmoja wa Bongo Fleva ambaye amefungua mgahawa yeye na mumewe, msanii huyo naye nasikia amemaindi na amewajibu.

SA SIKIZA MAN, VIPI SHEMU MAMA IVAN? TUPOTUPO TU ILA SI KAMA ZAMANI… NAWE VIPIB KWANI, MBONA WIFE SIMUONI NYUMBANI? CHILL MAN, SINA MAJIBU DEAL DONE.

Hapa wamejipiga madogo wao wenyewe, wametoa majibu ya kile kilichokuwa kikizungumzwa kwa muda mrefu kwamba ndoa zao zinapumulia mashine. Ndoa zilitajwa kuwa kwenye migogoro ya muda mrefu na wamedhihirisha wao wenyewe kwenye wimbo huo kwani Roma amesema ‘tupo tupo si kama zamani’ na Stamina naye amejibu ‘deal done’ hali ambayo inaashiria kabisa ndoa zao zilitetereka na huenda kwa sasa bado hali ni si hali.

BONGO BWANA NDIO NCHI INAYOSAPOTI SANA UJINGA…

Huu nao ni miongoni mwa mstari unaowachana Watanzania ambao wanaendekeza kushabikia mambo ya kijinga yanapoibuka kwenye mitandao ya kijamii. Wametolea mfano Mariamu Biriani na Amber Rutty!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic