MPOKI FEDHA INAONGEA
FEDHA inaongea! Wakati baadhi ya wale wasiojituma kufanya kazi kwa bidii wakilia njaa, hali ni tofauti mno kwa mchekeshaji maarufu Bongo ambaye pia ni Mtangazaji wa Kipindi cha Ubaoni kinachoruka kupitia Radio Efm, Sylvester Mujuni ‘Mpoki’, Amani limedokezwa.
AWAVIMBIA JOTI, MASANJA
Mpoki au Bepari la Kihaya, anatajwa kuwavimbia wachekeshaji wenzake, Lucas Lazaro Mhuvile ‘Joti’ na Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ kwa kumiliki mijengo mingi zaidi yao kwa sasa.
Awali, Joti na Masanja ndiyo wachekeshaji waliotajwa kumiliki mijengo mingi na ya kifahari, lakini sasa upepo umebadilika.
Mpoki anasemekana kuwapiku wenzake hao ambao walikuwa wote kwenye Kundi la Orijino Komedi kabla ya kusambaratika, yapata miaka mitano iliyopita.
TWENDE MOROGORO
Ukiachilia mbali mijengo mitatu anayomiliki maeneo tofauti jijini Dar, ukiwemo ule wa kifahari wa Kibada-Kigamboni, Mpoki amewaacha midomo wazi baadhi ya wananchi maeneo ya Kigurunyembe katika Mtaa wa Mahedu Kata ya Kilakala mkoani Morogoro.
Wananchi hao waliliambia Amani kuwa, walipigwa na butwaa kumuona Mpoki ambaye ni jirani yao akiangusha mijengo minne kwa mpigo ndani ya muda mfupi huku wenyewe wakilia maisha magumu.
Hivi karibuni, baadhi ya wananchi wa mtaa huo walilivutia waya gazeti hili na kulitonya juu ya ishu hiyo ambayo ni gumzo maeneo hayo.
AMANI ENEO LA TUKIO
Baada ya kupokea taarifa hizo, Amani lilifika eneo la tukio na kushuhudia mijengo hiyo.
Amani lilipogonga hodi, lilipokelewa na mlinzi aliyejitambulisha kwa jina la Michael Samwel ambaye alikiri jamaa huyo kumiliki mijengo hiyo.
MLINZI AFUNGUKA
“Ni kweli nyumba hizi ni za Mpoki,” alisema mlinzi huyo na kutoa nafasi mwandishi wetu kuuliza swali kama analo;
Amani: Unamaanisha Mpoki huyu mchekeshaji au mwingine?
Mlinzi: Sasa wewe huamini? Hizi nyumba ni za bosi wangu Mpoki huyuhuyu unayemjua. Hizi nyumba amezijenga kwa lengo la kuzipangisha, kwani mwenyewe anaishi Dar. Kule (Dar) nako ana nyumba nyingine tatu na kijijini kwa wazazi wake kule Bukoba (mkoani Kagera) amewajengea nyumba.
MIL. 80?
Amani: Kila moja itakuwa imegharimu shilingi ngapi?
Mlinzi: Sina uhakika kabisakabisa, lakini kutokana na namba zilivyo ndani na matirio yaliyotumika, naweza kusema siyo chini ya shilingi milioni 80 kwa kila moja.
PICHA VIPI?
Baada ya kuziona nyumba hizo kwa ndani, Amani liliomba kupiga picha za nyumba hizo kwa ajili ya ushahidi ambapo ilibidi mlinzi amuulize kwanza Mpoki.
Mlinzi: Kuhusu kupiga picha, ngoja nimuulize, ila kila wikiendi huwa anakuja, hivyo njoo ljumaa au Jumamosi utamkuta.
Baada ya kuzungumza na Mpoki, mlinzi huyo alimruhusu mwandishi wetu kupiga picha nyumba hizo.
AMANI NA MPOKI
Ili kujiridhisha kama kweli nyumba hizo ni za Mpoki, Amani lilimuendea staa huyo hewani ambaye alikiri kumiliki nyumba hizo.
“Ni kweli hizo nyumba ni zangu. Nimezijenga kwa lengo la kuzipangisha kama kitega uchumi changu. Hizo nyumba ziko nne na ndani zina kila kitu.
“Kila nyumba moja kodi kwa mwezi ni shilingi laki tatu, hata wewe ukipata mtu, nijulishe nimpe mkataba,” alisema Mpoki.
WANANCHI
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaoishi kwenye mtaa huo walisema nyumba hizo zinasuasua kupata wapangaji kwa kile wanachodai kodi iko juu.
“Kwa sasa maisha ni magumu mno, kodi ya shilingi laki tatu ni kubwa mno kwa hapa Moro.
“Mpoki anatakiwa ajue kuwa maisha ya Dar na Moro ni tofauti, angefanya hata shilingi laki mbili.
“Jambo lingine ni kwamba, madalali wanasema ugumu unakuja pale ambapo mteja anakuta zina vyumba viwili vya kulala, sebule, choo na jiko, hivyo kama mtu ana familia ya watoto wakubwa wa kike na kiume inakuwa mtihani,” alisema Ombeni Masawe ambaye ni jirani wa Mpoki.
NYUMBA NYINGINE ZA MPOKI
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba, mbali na nyumba hizo, jijini Dar, jamaa huyo anamiliki nyumba tatu za kifahari ambapo moja ipo Kigamboni, nyingine ipo Kinyerezi (Tabata) na Kijichi.
JOTI NA MASANJA
Kwa upande wake, Joti anamiliki anamiliki nyumba ya ghorofa moja iliyopo Kibada- Kigamboni Dar ambayo inakadiriwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 300.
Masanja yeye anamiliki nyumba za maana, moja ni ya ghorofa moja ambayo ipo Tabata, nyingine Kigamboni na nyumbani kwao, Mbarali, Mbeya.
WOTE WAMESOTA
Mpoki, Joti na Masanja, wote walianzia kwenye msoto mtaani ambapo majina yao yalikuwa zaidi walipokuwa wakifanya Kipindi cha Original Comedy na wenzao, Isaya Mwakilasa ‘Wakuvwanga’, Alex Chalamila ‘MacRegan’ na Joseph Shamba ‘Vengu’ kilichokuwa kikirushwa kupitia East Africa Television (EATV).
Baadaye walihamia TBC1 wakitumia jina la Orijino Komedi kabla ya kusambaratika rasmi mwaka 2014.
Mbali na shoo yao kwenye televisheni kutoonekana kwa muda wa takriban miaka mitano sasa, mastaa hao wamejiongeza na kuwa kivutio kwa kufanya matangazo makubwa huku kila mmoja akiendelea kuuza vichekesho vyake kupitia mitandao ya kijamii na kujiingizia vipato vyao.
0 COMMENTS:
Post a Comment