LEO nchini
Sudan, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Etienne
Ndayiragije atakuwa na kazi ngumu ya kupindua meza kibabe mbele ya Sudan kwenye
mchezo wa kutafuta tiketi ya kufuzu
michuano ya CHAN ambayo inawahusisha wachezaji wa ndani.
Mchezo huu
utapigwa uwanja wa El Merriekh, Omdurman ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa
kufungwa bao 1-0 uwanja wa Taifa jambo ambalo limeongeza mlima mzito kwa timu
ya Taifa kupata ushindi.
Rekodi
zinaonyesha kwamba, Ndayiragije hajawa na bahati ya kupata ushindi katika
michezo sita ambayo ameiongoza baada ya kukabidhiwa timu kutoka kwa Mnigeria,
Emmanuel Ammunike kwa kushindwa kupata ushindi ndani ya dakika 90.
Kwenye michezo
hiyo sita safu yake ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao mawili pekee huku
ikikubali kufungwa jumla ya mabao matatu ambapo imepoteza mchezo mmoja mbele ya
Sudan ambao wanarudiana nao leo, sababu zinazofanya mtihani kuwa mgumu hizi
hapa:-
Hajaambulia ushindi ndani ya dakika
90
Ndayiragije
kwenye michezo sita aliyoongoza hajaambulia ushindi ndani ya dakika 90 zaidi ya
sare na kufungwa.Taifa Stars ilianza kupata sare ya bila kufungana na Kenya
kwenye mchezo wa CHAN uwanja wa Taifa, mchezo wa marudio uliopigwa Kenya
matokeo ilikuwa ni 0-0 Stars ilishinda kwa penalti 4-1 ikasonga mbele na
kukutana na Sudan ambapo ilipoteza mchezo wa kwanza uwanja wa Taifa kwa
kufungwa bao 1-0.
Mechi
nyingine ilikuwa dhidi ya Burundi kwa ajili ya kusaka tiketi ya kuwania kufuzu
makundi ya Kombe la Dunia mchezo wa kwanza ilikuwa sare ya bao 1-1 na mchezo wa
marudio uwanja wa Taifa sare ya bao 1-1 na Stars ilishinda kwa penalti 3-0.
Mchezo
wake wa sita ilikuwa dhidi ya Rwanda ambao ulikamilika kwa sare ya bila
kufungana.
Ubutu wa safu ya ushambuliaji
Mpaka sasa
kwenye michuano ya Chan hakuna mshambuliaji ambaye amefunga bao jambo ambalo
linampasua kichwa Ndayiragije na benchi nzima la ufundi linaloundwa na Seleman
Matola pamoja na Juma Mgunda ambaye aliweka wazi kwamba kuna janga kwenye safu
ya ushambuliaji.
Mabao mawili
ambayo Stars imefunga yalipachikwa kimiani na wafungaji wanaokipiga nje ya
Bongo ambao ni Mbwana Samatta nahodha anayecheza KRC Genk na Simon Msuva
anayekipiga Difaa El Jadida ya Morocco.
Pengo la Bocco na Aiyee
John Bocco
kwa sasa bado hajarejea kwenye ubora wake kutokana na kusumbuliwa na majeraha
ya goti ambayo aliyapata kwenye mchezo dhidi ya Azam FC kukosekana kwake ndani
ya kikosi cha Taifa Stars kumekuwa kukiwapa taabu makocha kumtafuta mbadala
wake ambae imekuwa ngumu kumpata.
Salum Aiyee
anayekipiga KMC naye amekuwa nje ya timu ya Taifa kutokana na kusumbuliwa na
majeruhi, licha ya kutokuwa na muda mrefu ndani ya timu ya Taifa ni miongoni
mwa washambuliaji wazawa ambao wanalijua lango kwani msimu uliopita alifunga
jumla ya mabao 18 jambo linaloongeza ugumu kwa Ndayiragije.
Mfumo wa Ndayiragije
Asili ya
Ndayiragije muda mwingi ni kujilinda kwani kwenye mechi sita alizosimia timu ya
Taifa ya Tanzania ameambulia sare tano ndani ya dakika tisini na kupoteza mchezo
mmoja dhidi ya Sudan ambao ulichezwa uwaja wa Taifa.
Mmachinga anatoa somo hili
Mshambuliaji
wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ ambaye ni
Kocha wa timu ya Vijana ya Yanga, alisema kuwa tatizo kubwa inatokana na wachezaji
wengi kushindwa kujitambua na kuwa na papara wakiwa eneo la hatari.
“Kuna
umuhimu wa kocha kubadili mbinu hasa ukizingatia amekuwa akipata sare michezo
yake mingi, tatizo la ushambuliaji lipo kwa wachezaji wetu ila linapaswa
litafutiwe dawa na benchi la ufundi, jambo la msingi ni wachezaji kupunguza
papara wakiwa eneo la hatari itasaidia kupata matokeo chanya,” alisema.
Julio pia aongeza neno
Jamhuri
Kihwelo ‘Julio’ Kocha wa zamani wa Simba na Dodoma FC alisema kuwa wachezaji wa
timu ya Taifa wanapaswa wapambane kufa na kupona kupata matokeo chanya licha ya
kuwa ugenini nafasi ya kushinda ipo mikononi mwao.
“Ushindi
kupatikana ni mbinu na kujituma kwa wachezaji ndani ya uwanja na sio maneno,
ninaona kuna uwezekano kwa timu kupata matokeo chanya iwapo wachezaji
watajituma na kutimiza majukumu kwa wakati ndani ya uwanja,” alisema Julio.
0 COMMENTS:
Post a Comment