October 14, 2019



ZUBER Katwila, Kiongozi wa benchi la ufundi kwenye timu ya Taifa ya Vijana chini ya Miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ anastahili pongezi kwa alichokifanya.
Benchi la ufundi kiujumla linastahili pongezi kubwa kwa kufanya kazi ngumu na yenye heshima kwa Taifa letu wakiwa ugenini.
Walikuwa wanapambana kwa ajili ya Taifa nchini Uganda na mwisho wa siku wanarejea na ubingwa wa michuano ambayo inahusisha timu za Afrika Mashariki na Kati kwa kutwaa ubingwa wa CECAFA.
Haikuwa kazi rahisi kufikia mafanikio kutokana na ushindani ulikuwepo kwenye timu zote na mpaka sasa kila mtanzania anafurahia matunda ya timu ya vijana.
Kufikia mafanikio ni suala la kuamua na kuweka nia kama ambavyo imekuwa kwa Ngorongoro ambao kwa sasa ni mashujaa.
Wachezaji chukueni tano za nguvu kutokana na  kujitambua mlipokuwa uwanjani kwani kazi mliyofanya inaonyesha mmekomaa na mna uchungu na Taifa.
Safu ya ushambuliaji iliyokuwa chini ya Kelvin John na Andrew Simchimba imefanya kazi kubwa na tunaona kwamba John ni miongoni mwa wachezaji ambao wana mwenendo mzuri katika soka.
Mkiwa uwanjani wachezaji mlitambua ni nini mnatakiwa kufanya na wakati gani hatimaye mmevuna kile ambacho mmekipanda nasema mia kwenu.
Kwa mafanikio mliyoyapata msijisahau na mkadhani mafanikio yataendelea kuwafuata endapo mtapumzika na kusahau yote mliyojifunza.
Mna kazi ngumu na kubwa kulinda viwango vyenu na juhudi ambazo mmezionyesha ziishi siku zote kwenye maisha yenu ya soka popote mtakapokuwa.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) hamuwezi kukwepa pongezi kwani zinawahusu katika hili kutokana na kuwapa sapoti vijana mwanzo mwisho.
Hii inatokana na uwekezaji ambao mmeshtuka na kuanza kuufanya kwa vijana wenye vipaji ndani ya Taifa hilo ni jambo la msingi na linatakiwa kuwa endelevu.
Hili ni somo kwa kila mmoja bila kusahau TFF kwamba kuna deni jingine ambalo mnatakiwa kulilipa mapema kwani maana halisi imejificha kwenye matokeo.
Kushinda kwa timu ya vijana kuna maana ambayo ni lazima itafutiwe majibu ya jumla,maana yake inatokana na uwezekezaji kwa vijana ni jambo ambalo linapaswa liwe endelevu siku zote.
Somo hili la uwekezaji ni lazima likae sawasawa kwa kila mmoja kichwani kutokana na kuona kwamba kwa sasa kila mmoja anachekelea mafanikio ili hali ni lazima tuangalie na wakati ujao.
Tukizitazama nchi ambazo zimefikia mafanikio kwenye suala la michezo hazikufika huko ghafla bila kujua wapi zimetokea ziliwekeza kwa vijana.
Ukitazama Taifa la Argentina, Hispania kuna vituo vingi maalumu kwa ajili ya kulea vijana kwa lugha yao wanaita ‘academy’ ni vitu vya msingi kuwepo ndani ya nchi.
Endapo Tanzania kutakuwa na vituo vingi vya vijana na vinafuatiliwa kwa kupewa huduma stahiki shida zote kwenye michezo zitawekwa chini na tutakuwa bora muda wote.
Huu ni mzigo kwa TFF kuamua  na kujitoa kuwekeza kwenye soka la vijana jumla na sio kwa kuungaunga ili mradi mambo yaende si sawa kwa nchi inayotafuta mafanikio.
Tukubali tukatae sisi tuna uchache wa wachezaji wenye uwezo kutokana na uhaba wa vituo vya kuwalea vijana wetu ambao ni msingi wa maendeeo ya mpira.
Hii inafanya timu ya taifa kuwa na wachezaji walewale ambao wanajirudia mara kwa mara jambo ambalo linadumaza mafanikio yetu kufika pale ambapo tunahitaji kufika.
Kuna ulazima wa kuona kwamba tunapata wachezaji wengi na wenye ubora kwenye soka la Tanzania na ni sehemu moja pekee ambayo inaweza kutengeneza wachezaji bora na makini kwenye ligi ya vijana pamoja na vituo vya kuibua vipaji.
Watanzania wanapenda mpira na raha ya mpira ni kupata matokeo chanya hakuna nafasi kwa timu kupata nafasi chanya iwapo maandalizi ni chini ya kiwango.
Hatua ambayo tumefikia kwa sasa ni kubwa kiasi hatupaswi kujisahau tukiamini kwamba tumefika ilihali bado safari inaendelea.
Bado TFF haipaswi kuwaacha vijana wetu wakipotea jumla bila kuwa na msaada wowote kwani itawapoteza kweye ramani ya soka .
Vijana wetu wana deni kubwa sawa na TFF kuendeleza kuwekeza na kuandaa ligi ya Vijana ili kuwapa nafasi ya kuibua vipaji vingi zaidi ya hapa.
Naona mwanga upo kidogo kwa kule tunakoelekea hii inaleta picha nzuri na inaleta maana halisi ya kukua kwa soka kwani kama vijana wanakua ni maana halisi kwamba wanakwenda kuvunja ule ufalme uliokaa muda mrefu.
Ushindani ni kitu kisichoepukika kwa wachezaji wote ambao wanacheza kwa sasa, makocha nao wana kazi ya kufanya kuibua vipaji zaidi katika kile ambacho wanakifanya.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic