November 2, 2019


MASHINDANO ya kimataifa kwa timu zetu zote nne msimu huu yamekuwa ni magumu kwa upande wa matokeo na hii inatokana na maandalizi kwa timu zetu kutokuwa ya uhakika.

Kutoka timu nne ambazo zilikuwa zinawakilisha nchi mpaka kubakiwa na timu moja ni hatua moja ngumu na mbaya kwa Taifa kwenye ulimwengu wa soka.

Wakati zinaanza kushiriki michuano ya kimataifa malengo ya timu zote ilikuwa ni kusonga mbele na kutimiza kiusawa majukumu ya Taifa.

Kazi ilianza kuwa ngumu kwa KMC ambayo iliishia hatua ya awali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kabla ya Simba ambao walikuwa wanajiamini kufanya makubwa kutolewa na UD do Songo uwanja wa Taifa.

Kiasi chake matumaini yalianza kuonekana kwa Azam FC ila nao nguvu zao zikaisha mapema kwenye hatua ya kwanza michuano ya kimataifa wao wakiwa kombe la Shirikisho.

Kwa sasa imebaki timu  moja pekee kutoka Tanzania ambayo ni Yanga nayo mwendo wake ni uleule wa kinyonga.

Inaumiza kwa mashabiki namna ambavyo timu inapata matokeo yasiyopendeza tena kwenye uwanja wao wa nyumbani hii ni mbaya.

Kama safari ya kwanza imeanza hivi safari ya pili itakuaje huenda mipango isipofanyika kuna makubwa zaidi ya haya tutashuhudia.

Ulimwengu umeshuhudia Yanga ikikubali kufungwa bao 1-0 uwanja wa CCM Kirumba na wapinzani wao Pyramids FC hii ni ngumu kwao hasa kutokana na mashindanohaya ya kimataifa yalivyo.

Kwa bara la Afrika mashindano megi ya kimataifa timu nyingi zimekuwa zikitamba nyumbani kutokana na uwepo wa mashabiki pamoja na kuzoea mazingira.

Mfano mzuri ni kwa Simba namna walivyopenya kwenye hatua ya robo fainali, walikuwa wakitoka nje wanapewa furushi la mabao kuanzia matatu na kuendelea ila wakirudi Taifa wanalipa kisasi.

Kwa matokeo ambayo Yanga imeyapata kwa sasa kinachotakiwa ni kujiaandaa upya kwa ajili ya mchezo wa marudio unaotarajiwa kupigwa nchini Misri kesho.

Timu inayojiandaa ndiyo inayoshinda jambo hili liwe kichwani mwa wachezaji na bench la ufundi wakijisahau tena huenda itakuwa mwisho wa safari yao kwani wapinzani wao wameonekana kujipanga na kucheza soka la kutulia.

Nilipata muda wa kutazama namna Waarabu walivyokuwa wakifanya ndani ya uwanja inaonyesha kabisa kile walichokipata walistahili kutokana na maandalizi makini.

Naskia kwa sasa shutma kwa kocha Mwinyi Zahera zimekuwa nyingi kwake kwa kuwa ameshindwa kupata ushindi, hapaswi kulaumiwa sana kwani mpira ni mchezo wa wazi na matokeo mashabiki wanapaswa wayapokee.

Kama kelele zitaendelea itakuwa rahisi kwa Yanga kupoteza dira ambayo walikuwa nayo awali hivyo ni suala la kuwa na subra na kufanya tena majaribio ya kutafuta matokeo chanya.

Kama mwalimu alifeli basi wachezaji wetu iliwapasa wajitahidi kupambana ndani ya uwanja kutafuta matokeo mazuri kwa ajili ya mashabiki na Taifa kiujumla.

Wachezaji wanajukumu la kuibeba timu hasa inapokuwa imezidiwa licha ya kutokuwa kwenye mpangilio mzuri, kuna wakati wa kucheza kwa mbinu na kuna wakati wa kucheza kutafuta matokeo kwa namna yoyote ile.

 Utulivu wa wachezaji ni jambo la msingi naona Yanga haikuwa kwenye utulivu jambo ambalo limewafanya wapate kadi nyingi za njano pia na ile kadi moja nyekundu ya beki Kelvin Yondani ni pigo.

Kuna umuhimu wa kukaa chini na wachezaji kuwaambia kuhusu nidhamu nje na ndani ya uwanja jambo ambalo litasaidia kupunguza adhabu ambazo hazistahili.

Wachezaji wana jukumu la kutulia na kupanga mikakati upya kwa ajili ya mchezo wa marudio kupata matokeo chanya ili isonge mbele.

Kama kila mmoja atajikatia tamaa itakuwa ngumu kupata ushindi ugenini, muda upo na mpira asili yake ni maandalizi na sio porojo.

Hakuna anayeshinda mdomoni ni lazima awe na mbinu kali na mikakati inayoeleweka kutafuta ushindi ndani ya uwanja jambo ambalo litasaidia kurejesha furaha kwa mashabiki.

Kila kitu kinawezekana endapo mashabiki wataungana na kuendelea kuwa kitu kimoja kwa sasa malumbano yawekwe pembeni bado matokeo ndio kinachohitajika.

Hakuna ambaye ataweza kufanikiwa endapo atakosa utulivu wa kuamua kile anachopenda kukifanya kwa usahihi na kukifuatili endapo kutakuwa na kelele.

Kila la kheri Yanga kuelekea mchezo wa marudio hakuna ambaye anaweza kuwarudisha nyuma endapo mtakuwa mmeamua kusonga mbele kwa pamoja. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic