MCHEZAJI SIMBA AMUUMIZA KICHWA NDAYIRAGIJE
KOCHA wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije alikuwa kama amepigwa ganzi baada ya daktari kumueleza baada ya mechi na Equatorial Guinea juzi kwamba; “Erasto Nyoni ameumia.”
Beki huyo aliyecheza kwa kiwango cha juu juzi Stars ikishinda mabao 2-1, atakaa nje kwa wiki kadhaa na ameshindwa kusafiri na kikosi cha timu hiyo kwenda Tunisia kucheza dhidi ya Libya kutokana na majeraha ya goti.
Ndayiragije ameliambia Spoti Xtra kuwa, Nyoni ni mhimili mkubwa kwenye kikosi hicho haswa alikuwa anamtegemea kwenye mechi ya Jumanne lakini atapata mbadala wa haraka kwa vile kikosi hicho ni imara na uteuzi ni panama.
“Wachezaji wote wapo vizuri isipokuwa Nyoni, ambaye tumemuacha kutokana na majeraha ya goti aliyoyapata kwenye mchezo dhidi ya Equatorial Guinea, tumemuacha ili afanyiwe vipimo na aendelee na matibabu,” alisema Ndayiragije, kocha wa zamani wa Mbao, KMC na Azam.
Kocha huyo raia wa Burundi, aliongeza kuwa, anayo njia mbadala ambayo ataitumia ili aweze kuziba pengo la mchezaji huyo wa Klabu ya Simba ambaye huenda akaiathiri timu hiyo kwenye kampeni za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwani ni tegemeo la Kocha Patrick Aussems.
0 COMMENTS:
Post a Comment