WATOFAUTIANA! Ndivyo inavyoonekana baada ya hivi karibuni Tanasha Donna ambaye ni mzazi mwenza na staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kutangaza uwepo wa sherehe ya 40 ya mtoto wao, Nasibu Junior lakini mama mkwe wake, Sanura Kassim ‘Sandra au mama D’ ameibuka na kusema hakuna kitu kama hicho, Risasi Jumamosi linakupa habari kamili.
ILIKUWAJE?
Awali, Tanasha kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Instagram alitangaza kuwa Novemba 26, mwaka huu itakuwa ni siku ya kusherehekea 40 ya mtoto wao huyo ikiwa ni baada ya kutimiza siku arobaini Novemba 11, mwaka huu.
“My happiness in one pic. We celebrate my son’s 40 days on the 26th (though he turned 40 on the 11th) LEGGO!” aliandika Tanasha maneno hayo chini ya picha yake akiwa amembeba mwanaye akimaanisha kuwa watafanya sherehe Novemba 26 licha ya kwamba tayari mtoto alishafikisha siku arobaini Novemba 11.
RISASI NA MAMA D
Gazeti la Risasi Jumamosi liliingia kazini na kutaka kujua maandalizi ya sherehe hiyo yakoje kwani presha yake mitandaoni ilikuwa imepanda kama yote ambapo mama D alipopatikana, akasema hakuna sherehe.
Mama D alisema hiyo sherehe hakuna kwa sababu tayari Novemba 11, mwaka huu mtoto alishatolewa na kufanyiwa dua huku wakichinja mbuzi na kupika vyakula mbalimbali na kwamba walialikwa watu wachache tena wale wa karibu.
KWA NINI HAKUNA SHEREHE?
Mama D alisema siku hizi hawana mbwembwe na wala hawazitaki hivyo mambo ya kufanya sherehe kama zamani hakuna kwani kwanza mwanaye (Diamond) amekua kiakili hivyo mambo ya kuchezea pesa tena hakuna, kwa sasa anafanya mambo ya maana.
“Pamoja na hilo pia hiyo sherehe haiwezi kufanyika kwa sababu Diamond yupo nchi ya mbali huko (Cameroon) kwa hiyo hata hakuna cha maandalizi wala nini maana sherehe haipo.
ETI ULIKUWA UTOTO…
“Unajua zamani Diamond ile kufanya sherehe za mbwembwe za kumtoa mtoto 40 ulikuwa ni utoto pia wale ilikuwa ni watoto wa kwanza kwa hiyo sasa hivi huyu ni wa nne mpaka hapo ameshazoea yaani.
“Si unajua mtu ukipata kitu kwa mara ya kwanza inavyokuwa? Ndivyo ilivyokuwa kwa Diamond lakini kwa sasa ameshazoea kwa hiyo mambo ya sherehe hakuna maana hatuna pesa,” alisema mama D.
AMZUNGUMZIA TANASHA
Kwa upande mwingine mama D alisema Tanasha ni mkwe mzuri na anampenda kwani anajielewa na ana heshima pia.
AHAMIA KWA TANASHA
Hakuishia hapo, mama D alisema kwa sasa amehamia nyumbani kwa Tanasha anakoishi na mpenzi wake Diamond maeneo ya Mbezi Beach ili amsaidie kumlea mtoto.
“Nimeama kwangu Madale na kuhamia kwa Tanasha ili niweze kumlea mjukuu wangu mpaka akuekue maana sitaki mkwe wangu apate shida, kule Madale nimemwacha mume wangu Shamte na mlinzi,” alisema mama D.
NDOA LINI?
Alipoulizwa ndoa ya mwanaye na Tanasha itakuwa lini, mama D alisema hawezi kuanika gazetini kwa kuwa watu wa muhimu kupewa taarifa ni mashehe watakaoenda kuwafungisha ndoa.
Kuhusu kama Tanasha anafaa kuolewa na Diamond mama huyo alisema hawezi kumchagulia mwanaye huyo mwanamke wa kuoa bali anatakiwa kuchagua mwenyewe hivyo kila atakayepelekwa kwake kama mkwe anampokea hawezi kuwafukuza.
TUJIKUMBUSHE
Diamond na Tanasha walijaliwa kupata mtoto wa kiume hivi karibuni ikiwa ni mtoto wa nne kwa mwanamuziki huyo aliyezaa na wanawake watatu tofauti huku kwa Tanasha akiwa ndiyo mtoto wake wa kwanza.
MHARIRI
Kutokana na kutofautiana huko, tusubiri Novemba 26, mwaka huu siku ambayo Tanasha ameitangaza kama siku ya sherehe ili kuweza kujua mbivu na mbichi za ishu hii!
0 COMMENTS:
Post a Comment