NYOTA SIMBA, MOLINGA ATAIBEBA YANGA
Mambo ni moto ndani ya Yanga. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya benchi la ufundi la timu hivi sasa kuwa katika harakati kabambe za kuhakikisha wachezaji wake wanakuwa fiti tayari kwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya Pyramids ya Misri.
Hata hivyo, wakati maandalizi hayo yakiendelea, kiungo mshambuliaji wa zamani wa Simba, Uhuru Selemani ambaye sasa anakipiga katika timu ya soka ya DC Motema Pembe ya DR Congo, ameitabiria makubwa Yanga katika mchezo huo utakaochezwa Oktoba 27, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Uhuru ameliambia Championi Jumatatu kuwa kitendo cha mshambuji wa timu hiyo raia wa DR Congo, David Molinga ‘Falcao’ kupata kibali kitakachomruhusu kucheza mechi hiyo, ni moja ya chanzo kikubwa kwa Yanga kufanya vizuri dhidi ya Waarabu hao wa Misri.
Alisema Molinga ni bonge la mshambuliaji ambaye nchini DR Congo jina lake ni kubwa na wachezaji wengi nchini humo wanaamini kuwa ataisaidia Yanga kufanya vizuri katika mechi hiyo lakini pia Ligi Kuu Bara.
“Baada ya mimi kutua DC Motema Pembe kila mchezaji alikuwa akimzungumzia Molinga ambaye huko anajulikana kwa jina na Falcao.
“Wanasema kuwa ni bonge la mshambuliaji, anajua sana kufunga, sema tu kabla ya kuja Yanga alikaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi sita bila kucheza kutokana na kuwa majeruhi. Kwa hiyo Yanga wampatie muda tu kwani kutokana na jinsi wanavyomzungumzia huko DR Congo naamini atawasaidia hata katika mchezo dhidi ya Pyramids anaweza kufanya vizuri kutokana na kuwa na uzoefu na mechi za kimataifa,” alisema Uhuru.
Katika hatua nyingine rekodi zinaonyesha kuwa tangu Molinga atue Yanga akitokea DR Congo, amefanikiwa kufunga mabao manne mpaka sasa kwenye mechi zote alizocheza zikiwemo za kirafiki.
Mabao mawili amefunga kwenye mechi za kirafiki na mengine katika mechi za ligi kuu ambazo mpaka sasa Yanga imeshacheza.
Rekodi hizo pia zinaonyesha kuwa Molinga ndiye mshambuliaji pekee wa Yanga aliyezifumania nyavu katika michuano ya ligi kuu na ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi.
CHANZO: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment