November 15, 2019







Na Saleh Ally, aliyekuwa Johannesburg
JUZI Jumatano, Banda alielezea mambo kadhaa kuhusiana naye na maisha yake nchini Afrika Kusini.


Akafafanua kuhusiana na namna alivyoishi bila ya kuwa na mashahara kwa miezi miwili.


Muda wote huo alianza kuishi kimyakimya, bila ya kuzungumza jambo lolote na akafanikiwa kuendelea na matibabu hadi aliporejea katika hali yake.


Banda sasa yuko katika kikosi cha Highlands Park cha jijini Johannesburg. Kikosi hicho kinashiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini maarufu kama PSL. Maisha kwa kwake yanaendelea lakini bado hajapata namba.


Banda ambaye ni beki wa zamani wa Coastal Union na Simba, ameliambia gazeti hili kwamba katika kikosi chake kuna mabeki wa kati tisa. Yaani set mbili na beki mmoja.


Swali lilikuwa ataweza vipi kupata namba katika kikosi ambacho kina wachezaji wengi kwa kiwango hicho katika namba mbili tu? Mwenyewe anajiamini.


“Kweli ni changamoto kubwa, huwezi kusema utawasukuma tu uingie. Lakini lazima nipambane niingie kwenye nne bora ambayo naweza kupata nafasi ya kucheza.


“Nina advantage kidogo, mabeki wote nane wanapiga mguu wa kulia kasoko mimi ninayepiga kwa mguu wa kushoto. Hii ni sehemu ambayo itanisaidia kusogea karibu.


“Nakumbuka wakati wa mazoezi, taratibu nilianza kupata nafasi ya kucheza mechi za kirafiki, baadaye nikasafiri.


“Mechi moja ya ligi nimecheza dhidi ya Mamelodi Sundowns na tulipoteza kwa bao 1-0. Lakini tayari imenipa matumaini ya kucheza tena.


“Niliingia katika kipindi cha pili na yalikuwa ni mabadiliko ya kiufundi tu ya mwalimu. Baada ya kuwa nimekaa nje kwa miezi sita hadi tisa, lakini kuingia uwanjani imenipa matumaini makubwa kuwa sasa naweza kurejea tena,” anasema Banda.


Je, bado ana matumaini makubwa kuwa ataingia hadi kufikia kuwa tegemeo.


“Ninajiamini sana tena sana, lakini ni suala la muda. Ninatatizwa na kitu kimoja tu, hii timu inacheza mpira kama ule wa Stock City. Hawa hawachezi, maana yake wao wanapiga pasi chache tu.


“Kwa kifupi hawawezi kucheza zile pasi ndogondogo na kweli natakiwa kufuata mfumo wa timu lakini nimekuwa nikijiuliza kwa kuwa na mimi ninataka kujiuza, yaani niko sokoni. Sasa kama nikiendelea hivi mwisho wangu utakuwa nini, nitauzika kweli?


“Kwa mfumo wa Highlands Park unatakiwa kukimbia na mtu wako hata kama atakimbilia langoni mwao. Kweli ni ugumu sana na muda wote ni kukaba tu, inanipa ugumu na nimekuwa nikiendelea kupambana kujitahidi kuweza kucheza mfumo huu ili niuweze lakini sitaki kutoka kabisa katika mfumo ninaoona unaweza kunibeba siku nyingine kama nitahama,” anasisitiza Banda.


“Ingekuwa ni maoni binafsi naweza kusema mfumo umenishinda lakini nasisitiza unapocheza timu tofauti unazidi kujifunza mambo taratibu. Kwa mwalimu anachotaka ndicho kinakuwa ni sahihi na mimi naendelea kukifanyia kazi lakini bado nasisitiza, bado niko sokoni na ninataka kuwa tayari kwa kucheza au kuzivutia na timu nyingine na hii ndiyo maana ya mafanikio.



“Ndiyo maana nimekuwa nikisema, nataka timu inayocheza zaidi. Mpira ambao tunaweza kupambana na kucheza mpira pia na si kukaba pekee kama ambavyo mfumo tunaoutumia hapa.”


Banda anasema katika mechi aliyocheza aliingia dakika 20 za mwisho lakini akagusa mpira mara moja tu.


“Ndiyo mara moja, tena ulikuwa ni mpira wa kichwa. Kwa kweli kuna ugumu sana na ninaendelea kupambana nikiangalia huenda mambo yatabadilika.


“Kama mambo yataendelea hivi na mfumo ni huu, mwakani mwezi wa tano, nitaomba kwa timu kuwa ninaomba nafasi wanitafutie sehemu au waniruhusu niondoke na hii naona itanisaidia kucheza katika sehemu ambayo itakuwa ni sehemu ya maisha yangu ya baadaye ya mchezo wa soka.”



Banda anaona anaweza akaondoka kutoka Highlands Park na kupata timu nyingine. Je, akipata timu ipi ambayo anaona anaweza kucheza kama akipata nafasi ya kuondoka?


USIKOSE KESHO KATIKA BLOG HII YA SALEHJEMBE.


2 COMMENTS:

  1. Hapo unaweza kuona tofauti kati ya mpira wetu na nchi hiyo. Kama kwa Simba alikuwa mchezaji tegemeo lakini huko yuko timu ambayo hata haijulikani, bado tuna safari ndefu. Pengine alikuwa na haraka ya mafanikio. Angesubiri kama walivyoenda kina Kotei ambao wamepata timu kubwa.

    ReplyDelete
  2. Enter your comment...ana miaka mingapi ametoka Simba? pia angalia mfumo wa uchezaji wa timu.

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic