November 29, 2019


WIKI iliyopita kwenye Championi Jumatatu tuliishia kuona maisha ya Dida ambaye ni mlinda mlango wa zamani wa Simba akizungumzia kuhusu maisha yake ya shamba na kugusia kidogo kuhusu mipango yake ya soka.

Huyu hapa leo anaendelea kuzungumza juu ya maisha yake na soka endelea; “Nime kuwa nikieleza mara kwa mara kwamba suala la mimi kujishughulisha na masuala ya ukulima siyo jambo la kushtua kwani ni kitu ambacho nakimudu na ninakipenda.

JEMBE GANI UNATUMIA? “Kuanza kulima natumia trekta ambalo hilo linafanya kazi yake ila maandalizi ya shamba ninatumia jembe la mkono.

Wakati wa kupalilia natumia pia jembe la mkono kwani katika muda huo haiwezekani ukatumia trekta.

MAZAO YAKO NI KWA AJILI YA NINI? “Mazao yote ni kwa ajili ya vitu vyote viwili yaani kwa chakula na biashara. Nafanya hivyo kwa sababu nina machaguo yote mawili kwa wakati mmoja.

UNAKUTANA NA UGUMU GANI KATIKA KULIMA?

“Kuna mengi ambayo yapo kwenye kilimo ila kikubwa ni pembejeo pamoja na namna ya usimamizi. Kuna wakati nakuwa sipo shamba nipo mjini wale wasimamizi ndiyo ambao wanashughulikia sasa hawawezi kwenda kwa spidi ambayo unahitaji jambo ambalo linaleta ugumu. “Kikubwa cha kujua ni kwamba changamoto haziepukiki kila sehemu zipo muhimu kupambana nazo.

SHAMBA KUNA MKWANJA KULIKO SOKA? “Mkwanja upo kwani hakuna kitu ambacho hakina faida ila kuhusu kuifananisha na soka hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa.

UKIACHA KILIMO UNADHANI UNAWEZA KUREJEA KWENYE UBORA WAKO? “Nina uhakika na kile ambacho nakifanya kwani kati ya vitu ambavyo huwa havipotei ni kipaji. Nikipata nafasi sehemu nina uhakika kabisa wa kufanya vizuri kwa sababu kipaji hakipotei.

KUNA TIMU YOYOTE UNA MAZUNGUMZO NAYO? “Hilo lipo kwani kuna timu ambazo zimekuwa zikiwasiliana nami na wengi wamekuwa wakionyesha kwamba wanahitaji huduma yangu, wakati ukifika nitajua najiunga na timu gani.

ULIKUWA UNAHUSISHWA KUREJEA AFRIKA KUSINI, MPANGO HUO UPOJE? “Kweli ilikuwa hivyo na kuna timu nyingi ambazo zimekuwa zikinihitaji ila kama ambavyo awali nimesema kwamba ni suala la muda. Ninajua changamoto za soka la Afrika na ukizingatia kwamba nimecheza huko na kwa sasa naendelea na mambo mengine.

NAMNA GANI UNAWASILIANA NA HAO WATU? “Dunia imeendelea na mambo yamebadilika sana kwa sasa, kuna mitandao ambayo inatufanya tuwe kwenye kijiji kimoja na wote tunafanya yale ambayo yanafanana hivyo sina mashaka katika hilo, ninafanya kwa wakati na hao ninawasiliana nao kwenye mitandao.

KIPI AMBACHO KINAKUPA UWEZO WA KUJIAMINI? “Uwezo binafsi na kujituma katika kazi ninayofanya, ndiyo yananifanya nakuwa kwenye ubora wangu muda wote.

UMECHEZA SIMBA NA YANGA KWA NYAKATI TOFAUTI KIPI UMEJIFUNZA?

“Zote ni timu kubwa na zina heshima yake hasa kutokana na kile ambacho wanakifanya, mashabiki wao ni wengi na zinajulikana duniani kucheza ndani ya hizi timu ni heshima na historia kwa kila mmoja anayetumikia ndani ya timu hizi. “Nimejifunza mengi namna ya kuishi na watu tofauti kwa nyakati tofauti na bado tumekuwa na furaha kwa wachezaji na viongozi pia.

LIGI YA BONGO UNAIONAJE? “Inazidi kuwa bora na ushindani ni mkubwa kwani kila timu inapambana kufikia malengo yake jambo ambalo linafanya kila timu ionyeshe ukomavu wake ndani ya ligi.

NAFASI YAKO KWENYE TIMU YA TAIFA? “Bado ni Mtanzania na ninaipenda nchi yangu wakati huu nimepewa nafasi kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Beach Soccer ni sehemu ya kuanzia na ukifika wakati nitaonyesha mengi makubwa.

NENO KWA WACHEZAJI WENGINE “Mpira huwezi kucheza muda wote hivyo ni muhimu kuwekeza kwenye masuala mengine ambayo yatafanya maisha kuendelea. Kwa wale ambao wapo kwenye kilimo wanapaswa watambue kuwa nacho ni kipaji,” anamaliza Dida

CHANZO: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic